1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Iran

Marekani na Iran zafanikiwa kubadilishana wafungwa

Sylvia Mwehozi
18 Septemba 2023

Wafungwa watano wa Kimarekani walioachiwa na Iran wameondoka mjini Doha kama sehemu ya mpango wa kubadilishana wafungwa baada ya Dola bilioni 6 za Iran kuhamishiwa katika akaunti za nchi hiyo nchini Qatar.

https://p.dw.com/p/4WU4Z
Symbolbild | Flaggen | USA und Iran
Picha: Dado Ruvic/REUTERS

Duru zinasema kwamba wafungwa hao watano wa Kimarekani wanaojumuisha mfanyabiashara na mwanamazingira waliondoka Iran wakiwa katika ndege ya Qatar na kusindikizwa na ndugu wawili na balozi wa Qatar.

Mpango huo wa kubadilishana wafungwa kati ya Iran na Marekaniumefikiwa kufuatia uratibu wa Qatar. Iran ilitaka kuachiliwa kwa fedha zake takribani dola bilioni 6 za kimarekani na kisha fedha hizo kuhamishiwa katika benki za Tehran nchini Qatar, huku ndege ya kuwabeba wafungwa hao ikiwa tayari muda wote mjini Tehran.

Wafungwa hao watano wa Marekani walio pia na uraia wa Iran ambayo haitambui uraia pacha, waliachiwa baada ya kuwekwa kwenye kizuizi cha nyumbani kufuatia kufikiwa makubaliano ya kubadilishana wafungwa mwezi uliopita.

Iran Qatar
Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Qatar katika Masuala ya kikanda Dk. Mohammed bin Abdulaziz bin Saleh Al Khulaifi alipokutana na Naibu Waziri wa Masuala ya Kisiasa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Dk. Ali Bagheri, mjini Tehran.Picha: Qatar News Agency/Handout via REUTERS

Miongoni mwao yumo mfanyabiashara Siamak Namazi, aliyekamatwa mwaka 2015 kwa mashtaka ya ujasusi ambayo familia yake iliyakataa. Wengine ni mhifadhi wa wanyamapori Morad Tahbaz, mwekezaji Emad Sharqi, na wengine wawili ambao hawakutaka kutajwa majina yao.Iran: Wanaharakati wa Mazingira wafungwa jela

Kuachiliwa kwa fedha hizo zilizokuwa zimefungiwa na mshirika wa Marekani Korea Kusini chini ya vikwazo vya muda mrefu ilikuwa ni sharti kuu la Iran kuwaachia wafungwa watano wa Kimarekani na Marekani pia kufanya vivyo hivyo kwa wafungwa watano wa Iran. Qatar iliyokuwa mpatanishi kwasababu Tehran na Washington hazina uhusiano wa kidiplomasia, imeziarifu pande zote mbili kwamba miamala ya fedha imefanikiwa. Awali msemaji katika wizara ya mambo ya nje ya Iran Nasser Kanani alidokeza kuhusu wafungwa wa Iran.

"Suala la kubadilishana wafungwa litafanyika ndani ya siku moja. Wairani watano wataachiwa kutoka jela ya Marekani. Kulingana na taarifa za hivi karibuni wawili waliomba kubakia nchini Marekani, wawili watarejea Iran na mmoja ataungana na familia yake katika nchi nyingine ya tatu."

Iran, Tehran
Rais wa Iran Ebrahim Raisi Picha: Atta Kenare/AFP/Getty Images

Baadae kidogo shirika la habari la Iran la Tasnim likaripoti kwamba tayari wafungwa wawili wa Iran walioachiwa na Marekani wamewasili Qatar. Taarifa hiyo imewataja "Mehrdad Moein Ansari na Reza Sarhangpour" kama wafungwa waliachiliwa na kutua Doha na sasa wanapanga kusafiri kwenda Iran. Iran ilikuwa imezalisha dola bilioni 6 kupitia mauzo ya mafuta kwa Korea Kusini, ambayo ilizuia fedha hizo baada ya Marekani chini ya rais wa zamani Donald Trump kurejesha vikwazo wakati alipojiondoa kwenye makubaliano ya kihistoria ya nyuklia.

Soma pia: Iran yadai kukubaliana na Marekani katika kubadilishana wafungwa

Wakati zoezi hilo la kuwaachia wafungwa likiendelea, rais wa Marekani Joe Biden ametangaza vikwazo dhidi ya rais wa zamani wa Iran Mahmoud Ahmadinejad na wizara inayohusika na ujasusi.

Vyanzo: afp/reuters