1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Magazetini.

Abdu Said Mtullya13 Julai 2009

Wahariri wamezingatia mauaji ya mwanamke wa Misri na ziara ya rais Obama Ghana

https://p.dw.com/p/IoWQ
Rais Obama ziarani Ghana.Picha: AP

Leo wahariri wa magazeti ya Ujerumani kwa mara nyingine wanazungumzia juu ya mkasa wa kuuawa kwa mama mmoja wa kimisri kwa kuchomwa visu ndani ya mahakama na pia wanatathmini yaliyosemwa na rais Obama kwa viongozi wa Afrika.


Mama mmoja wa kimisri Marwa el Shirbini aliuawa kwa kuchomwa visu mara 18 ndani ya mahakama katika mji wa Dresden mashariki mwa Ujerumani.

Aliuawa na mtu aliemshtaki.

Mtu huyo alimkashifu Mmisri huyo kwa sababu alivaa hijab.

Wakati kesi ikifanyika mtu huyo alimchoma visu mama huyo aliekuwa mja mzito na kumwuua. Mkasa huo bado unazingatiwa na vyombo vya habari. Mhariri wa gazeti la Säschsiche Zeitung anasema kutumiwa mkasa huo kwa sababu za kisiasa hakutaleta manufaa kwa upande wowote. Mhariri huyo anasema kuuawa kwa mama huyo Marwa el Shirbini siyo tukio linalotokea kila siku nchini Ujerumani.

Hatahivyo mhariri huyo anaeleza kuwa sauti za ghadhabu zinazosikika kutoka Misri ni jambo linaloweza kueleweka, lakini mipaka ya staha imevukwa nchini Iran ambako wajerumani kwa jumla wanaitwa mafashisti kutokana na mauaji ya mama huyo wa kimisri.

Gazeti la Nürnberger pia limeandika juu ya mkasa huo kwa kusema kuwa

mtu aliemchoma visu na kumwuua mama huyo wa kimisri, ni mtu asiyekuwa na mizizi yoyote- ni mtu asiyekuwa na dini wala kigezo chochote cha maadili. Mtazamo wake juu ya dunia ni sawa na mtoto wa sanamu, walakini uhalifu alietenda haupaswi kupuuzwa.

Sababu ni kwamba unaweza kutendwa tena na watu wenye hofu juu ya kuenea kwa uislamu nchini Ujerumani.Lakini mhariri wa gazeti la Nürnberger anawakumbusha watu hao kwamba idadi ya wajerumani wanaosilimu inaendelea kuwa ndogo.

Jukumu la kuleta maendeleo barani Afrika ni la waafrika wenyewe na kwamba wakati wa kuwalaumu wakoloni kwa maovu yanayotendeka barani Afrika umeshapita. Hayo alisema rais Barack Obama wakati wa ziara yake nchini Ghana mwishoni mwa wiki iliyopita.

Juu ya mwito huo gazeti la Neue Osnabrücker linasema rais Obama amewaambia waafrika ukweli, bila ya kuwaonea haya.

Mhariri wa gazeti hilo anauliza jee ni nani anaepaswa kulaumiwa kwa umasikini, maradhi kama ukimwi,vita na kuangushwa kwa serikali mara kwa mara? Jee ni wakoloni wa hapo zamani au nchi za viwanda za leo? Jibu ni hapana, anasema mhariri wa gazeti hilo. Anatoa mfano wa zimbabwe- nchi iliyokuwa ghala la chakula barani Afrika hapo awali. Mhariri anahoji kuwa Zimbabwe haikugeuzwa nyumba ya njaa na nchi za magharibi.Wanaobeba lawama ni waafrika wenyewe na hasa viongozi.

Hatahivyo gazeti la Recklinghäuser linasema nchi tajiri zinapaswa kuacha mara moja, kupora raslimali za Afrika na ziondoe vizingiti katika biashara.