Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani. | Magazetini | DW | 28.10.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani.

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanatoa maoni yao juu ya soko la ajira na juu ya ndoa za kulazimisha.

default

Bunge la Ujerumani limepitisha sheria ya kuwaadhibu wanaolazimisha ndoa.

Wahariri wa magazeti ya hapa nchini leo wanatoa maoni yao juu ya mafanikio katika juhudi za kupambana na ukosefu wa ajira na juu ya ndoa za kulazimishwa.

Idadi ya watu wasiokuwa na ajira imepungua nchini Ujerumani katika kiwango kisichokuwa na mithili katika kipindi cha miaka 18 iliyopita .

Juu ya mafanikio hayo mhariri wa gazeti la Emder anasema kilichotokea ni muujiza ulioanza kuonekana mnamo miezi ya hivi karibuni. Mhariri huyo anasema hayo yanatokana na hali nzuri ya uchumi. Na anasema ingawa wanasiasa hawakufanya mengi juu ya hayo, pia hawakuweka vizingiti katika njia ya ustawi wa uchumi.Lakini licha ya mafanikio hayo, kwenye soko la ajira gazeti la Südkurier lina mashaka na linaeleza kuwa ni vigumu kuamini kwamba dunia imerejea katika hali nzuri baada ya migogoro ya miaka miwili iliyopita. Yumkini hiyo ndiyo sababu kwamba waajiri wanatoa ajira ya muda mfupi.

Mhariri wa gazeti la Neue Osnabrücker pia anazungumzia juu ya muujiza kwenye soko la ajira na anatilia maanani kwamba kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 18 iliyopita idadi ya watu wasiokuwa na kazi nchini Ujerumani imepungua na kufikia chini ya milioni tatu. Mhariri huyo anafafanua kuwa sasa ni wazi kwamba migogoro ya mabenki na uchumi imetatuliwa nchini Ujerumani. Mhariri huyo anasema nchi jirani zinaionea kijicho Ujerumani. Lakini anaeleza kuwa serikali ilitumia fedha ili kufadhli miradi ya ajira ya muda mfupi, na vyama vya wafanyakazi vilisaidia kwa kuepuka kudai mishahara mikubwa.

Mhariri wa gazeti la Neue Osnabrücker pia anatilia maanani kwamba sheria ya kustawisha uchumi iliyopitishwa na serikali mwanzoni mwa mwaka, pia imechangia katika mafanikio yaliyopatikana kwenye soko la ajira.

Wahariri wa magazeti leo pia wanazungumzia juu ya sheria ya kuwaadhibu wanaolazimisha ndoa nchini Ujerumani.Lakini mhariri wa gazeti la Lausitzer Rundschau anasema sheria hiyo ni sawa na kisu kidugi.Kwa sababu ni vigumu kuthibitisha iwapo ndoa kama hiyo imefungwa , madhali baadhi ya wahusika huamua kunyamaa kimya.

Naye mhariri wa Sächsiche Zeitung anasema haijulikani sheria hiyo itakuwa na athari gani, lakini anasema ni vizuri kwamba ipo, na anaetaka kujihami anaweza kuitumia.

Gazeti la Berliner Morgenpost linawafiki kwa kusema kwamba inajulikana kwa muda mrefu kuwa ndoa za kulazimishwa zimekuwa zinafungwa nchini Ujerumani. Kwani vijana wa Kituruki wanapelekwa nchini Uturuki kuoa au kuolewa. Kwa hiyo, ikiwa hakuna anaejitokeza kwa hiari yake na kuenda mahakamani, sheria iliyopitishwa haitaleta unafuu wowote.

Mwandishi:Mtullya Abdu

Mhariri: Miraji Othman

 • Tarehe 28.10.2010
 • Mwandishi Abdu Said Mtullya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PrMF
 • Tarehe 28.10.2010
 • Mwandishi Abdu Said Mtullya
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/PrMF
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com