Mazungumzo ya amani ya Sudan huko Qatar | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.11.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mazungumzo ya amani ya Sudan huko Qatar

Wapatanishi wanatumai kuwa mazungumzo rasmi kuanza wiki hii

Rais wa Sudan Omar Hassan Al-Bashir.

Rais wa Sudan Omar Hassan Al-Bashir.

Wapatanishi wa mazungumzo ya amani nchini Sudan yanayofanyika huko Doha, Qatar, wanatumai kuwa wataanzisha angalau mazungumzo rasmi ya amani baina ya serikali ya Sudan na waasi wa Jimbo la Darfur, wiki hii.

Waziri wa Serikali katika Ushirikiano wa Kimataifa, Ahmed al-Mahmud amesema makundi ya waasi ya Darfur na serikali ya Sudan hayatafanya mazungumzo ya kina hadi baada ya sikukuu ya Waislamu ya Eid al-Fitr inayotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 26 ya mwezi huu wa Novemba.

Waziri Mahmud ameongeza kuwa Qatar ina tumain kwamba pande hizo mbili zitaanzisha mazungumzo rasmi sambamba na mkutano wa siku tano unaofanyika nchini humo na kuwajumuisha wajumbe wa vyama vya kiraia, wakiwemo wawakilishi wa wakaazi wa Jimbo la Darfur wanaoishi nchi za nje.

Msimamo wa waasi

Miaka mitatu iliyopita, waasi hao wamegawanyika katika karibu makundi 20, hivyo kusababisha ugumu zaidi katika juhudi za kumaliza migogoro nchini Sudan. Mwezi Februari mwaka huu kundi kubwa lenye silaha la Justice and Equality Movement-JEM, walitiliana saini makubaliano na serikali ya Khartoum katika kile kinachoaminika kitafungua njia ya kufanyika mazungumzo zaidi. Lakini makundi mengine makubwa ya waasi yamekataa kushiriki katika mazungumzo hayo ya Doha yanayoonekana kuwa kama ya bandia, huku kundi la JEM nalo likisema hakuna haja ya kushiriki katika mazungumzo hayo kama hakuna ushirikiano kutoka katika makundi mengine ya waasi.

Kundi la JEM lilikubali kurejea katika meza ya mazungumzo na serikali ya Khartoum yaliyovunjika baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita-ICC kutoa waranti wa kukamatwa Rais Omar al-Bashir wa Sudan kwa tuhuma za kuhusika na uhalifu wa kivita.

Juhudi za Marekani

Tangu wakati huo, mjumbe maalum wa Marekani, Scott Gration amekuwa akiendelea na juhudi za kufufua mazungumzo hayo. Katika kusisitiza hilo, Bwana Gration wiki hii anatarajiwa kwenda Khartoum na Darfur katika kuendeleza juhudi za kidiplomasia za kuondoa hali tete katika eneo hilo. Mjumbe huyo maalum wa Marekani atakutana na wajumbe wa chama cha NCP cha rais Bashir na kundi la zamani la waasi la Sudan People's Liberation Movement-SPLM, ambayo kwa pamoja mwaka 2005 yalisaini makubaliano ya kumaliza vita vilivyodumu kwa zaidi ya miaka 20.

Umoja wa Mataifa umesema hadi watu 300,000 waliuawa na wengine milioni 2.7 kuyakimbia makaazi yao tangu kuzuka kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe ambapo waasi walikuwa wakipingana na serikali ya Khartoum inayoongozwa na Waarabu wengi mwezi Februari, mwaka 2003. Hata hivyo serikali ya Sudan inasema kuwa watu waliouawa katika mapigano hayo ni 100,000.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE)

Mhariri: M. Abdul-Rahman

 • Tarehe 18.11.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KaQJ
 • Tarehe 18.11.2009
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/KaQJ
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com