1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mashambulio ya kigaidi ya Mumbai

Miraji Othman27 Novemba 2008

Athari za mashambulio ya Mumbai yataonekana nje ya India

https://p.dw.com/p/G3Y7
Waziri mkuuwa India, Manmohan SinghPicha: AP Photo


Mlolongo wa mashambulio yaliofanywa jana katika mji wa Mumbai huko India umezorotesha maisha katika mji huo mkubwa wa kiuchumi wa India. Hisia waliokuwa nayo watu kukosa usalama inaweza kulinganishwa na ile hali waliokuwa nayo wakaazi wa New York, Marekani, katika mashambulio ya Septema 2001.

Miji mkubwa ya India mnamo miaka ya karibuni, kwa bahati mbaya, imebidi izowee kujionea mashambulio ya kigaidi. Wakati muda mrefu kila wakati nchi jirani ya Pakistan ilikuwa inanyoshewa kidole kwamba ndio inayochochea mashambulio hayo, hivi sasa inadhihirika kwamba kuna makundi mbali mbali katika ardhi ya India yenyewe, kutokana na sababu za kisiasa za ndani nchini, ambayo yanachochea maashambulio hayo. Kuna Waislamu wa India waliokumbatia siasa kali kutokana na kubaguliwa na pia kutokana na vitisho vya wanasiasa wa Kibaniani wenye siasa kali kutaka kuendesha mauaji dhidi ya makundi ya Kiislamu. Makundi mengi ya watu wenye kutaka sehemu zao zijitenge na India, kutokea Kashmir hadi Kusini Mashariki ya nchi hiyo, na pia katika wiki za karibuni wale watu wanaoshukiwa kuwa ni magaidi wa Kibaniani waliokamatwa na ambao walitaka kushambulia vituo vya Kiislamu- mambo yote hayo yamewafanya maafisa wa jeshi wawe na kazi ngumu.

Lakini mashambulio haya ya karibuni yana sura nyingine. Mashambulio ya wakati mmoja yaliochagua malengo dhaifu yanaashiria ule mtindo unaotumiwa na mtandao wa kigaidi wa al-Qaida. Mashambulio katika sehemu mbali mbali, yalioweza kuowanishwa na washambuliaji wengi, ni kazi kubwa kuweza kufanywa na vikundi venye ajenda ya kupigania haki za eneo fulani au haki za kitaifa. Pia lile lengo la kuwalenga mahabusi walio raia wa Kimarekani, Kiengereza na Ki-Israeli linaambatana na malengo ya magaidi wa kimataifa.

Waziri mkuu wa India, Manmohan Singh, katika tamko lake la kwanza kuhusu mkasa huu, pia aliashiria kwamba kundi liliofanya mashambulio hayo ya kigaidi ya jana lina kituo cha operesheni zake nje ya India. Japokuwa hajaitaja Pakistan kwa jina, hata hivyo, huu mlolongo mpya wa mashambulio utasababisha mvutano mpya kati ya India na Pakistan. Na jambo hilo linafaa pia lizingatiwe na wale wenye kuyatekeleza mashambulio hayo.

Inafaa kuukumbuka mwaka 2001, miezi michache baada ya Septemba 11, pale magaidi waliolipolivamia jengo la bunge la India. India iliilaumu Pakistan kwa jambo hilo na ikakusanya majeshi yake katika mpaka wa nchi hizo mbili. Miezi kadhaa hali ilizidi kuwa mbaya, hata ikafika hadi kwamba watu walitazamia kutatokea vita vya kinyukliya baina ya nchi hizo mbili jirani zilioko Kusini mwa Bara la Asia. Katika wakati huo, mtandao wa kigaidi wa al-Qaida na Wataliban yaliitumia nafasi hiyo ya kushughulika jeshi la Pakistan katika mpaka wa Mashariki kurejea nyuma hadi maeneo ya mpakani mwa Pakistan baada ya Marekani kuivamia Afghanistan.

Pia sasa mtandao wa al-Qaida uko katika mbinyo kwa vile wanajeshi wa Pakistan wameanzisha operesheni za kijeshi katika mpaka wa Afghanistan na mashambulio ya ndege za kijeshi za Marekani dhidi ya al-Qaida yanaanzia kutokea Afghanistan. Mtandao huo wa kigaidi una maslahi kuona kwamba uhusiano baina ya India na Pakstan unaharibika, ili macho ya jeshi la Pakistan yaelekee kwengine.

Kwa hivyo, mashambulio yaliofanyika Bombaya jana yatakua na athari nje ya India. Athari zake zitaligusa eneo lote, na huu utakuwa mtihani wa mwanzo kwa rais mpya aliyechaguliwa huko Marekani, Barack Obama. Atahitaji kuziangalia kwa ugalifu hali zilivyo huko Afghanistan na Pakistan.