Mapigano mengine kati ya Israel na Wapalestina. | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.04.2008
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mapigano mengine kati ya Israel na Wapalestina.

Hali inazidi kuwa mbaya huku mpango wa rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter kukutana na viongozi wa Hamas ukikosolewa vikali na Israel na Marekani.

Mwanajeshi wa Israel akimtia nguvuni kijana mmoja katika Ukingo wa magharibi.

Mwanajeshi wa Israel akimtia nguvuni kijana mmoja katika Ukingo wa magharibi.

Hali katika maeneo ya wapalestina inazidi kuwa mbaya, huku mapigano yakiendelea kati ya majeshi ya Israel na wapiganaji wa kipalestina. Baada ya mapigano ya jana huko Gaza leo yalizuka mapigano katika mji wa Jenin kwenye ukingo wa magharibi.

Msemaji wa jeshi la Israel ilisema wanajeshi wao waliwauwa watu wawili wakati wa harakati za kuwatia nguvuni katika kijiji cha Qabatiya, akiongeza kwamba watu hao walikua na silaha na wakijaribu kutoroka kwa gari kutoka jengo ambako walikua wamejificha.

Vifo hivyo vimekuja siku moja baada ya wanajeshi watatu wa Israel kuuawa waliposhambuliwa ghafla katika eneo la ukanda wa Gaza, na Israel kujibu kwa kuhujumu kutoka angani na kuwauwa wapalestina wapatao 18 wakiwemo raia kadhaa

Kiasi ya watu 412 wameshauawa tangu Israel wapalestina, walipoyafufua mazungumzo rasmi ya amani chini ya udhamini wa Marekani mwezi Novemba na wengi miongoni mwao ni wanaharakati wa kipalestina huko Gaza.

Hali hii inazidi kuwa mbaya katika wakati ambao rais wa zamani wa Marekani Jimmy Carter analitembelea eneo hilo la mashariki ya kati , na anapanga kukutana leo na viongozi wawili wa ngazi ya juu wa chama cha Hamas katika mji mkuu wa Misri-Cairo. Hata hivyo uamuzi wake wa kukutana na wanasiasa hao wa Hamas -chama kinachotajwa na Israel , Marekani na umoja wa ulaya kuwa ni cha kigaidi, umekosolewa vikali na Israel pamoja na utawala wa Marekani wa rais Bush. Bw Carter anasisitiza kwamba mawasiliano na mazungumzo ndiyo njia pekee ya kusaka suluhisho la mgogoro huo.

Baadae rais huyo wa zamani wa Marekani ambaye alikataa kutamka lolote juu ya mkutano wake na viongozi wa hamas alipowasili Cairo jana, anatarajiwa pia kukutana na kiongozi mkuu wa chama hicho Khaled Mashaala mjini Damascus atakapoizuru Syria kesho. Mashaal anaishi uhamishoni nchini humo.

Kwa upande wake rais wa wapalestina Mahmoud Abbas akiwa ziarani mjini Mosko amependekeza mkutano wa amani ya mashariki ya kati mwezi Juni ufanyike katika mji mkuu huo wa Urusi. Akizungumza na wanafunzi wa chuo kikuu Bw Abbas alisema mkutano huo unahitajika haraka kufutilia matokeo ya mazungumzo ya Novemba mwaka jana mjini Annapolis Marekani yaliosimamiwa na rais George Bush wa Marekani, wakati huo huo akilaani kuimarishwa kwa mashambulizi ya Israel ndani ya eneo la Gaza.

Kwa miaka kadhaa sasa Urusi ambayo ni mwanachama wa lile kundi la mawasiliano la pande nne kuhusu amani ya mashariki ya kati, imekua ikipigania kuwa mwenyeji wa mkutano huo. Wahusika wengine ni Marekani, Umoja wa mataifa na Umoja wa ulaya.

Kesho kiongozi huyo wa wapalestina atakua na mlolongo wa mazungumzo na maafisa wa Urusi kabla ya kukutana na rais Vladimir Putin . Bw Putin leo anaizuru Libya akikutana na kiongozi wa nchi hiyo Muammar Gaddafi, moja wapo ya ziara zake za mwisho kabla hajakabidhi hatamu za Urais kwa rais mteule Dmitry Medvedev tarehe saba mwezi ujao.


 • Tarehe 17.04.2008
 • Mwandishi Abdulrahman, Mohamed
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DjYK
 • Tarehe 17.04.2008
 • Mwandishi Abdulrahman, Mohamed
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/DjYK
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com