Marekani yaendelea kuiandama Ujerumani juu ya Nord Stream 2 | Matukio ya Kisiasa | DW | 07.08.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Marekani yaendelea kuiandama Ujerumani juu ya Nord Stream 2

Maseneta watatu wa chama cha Republican nchini Marekani wametoa onyo kali kwa waendeshaji wa bandari ndogo ya Ujerumani na kuwatishia kuwawekea vikwazo vya kisheria na kiuchumi wanaojihusisha na mradi wa bomba la gesi.

Maseneta watatu wa chama cha Republican nchini Marekani wametoa onyo kali kwa waendeshaji wa bandari ndogo ya Ujerumani na kuwatishia kuwawekea vikwazo vya kisheria na kiuchumi kutokana na madai ya kupeleka vifaa, huduma na msaada kwa manowari za Urusi zinazijihusisha na mradi wa bomba la gesi la Nord Stream 2, ambao Marekani inaupinga vikali. Mbunge mmoja wa Ujerumani amesema kitisho hicho cha Marekani kina alama zote za ubeberu. 

Barua iliyotumwa siku ya Jumatano na seneta Ted Cruz, Tom Cotton na seneta Ron Johnson, iliilenga kampuni ya Faehhafen Sassnitz, inayosimamia bandari ya Mukran, ambayo ni muhimu kabisa kwa meli zinazijihusisha na ujenzi wa mradi huo.

Sehemu ya barua hiyo iliandikwa na kusainiwa na wabunge hao ilisema "wajumbe wa bodi, maafisa na washika dau wa kampuni ya Faehrhafen Sassnitz watazuiwa kuingia Marekani, na mali yoyote ama maslahi waliyonayo kwenye mali waliyonayo ambayo imo ndani ya mamlaka yao kisheria vitazuiwa."

Deutschland Baustelle Eugal Pipeline (DW)

Sehemu ya mradi huo wa bombala Nord Stream 2 unaozua mvutano kati ya Ujerumani na Marekani

Barua hiyo pia imeonya kwamba kampuni hiyo ya Ujerumani inaweza ikaharibu mustakabali wake wa kifedha iwapo haitasitisha ushirikiano wa aina yoyote na makampuni yanayoshirikiana nayo kwenye mradi huo.

Maafisa wa Ujerumani walikosoa vikali vikwazo hivyo vya Marekani na baadhi ya wakosoaji walidai kwamba hatua hiyo ya Marekani ya kuupinga mradi huo mpya ilikuwa ni kwa sababu ilitaka kuuza gesi yake iliyogandishwa barani Ulaya.

Kiranja wa wabunge wa chama cha SPD kinachoshiriki katika serikali ya Ujerumani, Carsten Schneider ameiambia DW kuwa barua ya wabunge hao wa Marekani inazo alama zote za ubeberu mambo leo

Carsten Schneider Erster Parlamentarischer Geschäftsführer SPD Bundestagsfraktion (picture-alliance/dpa/K. Nietfeld)

Mbunge Carsten Schneider aonya kuhusu hatua hizo za Marekani akisema zina harufu ya kibeberu

.

Mbunge huyo amesema kitisho kutoka kwa taifa rafiki, cha kuangamiza uchumi wa kisiwa kidogo cha Ujerumani, ni hatua ya uhasama isiyokubalika.

Aidha, mbunge Schneider ameongeza kuwa hatua za Marekani zinazosukumwa na alichokiita, maslahi ya kiuchumi, zinaweza kuhujumu ushirikiano uliojengwa kwa miaka mingo kati ya Ujerumani na Marekani.

Hata hivyo Marekani yenyewe inadai kuwa bomba la Nordstream 2 litaongeza utegemezi wa Ujerumani kwa Urusi, madai ambayo kwa pamoja Berlin na Moscow wanayapinga.

Mradi wa Nord Stream 2 unaomilikiwa na kampuni kubwa la gesi la Urusi la Gazprom kwenye taarifa yake hapo jana ulisema kwa wakati huu wanaangalia mbadala wa kumalizia asilimia sita za mwisho za kilomita 1,230 za bomba, baada ya kusimamishwa kwa kampuni ya Allseas iliyokuwa ikifanya kazi ya kulaza mabomba, baada ya kutishiwa vikwazo na rais Donald Trump.

Kuna uungwaji mkono mkubwa miongoni mwa wabunge wa vyama vyote viwili vya Republican na Democrat kuhusiana na hatua hiyo ya vikwazo dhidi ya mradi huo wa bomba la gesi la Nord Stream 2, ambao ukikamilika utaweza kusafirisha gesi asilia kutoka Urusi hadi Ujerumani.

Soma Zaidi: Ujerumani yaishutumu Marekani kwa vikwazo vya mradi wa gesi

Mashirika: APE/DPAE

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com