Matumaini ya ufumbuzi wa amani Syria badala ya vita | Magazetini | DW | 16.03.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Matumaini ya ufumbuzi wa amani Syria badala ya vita

Mabadiliko katika msimamo wa Marekani kuelekea rais Basha al Assad wa Syria,mazungumzo ya mradi wa kinuklea wa Iran nchini Uswisi,na kupungua biashara ya nje ya silaha za Ujerumani ni miongoni mwa mada magazetini

default

Mapigano Kati ya vikosi vya serikali na waasi huko Aleppo nchini Syria

Tuanzie Mashariki ya kati ambako matumaini yameanza kuchomoza ya pengine kupatiwa ufumbuzi wa kisiasa mzozo wa Syria,miaka minne baada ya vita kuripuka na kuiteketeza moja kwa moja nchi hiyo.Matumaini hayo yamezushwa na waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry.Gazeti la "Landeszeitung" la mjini Lüneburg linaandika:"

Ni kweli kwa hivyo.Washington inaelezea utayarifu wa kuzungumza na yule aliyekuwa kwa muda mrefu akiangaliwa kama mtawala wa kiimla Bashar al Assad.Kwa mara nyengine tena Marekani inajikuta ikikabiliwa na magofu ya sera zake za Mashariki ya kati.Hata si zamani hivyo Marekani ilipania kumuona Assad aking'oka madarakani,bila ya kutilia maanani uungaji mkono wa dhati wa watu wa madhehebu ya shia,wafuasi wa chama tawala cha kijamaa,Iran,Urusi na China.Tamko la waziri wa mambo ya nchi za nje wa marekani John Kerry kwamba sasa mazungumzo ya ufumbuzi yanawezekana,linauma mtu akizingatia limetolewa baada ya watu laki mbili na 20 elfu kupoteza maisha yao.Kwanza Marekani iliwapa nguvu bila ya kutaka wafuasi wa makundi ya itikadi kali,ilipoachia wapatiwe fedha kutoka mataifa ya Ghuba.Hivi sasa yadhihirika nchi za magharibi zinamhitaji Assad ili kupambana na kitisho cha tawala za kidini-Khalifa.

Jee duru hii ya mazungumzo itafanikiwa?

Mazungumzo kuhusu mradi wa kinuklea wa Iran yanaanza upya katika mji wa Lausane nchini Uswisi.Ni duru ya mwisho ya mazungumzi yaliyoanza miezi 18 iliyopita na ambayo pindi yakifanikiwa,yanaweza kuibadilisha sura ya mambo katika eneo la Ghuba.Gazeti la "Lausitzer Rundschau" linaandika:

"Zaidi ya hayo Iran ni nchi iliyoendelea zaidi katika eneo hilo.Ikiwa badala ya kusumbuliwa na vikwazo vikali vya kiuchumi,itaachiwa kuwavutia wawekezaji na kunawiri kiuchumi,baasi hapo Iran itazidi kun´gara.Na hata wezani wa kisiasa katika eneo hilo utabadilika."

Biashara ya nje ya silaha za Ujerumani yapungua

Na hatimae ripoti ya taasisi inayochunguza masuala ya Usalama yenye makao yake makuu mjini Stockholm-Sipri imechapisha ripoti yake ya mwaka inayoonyesha Uchina imeipita Ujerumani katika biashjara ya nje ya silaha katika kipindi cha miaka minne iliyopita.Gazeti la "Südwest Presse" linaandika:"Biashara ya nje ya silaha za Ujerumani imepungua mno miaka ya nyuma.Hizo ni habari za kufurahisha bila ya shaka.Hata hivyo sekta hiyo inayochusha ya kiuchumi inasalia kuitia dowa jamii nchini Ujerumani.Mwenye kuuza silaha ni mkosa kwasababu anachangia katika mateso na mauwaji ya binaadam.Katika dibaji ya sheria msingi ya Ujerumani imeandikwa "Umma wa Ujerumani umedhamiria kutumikia amani ya dunia.Ni kauli tukufu hiyo ingawa inageuka potofu kwa wale ambao maisha yao hayendi bila ya matumizi ya nguvu,zikitumiwa silaha zilizotengenezwa Ujerumani

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com