Magazetini
9 Septemba 2009Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wanazungumzia juu ya uchaguzi wa rais nchini Afghanistan, tamko la kansela Angela Merkel juu ya shambulio lililofanywa na ndege za Marekani kwa niaba ya kikosi cha Ujerumani nchini Afghanistan.
Wahariri hao pia wameandika juu ya ripoti ya kiwango cha elimu nchini Ujerumani iliyotolewa na shirika la ushirikiano wa uchumi na maendeleo OECD.
Juu ya uchaguzi wa rais nchini Afghanistan gazeti la Financial Times Deutschland linasema yeyote anaetaka kuleta demokrasia nchini Afghanistan kwa kutumia vigezo vya magharibi atakuwa sawa na mtu anaenunua punda kiwete.! Sababu ni kwamba katika mazingira ya Aghanistan demokrasia ni msingi tu wa kujaribu kuleta utulivu nchini.
Gazeti la Financial Times Deutschland linaeleza kwamba uhalali wa serikali ya rais Karzai umetiwa dosari na madai juu ya udanganyifu uliofanyika katika kuhesabu kura. Na ndiyo sababu,ni lazima kura zihesabiwe tena katika maeneo ambako madai hayo yametolewa.
Wahariri wa magazeti pia wametoa maoni yao juu ya shambulio lililofanywa na ndege za Marekani baada ya kamanda wa majeshi ya Ujerumani kuomba msaada.
Katika shambulio hilo, katika jimbo la Kunduz raia zaidi ya 130 waliuawa. Jeshi la Ujerumani limelaumiwa vikali ndani na nje kwa vifo vya rais hao. Lakini Kansela wa Ujerumani Angela Merkel alitetea uamuzi wa kamanda wa jeshi la Ujerumani katika tamko alilotoa bungeni jana. Gazeti la Neue Osnabrücker linasema katika maoni yake kwamba msimamo wa Kansela Merkel ni sahihi kabisa katika kupinga lawama zinazotoka nje na ndani juu ya shambulio hilo lililoelekezwa dhidi ya taliban.
Mhariri wa Neue Osnabrücker anatilia maanani kwamba Kansela Merkel hakurudi nyuma bungeni katika msimamo wake, juu ya Afghanistan na badala yake amewataka wananchi wa Ujerumani watambue umuhimu wa jukumu la jeshi la Ujerumani nchini Afghanistan.Mhariri huyo anasema wajerumani wanahitaji kuwa na moyo wa kuwa tayari kujitoa mhanga na kusonga mbele.
Lakini mhariri wa Reutlinger General Anzeiger hakubaliani na hayo. Mhariri huyo anasema, ni kweli kwamba Kansela Merkel amezungumza vizuri bungeni, lakini lingekuwa jambo zuri zaidi iwapo serikali yake ingefanikiwa katika ujenzi wa Afghanistan na kuondoka haraka.
Shirika la ushirikiano wa uchumi na maendeleo OECD limetoa ripoti juu ya elimu katika nchi za shirika hilo.Ripoti hiyo imeonyesha kuwa Ujerumani inalega nyuma ya nchi nyingi. Juu ya hayo gazeti la Oldenburgische Volkszeitung linasema
"Wanasiasaa nchini Ujerumani wanafikiria tu juu ya ustawi wa uchumi, takwimu za bajeti na asilimia za kodi." Gazeti linasema hayo ni sawa,lakini bila ya kuekeza katika maendeleo ya elimu na utafiti hapatakuwa na ustawi. Kwa hiyo viongozi wanatakiwa halakuli hali,wachukue hatua thabiti.
Mwandishi/Mtullya /Deutsche Zeitungen
Mhariri/ Abdul-Rahman
.....