Matatizo ya kiuchumi katika Zimbabwe | NRS-Import | DW | 27.01.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

NRS-Import

Matatizo ya kiuchumi katika Zimbabwe

Maisha yanazidi kuwa magumu huko Zimbabwe

default

Rais Robert Mugabe wa Zimbabwe(kushoto) akipeana mkono na kiongozi wa MDC, Morgan Tsvangirai, baada ya kufikia muwafaka wa kuunda serekali ya Umoja wa taifa katikati ya mwaka jana

Matokeo ya mkutano wa kilele wa karibu ni wa Jumuiya ya Uchumi ya Kusini mwa Afrika, SADC, juu ya mzozo wa Zimbabwe, yamekivunja moyo chama cha upinzani cha MDC kinachoongozwa na Morgan Tsvangirai. Viongozi wa jumuiya hiyo ya nchi 15 wametaka Morgan Tsvangirai aapishwe kamwa waziri mkuu wa Zimbabwe ifikapo Februari 11, na kwamba vyama vya ZANU-PF cha rais Mugabe na MDC vigawane katika kuidhibiti wizara ya mambo ya ndani ya nchi hiyo, jambo lililokuwa linabishaniwa, kila chama kikiikamata wizara hiyo kwa miezi sita. Lakini baada ya mkutano huo uliofanyika Pretoria, MDC ilitoa kwa haraka taarifa baada ya kutolewa taarifa ya SADC kikiweka wazi kwamba kimevunjika moyo, hivyo kuna uwezekano kwamba mkwamo huo wa kisiasa utaendelea , huku Wa-Zimbabwe wakikabiliana na shida za kiuchumi zinazozidi...

Kipindupindu, mfumko wa bei za bidhaa usiokuwa na mipaka, ugonjwa wa ukimwi, yote hayo hayatoi sura ya mustakbali mzuri. Zimbabwe imemalizika, iko sakafuni, na pia wananchi wake...

Askofu wa kikatholiki, Wilson Mugabe, alilalamika hivyo katika Mkutano wa Mashikamano na Watu wa Zimbabwe uliofanywa Johannesburg na ambao uliomba msaada wa kimataifa. Alisema shida zilizokuweko nchini mwake hazistahamiliki tena. Wajina huyo wa mdikteta Robert Mugabe, kwa mujibu wa usimulizi wake,alikuwa karibu apoteze maisha yake alipokimbia Zimbabwe kwenda Afrika Kusini:

" Kwa hisani zenu, tusikilizeni, tumeteseka vya kutosha."

Wazimu unaoonekana Zimbabwe hauwezi tena kuelezeka, katu hauwezi kuhesabika. Idadi ya watu waliokufa kwa ugonjwa wa kipindupindu imepanda kwa asilimia 25 mnamo mwa wiki na kufikia 27,000. Wale walioambukizwa na ugonjwa huo inafikia 50,000. Pia athari za ugonjwa huo kwa nchi jirani sasa zimekuwa kubwa, licha ya mwanzoni kufifirishwa. Msumbiji imeripoti kwamba watu 80 wamekufa katika nchi hiyo na 10,000 wameambukizwa; Afrika Kusini wamekufa watu 30 na 3,000 wamebakia wagonjwa kutokana na janga hilo. Pia Kimeta, Malaria na kifua kikuu pamoja na homa ya mapafu ni magonjwa yanayotapakaa kutokana na kuzorota mfumo wa afya.

Katika kila kona ya njia utaona watu mabarabarani wakiuza vitu vyao vya kibinafsi. Katika kila Wa-Zimbabwe watano, basi wanne hawana ajira na wanauza kila kitu walicho nacho. Dola ya Kimarekani bei yake inafikia dola bilioni 10 za Zimbabwe, na kima cha mwishoni cha mfumko wa bei katika nchi hiyo kimefikia asilimia milioni 231. Kila kitu kinahesabiwa kwa dola ya Kimarekani, Peter mapunda, mhasibu mwenye umri wa miaka 33, aliliambia shirika la televisheni la Kijerumani, ARD. Alisema hawezi sasa kumudu gharama za usafiri kwendea kazini:

" Keshia hana fedha za kubadilisha, unampa fedha, mara anatoweka, humuoni. Mtu hawezi kujuwa vima vya ubadilishanaji wa sarafu, na wengi kati yetu sisi hawana fedha za kigeni. Ukihesabu vipato vyetu, ni chini ya dola za Kimarekani tano kwa mwezi, na mimi angalau nahitaji si chini ya dola mbili kuniwezesha kuja kazini. Tunajiuliza, wapi tutapata fedha."

Katika soko la njiani, bila huruma, sarafu inayotawala ni ile ya dunia- dola ya Kimarekani. Mayai thalathini yanagharimu dola tano hadi nane, gunia la viazi dola kumi na tano. mikebe sita ya biya kwa dola kumi.

