Mashambulizi ya treni yawaua watu 66 nchini India | Matukio ya Kisiasa | DW | 19.02.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mashambulizi ya treni yawaua watu 66 nchini India

Baada ya mashambulizi ya mabomu dhidi ya treni iliokuwa ikisafiri kati ya Pakistan na India katika usiku wa kuamkia leo, ambayo yaliwaua watu wasiopungua 66, serikali zote mbili za India na Pakistan - zililishutumu tukio hilo kama ni kitendo cha kigaidi. Mashambulizi haya yalitokea siku moja tu kabla ya waziri wa nchi za nje wa Pakistan kutarajiwa kuwasili India kwa ziara fupi.

Moto iliharibu kabisa treni iliyoshambuliwa

Moto iliharibu kabisa treni iliyoshambuliwa

Hili ni shambulio la kutisha la kigaidi, alisema waziri wa nchi za nje wa Pakistan, Khurshid Kasuri alipoongea na waandishi wa habari leo asubuhi. Waziri Kasuri ameitaka India kuchunguza tukio hili. Lakini shambulizi hilo halitabadilisha mpango wake wa kutembelea India kwa ziara ya siku nne kuanzia kesho Jumanne.

Mabomu mawili yaliripuka katika treni hiyo ambayo ni mojawapo ya treni mbili zinazoiunganisha India na Pakistan na kusababisha moto katika mabehewa mawili. Kama kawaida kwenye treni nyingi za India, madirisha katika vyumba vya daraja la chini yalifungwa yakizuiliwa na nondo na hivyo kuwa mtego kwa abiria walioko ndani. Hivyo, licha ya kuwa madogo, mabomu hayo yaliweza kuwaua watu wasiopungua 66 na kuwajeruhi wengine si chini ya 13. Masanduku mengine mawili yenye mabomu ambayo hayajaripuka yamegunduliwa nje ya treni baada ya shambulio hilo.

Wengi wa walioathirika ni watu wa Pakistan wakirudi kutoka safari ya kuwatembelea jamaa zao nchini India, lakini baadhi yao pia ni Wahindi na maafisa watatu wa reli. Abiria wengine 600 wa treni hiyo walipelekwa kwenye mji wa mpakani wa Attari.

Treni hiyo imepewa jina la Kihindi lenye maana ya “treni ya makubaliano”. Alipoongea katika mji wa Patna, waziri wa mambo ya reli wa India, Laloo Prasad, alisema hicho ni kitendo cha hujuma ambacho kinalenga kuharibu mahusiano bora kati ya India na Pakistan. Wizara ya nchi za nje ya India iliarifu kuwa itafanya kila iwezalo kuzisaidia familia za wahanga na kuwapa viza haraka ili waweze kuingia India.

Kwa upande wake, waziri wa nchi za nje wa Pakistan, Khurshid Kasuri, alisisitiza kuwa mazungumzo ya amani yaimarishwe na kupewa uzito zaidi.

Bado haijulikani kundi gani limeweka mabomu hayo. Waziri Prasad wa India anawatuhumu Waislamu wenye msimamo mkali ambao pia wanaaminika walisababisha mashambulizi ya treni nchini India mwaka jana ambayo yaliwaua watu 185.

Kwa muda mrefu, waasi wa itikadi kali za Kiislamu wanapigania eneo la Kashmir litengwe kutoka India. Tangu mwaka 1989 zaidi ya watu 44.000 wameuawa katika mapigano haya. Baada ya mvutano huu kuwa ni mkali sana na karibu kusababisha vita kati ya India na Pakistan, nchi ambazo zote mbili zina silaha za kinyuklia, treni za kuvuka mpaka zilisitishwa mwaka 2002 na kurejeshwa tena mwaka 2004.

 • Tarehe 19.02.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHJy
 • Tarehe 19.02.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHJy

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com