Merkel akutana na Tsipras | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.03.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Merkel akutana na Tsipras

Mazungumzo ya Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel na Waziri Mkuu wa Ugiriki, Alexis Tsipras, yamemalizika huku kukiwa na dalili ndogo za kupatikana suluhu ya mvutano uliopo kuhusu mpango wa uokozi wa Ugiriki.

Kansela Angela Merkel na Waziri Mkuu wa Ugiriki, Alexis Tsipras

Kansela Angela Merkel na Waziri Mkuu wa Ugiriki, Alexis Tsipras

Kansela Merkel na Tsipras walikuwa na mazungumzo ya kina yaliyodumu kwa muda wa saa tano mjini Berlein, ambayo yameonekana kuwa ya kujenga katika mazingira ya kirafiki, huku wakisisitiza nia yao ya kuondoa mvutano uliopo kati ya serikali zao. Viongozi hao wamezungumzia kuhusu hali ya kiuchumi ya Ugiriki, utaratibu wa Umoja wa Ulaya na mustakabali wa ushirikiano kati ya Ugiriki na Ujerumani.

Akizungumza katika mkutano wake na Tsipras na waandishi wa habari, Merkel amesema licha ya tofauti zilizopo sasa kuhusu mpango wa uokozi kuisaidia Ugiriki isifilisike kiuchumi pamoja na masuala mengine kadhaa, nchi zao zimeendelea kubakia washirika wa karibu, huku wakiwa na uhusiano mzuri kisiasa na kwamba uhusiano kati ya nchi hizo mbili ni muhimu.

''Nataka kusisitiza wazi kuwa Ujerumani ina uhusiano wa karibu na kirafiki na Ugiriki pamoja na watu wa Ugiriki. Kuna watu wengi wanaoishi Ujerumani ambao wana asili ya Kigiriki,'' alisema Merkel.

Tsipras akiwa na maafisa wa Ujerumani

Tsipras akiwa na maafisa wa Ujerumani

Kwa upande wake Tsipras ambaye anazuru rasmi Ujerumani kwa mara ya kwanza tangu aingie madarakani mwezi Januari mwaka huu, ameonyesha kuwa nchi yake bado inatafuta masharti nafuu yatakayosaidia kuunusuru uchumi wake.

Tsipras kuzingatia mafanikio yaliyopatikana

''Hatutaki kuharibu mafanikio yaliyopatikana miaka mitano iliyopita. Tunahitaji kutekeleza mageuzi ambayo awali serikali zilizotangulia, zilishindwa kuyafikia, mageuzi ya kodi, hatua za kupambana na rushwa pamoja na ukwepaji wa kulipa kodi,'' alifafanua Tsipras.

Uhusiano kati ya Ujerumani na Ugiriki uliingia dosari tangu Tsipras na serikali yake inayoongozwa na chama cha Syriza kuingia madarakani na kuendeleza sera yake ya kupinga vikali masharti magumu ya kubana matumizi.

Kansela Merkel amesema uamuzi wowote kuhusu suluhisho la matatizo ya kifedha yanayoikumba Ugiriki utapatikana tu kutoka kwa mataifa yote yanayotumia sarafu ya Euro. Wiki ijayo serikali mpya ya Ugiriki inatarajia kuwasilisha orodha yake ya mageuzi ya kiuchumi.

Makumbusho ya mauji ya Wayahudi, Berlin

Makumbusho ya mauji ya Wayahudi, Berlin

Asubuhi hii, Tsipras atakutana na viongozi wa chama cha upinzani cha siasa kali za mrengo wa kushoto-Die Linke, Katja Kipping na Gregor Gysi, ambapo majira ya mchana anatarajiwa kukutana na viongozi wa chama cha Kijani, Cem Özdemir na Simone Peter.

Baadae, waziri huyo mkuu wa Ugiriki, atatembelea makumbusho ya mauwaji yaliyofanywa na utawala wa Wanazi dhidi ya Wayahudi, Holocaust mjini Berlin, hatua ambayo inaelezwa huenda ikatilia mkazo madai ya serikali yake ya kutaka kulipwa fidia, ambayo Tsipras ameyaita kama ''suala la kimaadili.''

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/DPAE,RTRE
Mhariri: Iddi Ssessanga

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com