"Watu wengi wameyaacha maisha yao katika mikono ya Mwenyezi Mungu. Hatuna matumaini tena kwa Zimbabwe, hatujuwi nini kitakachojiri kwetu, tumepoteza matumaini yote."

Huyo ni Letwin Mugavazi, msanii wa uchoraji aliye na umri wa miaka 38, lakini kwa muda mrefu sasa anapigana na maisha. Vipi ataweza kuwalea watoto wake wawili?

Shule zitachelewa kufunguliwa kwa wiki baada ya mapumziko ya kiangazi. Hivi sasa zimebaki zimefungwa, kwani waalimu hawawezi kusomesha. Letwin Mugavazi anasema kwamba kusambaratika mfumo wa elimu nchini Zimbabwe hakutokani tu na utawala wa Mugabe, lakini pia umesababishwa na chama cha upinzani cha MDC cha Morgan Tsvangirai, ambacho kilishinda katika uchaguzi wa mwezi Machi mwaka jana, lakini hadi sasa hakijakubali kuingia katika serekali ya mpito ya pamoja na Robert Mugabe.

" Watoto wetu hawaendi tena shule. Katika nusu au robo tatu ya mwaka jana, shule zilifungwa, kwa vile hakujakuweko waalimu na hakujakuweko chakula shuleni. Kila mahala, watu wanalalamika. Vyama hivi viwili si viamini tena."

Pia vyuo vikuu na shule za mafunzo zimefungwa, vingine tangu miaka miwili sasa. Mwanafunzi wa uandishi wa habari, Edward Khupe, aliye na umri wa miaka 21 na ambaye karibu ilikuwa afanye mtihani wake:

"Mateso haya yote yanatokana na siasa mbovu. Chama cha ZANU-PF cha Robert Mugabe na kile cha MDC cha Morgan Tsvangirai vimeifanya nchi nzima kuwa mahabusu. Inabidi vyama hivyo viwili vikae pamoja na mwishowe kuja na suluhisho. Hatuwezi kungojea msaada wa kimataifa. hHawa jamaa wanakaa tu na kuzungumza. Suluhisho lazima litokee ndani nchini, kutoka kwetu wenyewe Wa-Zimbabwe."

Mwanafunzi wa tiba, George Chisvo, aliye na umri wa miaka 26, haridhiki na mambo yalivyo. Karibu ilikuwa afanye mtihani wake wa mwisho, lakini kitivu cha tiba katika chuo kikuu chake kimefungwa tangu mwezi Oktoba. Na pindi chuo kikuu hicho cha Zimbabwe kitafunguliwa baada ya mapumziko ya muhula wa kiangazi, basi atatakiwa alipe karo, tena kwa dola za Kimarekani. Pia George anahisi ni wanasiasa wanaokorofisha mambo na anawalaumu mahasimu hao wawili wa kisiasa, Mugabe na Tsvangirai, kuwa ndio thamana ya mzozo ulioko. Lakini, Chisvo anasema:

" Binafsi, hasa namuona Mugabe ndie anayebeba dhamana kubwa. Lazima tujuwe wazi kwamba watu wa Mugabe hawajali juu ya maslahi ya wananchi, wanan'gan'gania madaraka ili kuiibia nchi. Na hali hii imekuweko si chini ya miaka kumi sasa. Napata taabu kufikiria kwamba itabidi kushirikiana na watu hawa ili kuukiuka mzozo huu. Ingekuwa bora, kwamba isiwe lazima tena kushirikiana na watu hawa au kufanya kazi chini ya serekali yao. Kwa kweli nisingefurahi hadi pale nitakapowaona wanaishia gerezani."

Yaonesha mazungumzo ya mwishoni baina ya Rais Robert Mugabe na Morgan Tsvangirai yameshindwa kutoa matunda, wote wawili wanabakia wakaidi, wakishikilia misimamo yao. Mikutano maalum ya kilele ya Umoja wa Afrika na shirika la mkoa la SADC, yote haijafua dafu. Hata bibi Graca Machel, mke wa rais wa zamani wa Afrika Kusini, Nelson mandela, na ambaye ni mwanachama wa baraza la wazee wa busara, ambalo ndani yake wamo Mabwana Mandela, Askofu Desmond Tutu, Jimmy Carter na Kofi Annan, yaonesha wote wametokwa na matumaini. Akikunja mikono yake, Bibi Graca Machel alisema:

"kwa muda mrefu tumewaamini viongozi wetu, na ni wakati sasa tunawaambia viongozi hao kwamba tunayaweka maisha ya wale wote waliokufa, na wale wanaoendelea kufa leo na kesho, tunayaweka maisha ya watu hao mikononi mwao. Lazima wabebe dhamana" • Tarehe 27.01.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Gh2h
 • Tarehe 27.01.2009
 • Mwandishi Miraji Othman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/Gh2h
Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com