1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

100610 Abbas Obama USA

Josephat Nyiro Charo10 Juni 2010

Marekani imeahidi msaada wa fedha kwa Wapalestina kufutia kikao kati ya rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina, Mahmoud Abbas na rais wa Marekani Barack Obama mjini Washington hapo jana.

https://p.dw.com/p/Nngo
Rais wa Marekani, Barack Obama, kulia na raia wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina, Mahmoud AbbasPicha: AP

Rais wa Marekani Barack Obama anafahamu kwamba rais Abbas ana wapinzani wengi katika maeneo ya Wapalestina na hivyo anakuwa na kibarua kigumu katika juhudi za kutafuta amani na Waisraeli. Licha ya changamoto hiyo, rais Obama alimpa zawadi rais Abbas ya kurudi nayo nyumbani. Dola milioni 240 za kimarekani zitakazowekezwa kwenye mradi wa ujenzi wa nyumba katika Ukingo wa Magharibi na dola nyengine milioni 75. Viongozi hao walijadiliana pia juu ya kuzingirwa kwa Ukanda wa Gaza.

Mkutano baina ya rais Obama na rais Abbas ulikuwa ufanyike wiki iliyopita, lakini ziara ya kiongozi huyo wa Wapalestina ikaahirishwa ghafla hadi wiki hii kufuatia hatua ya Israel kuishambulia meli ya misaada ya Uturuki iliyokuwa kwenye msafara wa meli za misaada zilizokuwa njiani kuekelea Gaza kuwapelekea Wapalestina misaada hiyo. Uvamizi huo ulisababisha vifo vya watu tisa akiwemo Mmarekani mmoja na kuzua masuali mengi ambayo mpaka sasa hayapatiwa ufumbuzi.

Viongozi hao walibadilishana mawazo huku rais Abbas akitaka kujua vipi Marekani inavyoitazama Israel kuhusiana na uvamizi wa meli hiyo ya misaada. Marekani imejiepusha na kauli za kuikemea Israel moja kwa moja, lakini hata hivyo rais Obama ameeleza wazi bayana kwamba Marekani inaunga mkono wito uliotolewa na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, wa kutaka kisa hicho kichunguzwe.

"Nimewaambia Waisraeli kuwa ni kwa maslahi ya Israel kuhakikisha kila mtu anafahamu vipi tukio hili lilivyotokea ili kuhakikisha halitoei tena. Tunatarajia wito wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa utatekelezwa."

Israelischer Angriff auf Hilfskonvoi für Gaza
Wanajeshi wa Israel wakiivamia meli ya UturukiPicha: AP

Israel imekuwa ikiuzingira Ukanda wa Gaza tangu mwezi Juni 2007, miaka 3 sasa, lakini hata hivyo chama cha Hamas ambacho kinatawala Gaza kimekuwa kikijipatia silaha kutoka kwa mataifa ya kiarabu na kuihangaisha Israel kwa mashabulio ya kigaidi. Rais Obama hakusema ikiwa kuzingirwa kwa Ukanda wa Gaza na Israel si haki, wala ikiwa Marekani inaunga mkono hatua hiyo ya Israel.

"Inaonekana ipo haja ya kuwa na njia za kuchunguza usafirishaji wa silaha badala ya kuzingatia tu kuzuia kila kitu halafu kuruhusu vitu viingie Gaza. Pengine mkasa wa kuvamiwa meli ya misaada ya Uturuki iliyokuwa ikielekea Gaza kunaweza kutumiwa kama nafasi ya kusukuma mbele juhudi za kutafuta amani ya Mashariki ya Kati," amesema rais Obama. Kiongozi huyo aidha amesema swala nyeti kwa sasa ni vipi hatua ya kuuzingira Ukanda wa Gaza inavyoweza kuondoshwa.

"Ili magaidi watengwe badala ya kuwa na kisingizio cha kujiingiza katika vitendo vya kigaidi. Lakini pia ifanyike katika hali itakayohakikisha wasiwasi kuhusu usalama wa Israel, unazingatiwa. Nadhani rais Abbas anakubaliana na wazo hili, kusiwe na makombora yanayorushwa kutoka Gaza kwenda Israel, lakini katika kipindi kirefu njia muafaka ya kusuluhisha tatizo hili ni kuwa na taifa la Palestina litakaloishi kwa amani na Israel iliyo salama. Matatizo yaliyopo hivi sasa yametokana na kushindwa kwetu kulitatua tatizo hili."

Mgeni wa rais Obama hakusema mengi kwenye mkutano na waandishi habari. Haikuweza kubainika kwa hivyo ikiwa rais Abbas alihisi vipi kuhusiana na matamshi ya rais Obama. Hakuna jambo lolote jipya lililojitokeza kuhusu kuanza kwa mazungumzo ya ana kwa ana kati ya Israel na Wapalestina. Ni yale yale tu kwamba ipo haja ya kupiga hatua mbele kwenye mazungumzo.

Mwandishi: Hasselmann, Silke/Josephat Charo

Mhariri: Othman Miraj