1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Marekani: Urusi ilifanya uhalifu wa kivita Kherson

22 Novemba 2022

Afisa mmoja mwandamizi wa Marekani amesema Urusi imewauwa, kuwatesa na kuwateka nyara raia wa Ukraine kwa mfumo wa wazi uliopangwa.

https://p.dw.com/p/4JrOh
Ukraine ukrainsiche Armee bei Cherson
Picha: Metin Aktas/AA/picture alliance

Hatua hii inaonyesha kwamba huenda maafisa wakuu katika serikali ya Urusi walihusika katika uhalifu wa kivita. Haya yanafanyika wakati ambapo Ukraine inasema imegundua maeneo 4 yaliyokuwa yanatumiwa na Urusi kuwatesa Waukraine katika eneo lililokombolewa hivi majuzi la Kherson.

Akizungumza na waandishi wa habari mjini Washington, balozi wa Marekani kuhusiana na Sheria ya Uhalifu Duniani Beth Van Schaack amesema kuna ushahidi mkubwa kwamba vitendo vya mateso vya Urusi nchini Ukraine havikutekelezwa kwa kushtukiza tu.

Van Schaack amesema kuna ushahidi kwamba uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umeandamana na vitendo vya uhalifu wa kivita katika kila eneo ambalo majeshi ya Urusi yalitumwa.

Maeneo 4 ya mateso yagunduliwa Kherson

Balozi huyo anasema ushahidi kutoka maeneo yaliyokombolewa unaonyesha raia na wafungwa wa kivita walishambuliwa na kuteswa kwa kusudi. Waukraine wakiwemo watoto waliondolewa na kupelekwa Urusi kwa lazima na zaidi ya hayo kulikwua na mauaji na udhalilishaji wa kingono.

Ukraine-Krieg I Kherson I Cherson
Raia wa Kherson wakisubiri maji safi ya kunywaPicha: Bernat Armangue/AP/dpa/picture alliance

Nayo afisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa Ukraine imetoa taarifa iliyosema kwamba imegundua maeneo 4 yaliyotumiwa na Urusi kuwazuia na kuwatesa watu huko Kherson. Afisi hiyo ya mwendesha mashtaka inasema imegundua maeneo hayo baada ya kufanya uchunguzi kwa ushirikiano na maafisa wa polisi na wataalam.

Taarifa hiyo imesema walipata sime na kifaa kilichotumiwa na majeshi ya Urusi kuwatesa watu kwa kutumia umeme. Mamlaka za Urusi pia ziliacha nyaraka zilizoonyesha uongozi wa maeneo hayo ya mateso. Mkaazi mmoja wa Kherson ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kuwa aliteswa kwa wiki kadhaa katika mojawapo ya maeneo hayo.

NATO iitambue Urusi kama taifa la kigaidi

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy kwa mara nyengine ameitaka jumuiya ya kujihami ya NATO na marafiki zake kuitambua Urusi kama taifa la kigaidi.

"Natoa wito kwa jumuiya ya NATO kuchukua hatua madhubuti kutekeleza mpango wa amani wa Ukraine unaoweza kuhakikisha amani na haki kwa Ukraine na jamii nzima ya Ulaya na Atlantiki. Natoa wito pia kwa mabunge yote ya nchi wanachama wa jumuiya ya NATO kuchukua uamuzi wa kuitambua Urusi kama taifa la kigaidi. Naamini kwamba pole pole tutafika hapa, hivi ndivyo Urusi itakavyoonekana duniani," alisema Zelenskiy.

BG Ukraine-Krieg | Feier zur Rückgewinnung von Cherson
Rais Zelenskiy wa Ukraine akiwa na mmoja wa wanajeshi wa nchi hiyoPicha: Ukrainian Presidential Press Service/REUTERS

Hayo yakiarifiwa mamlaka nchini Ukraine zimeanza kuwaondoa raia kutoka maeneo yaliyokombolewa hivi majuzi ya Kherson na Mykolaiv kwa hofu kwamba ukosefu wa umeme na maji kutokana na mashambulizi ya Urusi, ni jambo litakalofanya hali ya maisha kuwa ngumu zaidi katika kipindi hiki cha majira ya baridi.

Naibu waziri mkuu wa Ukraine Iryna Vreshchuk amesema serikali itawapa raia usafiri, makazi na matibabu huku watakaopewa kipau mbele wakiwa kina mama wenye watoto, wagonjwa na wazee.

Chanzo: AP/AFP