1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa ulinzi wa Ufaransa na Urusi kukutana

21 Desemba 2015

Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian anakutana na mwenzake wa Urusi, Sergei Shoigu katika juhudi za kuongeza ushirikiano kwenye mapambano dhidi ya kundi lenye itikadi kali la Dola la Kiislamu-IS nchini Syria.

https://p.dw.com/p/1HR1E
Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Jean-Yves Le Drian
Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Jean-Yves Le DrianPicha: Reuters/D. Alvarez

Akizungumza kabla ya kuanza ziara yake, Le Drian amewaambia waandishi wa habari kwamba mazungumzo hayo kati yake na Shoigu yatakayofanyika kwenye mji mkuu wa Urusi, Moscow, yataangazia pia namna Ufaransa na Urusi zinavyoweza kupeana taarifa za kijasusi zinazohusiana na shughuli za kigaidi za IS.

Amesema watajadiliana jinsi ya kuyashughulikia makundi ya kigaidi na ambavyo Urusi inaweza kuongeza mashambulizi yake ya anga dhidi ya IS, ambalo ni kundi adui kwa Ufaransa.

Mataifa ya Magharibi yamelalamika kwamba kimsingi Urusi imekuwa ikiwashambulia waasi kwa mabomu, wakiwemo waasi wenye msimamo wa wastani ambao wanatishia utawala wa Rais Bashar al-Assad, kuliko kupambana zaidi na IS.

Lakini Le Drian amesema ana matumaini Ufaransa pia itaweza kushirikiana na Urusi katika maeneo mengine.

Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Sergei Shoigu
Waziri wa Ulinzi wa Urusi, Sergei ShoiguPicha: picture-alliance/AP Images

Amefafanua kwamba kuna watu wengi wanaozungumza Kirusi ndani ya kundi la IS, ambao wanaweza kuwa msaada katika kupatikana taarifa, na vivyo hivyo wanaweza kutoa taarifa kwa wanaozungumza Kifaransa. Amesema hatua ya kupeana taarifa za kijasusi inahitaji ushirikiano wa pande zote.

Mazungumzo yatahusu pia kuepuka muingiliano katika anga

Le Drian na Shoigu pia watajadiliana njia za kuepuka muingiliano wowote ule katika anga nchini Syria, kati ya Urusi na Ufaransa. Hivi karibuni Ufaransa ilipeleka manowari inayobeba ndege za kijeshi za Ufaransa, Charles de Gaulle, katika Ghuba ya Uajemi, ikiwa na ndege 26 za kivita ndani yake, kwa ajili ya kufanya mashambulizi dhidi ya IS nchini Iraq na Syria.

Ndege nyingine pia zimepelekwa Jordan na katika Umoja wa Falme za Kiarabu. Mazungumzo ya mawaziri hao wawili wa ulinzi yanafuatia ziara iliyofanywa mwezi uliopita na Rais Francois Hollande wa Ufaransa, ambapo aliomba msaada kutoka kwa mwenzake wa Urusi, Vladimir Putin, wa kuongeza mashambulizi zaidi dhidi ya IS kutokana na mashambulizi ya kigaidi ya Paris ya Novemba 13.

Viongozi hao wawili walikubaliana kuimarisha na kuratibu mashambulizi, hasa kwa kulenga njia za kusafirisha biadhaa za mafuta, ambazo zimekuwa zinalifadhili kundi la IS pamoja na kubadilishana taarifa za kijasusi.

Rais Francois Hollande & Rais Vladimir Putin
Rais Francois Hollande & Rais Vladimir PutinPicha: Reuters/S. Chirikov

Kwa mujibu wa duru kutoka ndani ya jeshi la Ufaransa, tangu wakati huo, mashambulizi ya anga ya Urusi dhidi ya IS yameongezeka, lakini asilimia 80 ya mashambulizi yao yamebakia dhidi ya waasi wa Syria.

Huo ni mkutano wa pili kati ya Le Drian na Shoigu, kutokana na uhusiano kati ya mawaziri hao wawili kusimamishwa kwa miaka miwili, baada ya Urusi kulichukua eneo la Crimea kutoka kwa Ukraine mwaka 2014.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman