1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kenya na Marekani kuimarisha zaidi ushirikiano

Angela Mdungu
24 Mei 2024

Rais wa Marekani Joe Biden ameahidi kushirikiana na Kenya katika sekta ya teknolojia, usalama na kutoa msamaha wa madeni. Ametoa ahadi hiyo alipokutana na Rais William Ruto katika Ikulu ya White House.

https://p.dw.com/p/4gErB
William Ruto ziarani Marekani
Rais wa Kenya William Ruto akiwa mjini Washington na Rais wa Marekani Joe Biden Picha: Susan Walsh/AP Photo/picture alliance

Ahadi hiyo kwa moja ya mataifa yenye demokrasia zaidi Afrika imetolewa na Biden wakati wa ziara hiyo rasmi ya kikazi ya kwanza ya kiongozi wa Afrika ndani ya Ikulu ya White House tangu mwaka 2008.

Soma zaidi: Biden kuipa Kenya hadhi ya mshirika mkuu nje ya NATO

Katika mkutano huo na Ruto, Biden amebainisha kuwa Marekani itaipa Kenya hadhi ya kuwa nchi ya kwanza barani Afrika  kusini mwa jangwa la Sahara kuwa mshirika muhimu ambaye sio mwanachama wa NATO. 

Biden amesema kuwa licha ya umbali kati ya Marekani na Kenya, nchi hizo zinaunganishwa na misingi yao sawa ya kidemokrasia. Ameeleza kuwa nchi hizo mbili zinaheshimu historia inayoziunganisha.

 Ruto alishiriki katika dhifa ya chakula cha jioni iliyohudhuriwa na watu mashuhuri 500 akiwemo makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris, Rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton na mkewe Hillary, jana Alhamisi.

Ushirikiano zaidi kuelekezwa pia katika mabadiliko ya hali ya hewa

Kando ya viongozi hao wawili kusisitiza juu ya misingi ya demokrasia wanayoiamini, wamezungumzia pia matamanio yao ya kushirikiana katika masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa, ukosefu wa utulivu wa kisiasa na uchumi.

Marekani na Kenya zimetiliana saini ushirikiano katika suala la ulinzi
Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd J. Austin na Rais wa Kenya William RutoPicha: Khalil Senosi/AP/picture alliance

Ziara Ruto nchini Marekani imefanyika wakati Marekani na Ufaransa wakikumbana ushindani barani Afrika. Ni kutokana na uwekezaji mkubwa wa China barani humo huku Urusi ikitumia makundi yake ya wanamgambo katika baadhi ya mataifa Afrika.

Katika ziara hiyo Biden ambaye ni mwenyeji wa Ruto ameikaribisha hatua ya Ruto kuunga mkono Ukraine ambayo ni moja ya mataifa 18 washirika yasiyo wanachama wa NATO  wakati ikipambana na uvamizi wa Urusi.