Meli ya Kichina yenye kubeba silaha kwa Zimbabwe huenda itarudi | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.04.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Meli ya Kichina yenye kubeba silaha kwa Zimbabwe huenda itarudi

Wakati matokeo ya uchaguzi wa Zimbabwe bado hayajatolewa kulikuwa na habari kuhusu meli kutoka China inayobeba silaha zilizoagiziwa kutoka Zimbabwe na ambayo ilizuiliwa katika bandari na nchi kadhaa za Afrika Kusini.

default

Meli ya kichina inayobeba silaha na risasi kwa Zimbabwe

Msemaji wa wizara ya masuala ya kigeni wa China alisema kwamba kampuni ya “China Ocean Shipping Company” ambayo inamiliki meli husika iliamua kuirudisha meli kwa sababu Zimbabwe haiwezi kupokea kwa wakati tani hizo 77 za silaha na risasi zinazobebwa na meli hiyo. Kupelekwa na meli hiyo yenye silaha na risasi hadi Zimbabwe wakati mzozo wa kisiasa haujatatuliwa kulizusha malalamiko dhidi ya China, miongoni wa walioyatoa ni rais wa Zambia, Levy Mwanawasa, na serikali ya Marekani.


Akijibu ukosoaji kutoka pande nyingi za kimataifa, msemaji wa serikali ya China alisema biashara hii ni ya kawaida na kwamba silaha hizo ziliagizwa na serikali ya Robert Mugabe mwaka uliopita, kwa hiyo hazihusiani na uchaguzi. Taarifa hizo zimepatikana wakati ambapo meli hiyo ilikuwa njiani kuelekea Angola ikitafuta bandari kupakua silaha hizo.


Chama cha upinzani cha “Movement for Democratic Change” MDC, leo hii kimesema kwamba kinaamini silaha hizo zitatumika kuwaua raia wasio na makosa. Chama hiki kimesema awali kuwa wanachama wake 10 waliuawa katika ghasia zilizotokea baadha ya uchaguzi wa March 29. Serikali ya Zimbabwe lakini ilitetea haki yake ya kuagiza silaha, kama alivyosema waziri wa sheria, Patrick Chinamasa:


Kiongozi wa chama cha MDC, Morgan Tsvangirai, alisema hawawapingi Wachina, lakini anapinga hatua ya kupeleka silaha kwa serikali ya Zimbabwe ambazo zitatumika kukandamiza wananchi. Tsvangirai yuko sarafini katika nchi mbalimbali za Kiafrika kuomba uungaji mkono katika mzozo wa kisiasa nchini mwake. Alipokutana na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki Moon, mjini Accra, Ghana, Tsvangirai alitoa mwito kwa Umoja wa Mataifa kuingilia kati nchini Zimbabwe. Alisema: “Tunakabiliwa na hali ngumu sana kwa binadamu kwa sababu ya matumizi ya nguvu yanayotokea na kwamba kuna watu walioacha makwao na kutafuta ukimbizi katika ofisi zetu mikoani.”


Ban Ki Moon leo hii alisema kutochapishwa kwa matokeo ya uchaguzi hadi sasa wiki tatu baada ya kupiga kura ni hali isiyokubalika na aliongeza kusema kwamba ataishurutisha serikali ya Zimbabwe na tume ya uchaguzi kuchapisha matokeo haraka iwezakanavyo. Serikali ya Zimbabwe ilitaka kura zihesabiwe upya.


Wakati huo huo, viongozi wa kanisa nchini Zimbabwe walitoa mwito kwa jumuiya ya kimataifa kuingilia kati Zimbabwe ili kuzuia nguvu inayotumiwa kuweza kufikia kiwango cha mauaji ya kimbari. Katika taarifa yao ya pamoja, viongozi hawa wa kanisa wanaendelea kueleza kuhusu mashambulio yanayotokea nchini kote dhidi ya watu, familia au makundi ya watu wa jamii fulani kwa sababu wanaunga mkono chama fulani.

 • Tarehe 22.04.2008
 • Mwandishi Dreyer, Maja
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Dmqu
 • Tarehe 22.04.2008
 • Mwandishi Dreyer, Maja
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Dmqu
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com