Wahariri wanazungumzia kuhusu bajeti ya Ujerumani iliyopitishwa bungeni ...
3 Julai 2008
►◄
Wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo wamezungumzia zaidi kuhusu kupitishwa kwa bajeti ya serikali na bunge la shirikisho kwa mwaka 2009, pamoja na mpango wa mafao ya jamii wa umoja wa Ulaya.
Aliyewakusanyia maoni hayo ya wahariri leo hii ni Sekione Kitojo.
Kuhusu kupitishwa kwa bajeti ya serikali ya mwaka 2009 gazeti la Westdeutsche Allgemeine Zeitung kutoka Essen linathibitisha kazi nzuri aliyoifanyika waziri wa fedha na kufanikisha kupitishwa kwa bajeti hiyo huku likisema kuwa pamoja na hayo amevuka vikwazo vingi. Gazeti linaandika.
Iwapo Steinbrück anajisikia sasa kuwa ni shujaa wa sera za masuala ya fedha , itakuwa ni kwa muda huu tu , kwa kuwa ameweza kufanikiwa kuzuwia matumizi mengine makubwa zaidi. Kwa hiyo anastahili kusifiwa. Kabla ya hapo ilikuwa kuna matumizi makubwa. Ubanaji wa matumizi hata hivyo gazeti linasema haukuhitaji kuchukua hatua nusu nusu. Hata hivyo gazeti hilo linasema kuwa waziri Steinbrück amepata bahati kubwa.
Katika njia sahihi na kuelekea katika lengo sahihi, linaeleza gazeti la Nordkurier kutoka Neubrandenburg.
Ukipima matarajio na mahitaji ambayo wajumbe wa baraza la mawaziri walikuwa nayo Steinbrück amepata matokeo mazuri. Waziri huyo linasema gazeti kuwa amefanikiwa kulielekeza jahazi katika njia nzuri, lakini amepoteza muda mrefu kuweza kuweka kasi zaidi.
Gazeti la Der Tagesspiegel kutoka Berlin linatoa sifa kwa serikali ya mseto. Linaandika.
Ni muhimu kwamba Angela Merkel na Peer Steinbrück waendelee kuzungumza kuhusiana na masuala ya upunguzaji wa kodi, mafao wanayopata wafanyakazi wanaofanyakazi mbali na makaazi yao , pamoja na ushuru. Tunaweza tu kutumai kuwa hali hii haitaweza kuingia katika mivutano ya uchaguzi ya shirikisho ama ya majimbo. Kwa sababu kile ambacho Merkel na Steinbrück wamekifanya katika kubana matumizi na kutokubabaika kisiasa , kwa kweli ni dhana , kwamba sera za kifedha za Ujerumani zitabaki kuwa imara.
Lakini gazeti la Lausitzer Rundschau la mjini Cottbus linapingana na kila anayefurahia muswada wa bajeti uliotolewa na Steinbrück.
Gazeti linasema kuwa katika muda wake madarakani kumekuwa na upungufu kuazia mwaka 2005 wa jumla ya Euro bilioni 159. Fedha hizi zilikuwa wapi linauliza gazeti hilo. Muungano mkuu wa serikali kama unavyoitwa haukuweza kutumia pato la ziada na wameendelea tu kubana matumizi zaidi. Mpango wa Steinbrück wa kujiondoa kutoka katika madeni hauna umakini wowote kama ilivyokuwa kwa waziri wa fedha Eichel mwaka 2002. Bado bajeti ina upungufu wa muundo linatahadharisha gazeti hilo na kusema kuwa bado hakuna kitu cha kujikinga na mzozo huu.
Suala jingine lililochambuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani ni kuhusu mpango wa mafao ya jamii uliotolewa na umoja wa Ulaya. Gazeti la Frankfurter Rundschau limejishughulisha zaidi na suala hilo.
Gazeti linasema kuwa kwa mtazamo wake kutokana na lawama kali inabidi mtu kujaribu kuitetea Ujerumani. Hii haina maana , kwamba mipango wa umoja wa Ulaya mjini Brussels isitumike. Kwa mfano sheria kuhusiana na mabaraza ya wafanyakazi kwamba inaweza kungojea zaidi, mpaka pale tume hiyo itakapotoa taarifa, kuhusiana na kusikilizwa kwa maombi ya uimarishaji wa wawakilishi wa wafanyakazi. Hata katika suala la kupambana na ubaguzi kuna maswali mengi hayajajibiwa.
Gazeti la Leipziger Volkszeitung, linadokeza kuwa katika siku za usoni wagonjwa wataweza kupatiwa matibabu katika mataifa , nje ya umoja wa Ulaya. Gazeti linaandika.
Lakini gazeti hilo linatanabahisha kuwa yule ambaye anataka nafasi kubwa zaidi ya uchaguzi wa kupatiwa matibabu hayo nje ya umoja wa Ulaya , ni lazima aweze kufahamu ni aina gani ya matibabu anaweza kuyapata huko na ubora wa utendaji. Katika baadhi ya nchi kuna upungufu mkubwa wa hilo. Uwanja mpana wa uchaguzi kwa wagonjwa , ambao hadi sasa umetumiwa na watu wachache tu , unaweza kuanzisha mashindano makubwa katika nchi mbali mbali , na pia utaalamu wa hali ya juu pamoja na ubora zaidi.