Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo | Magazetini | DW | 20.01.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo

Obama akamilisha mwaka mmoja madarakani

Rais Barack Obama

Rais Barack Obama

Gazeti la Darmstädter Echo ambalo linauliza, "Je mwaka mmoja wa rais wa Marekani Barack Obama kuwa madarakani umeupeleka mbele ulimwenguni angalau kwa hatua moja?"

Mhariri wa gazeti la Darmstäter Echo anajibu swali hilo akisema: kadri mtu anavyosafiri katika nchi nyingine zilizo mbali na Marekani, jibu linalosikika kwa sauti kubwa ni ndio! Sifa nyingi kwa Obama hazisaidii kitu kwani ingawa umaarufu wake barani Ulaya bado ni mkubwa na haujaporomoka, nchini kwake Marekani hali ya kuvunjika moyo imeenea miongoni mwa Wamarekani wengi. Hii ni kwa kuwa mwaka mmoja tangu rais Obama ashike hatamu za uongozi, bado hajatimiza ahadi yoyote kubwa miongoni mwa ahadi alizozitoa.

Nalo gazeti la Neue Osnabrücker Zeitung linathibitisha kwamba rais Obama hajapata maksi nzuri katika kipindi hiki cha mwaka mmoja madarakani.

Mhariri wa gazeti hilo la Osnabrücker Zeitung anasema rais Obama anastahili kabisa kupata maksi chache. Ni haki kwani hajatimiza matarajio yote waliyokuwa nayo wapiga kura wa Marekani waliomchagua na pia watu wa sehemu mbalimbali za ulimwengu waliokuwa na matumaini makubwa kwa rais Obama.

Gazeti la Leipziger Volkszeitung linadokeza kuwa sera ya kidplomasia ya rais Obama inabakia kuwa sahihi kama juhudi zake kubwa za kutaka ulimwengu uwe huru kutokana na silaha za nyuklia.

Gazeti linaongeza kusema mfumo wa kidplomasia wa rais Obama pamoja na bidii aliyonayo kuhakikisha ulimwengu huru usiokuwa na silaha za nyuklia ni mambo yasiyo na mbadala. Ni kama vile anavyoshinikiza kupatikana kwa suluhisho la haraka katika mzozo nchini Afghanistan, ambako rais Obama ameahidi kumaliza vita nchini humo kwa kuongeza wanajeshi zaidi.

Mhariri wa gazeti la Leipziger Zeitung anasema, hata hivyo au pengine, ndio maana kwa wakati huu matumaini bado yapo rais Obama kushinda tuzo ya amani ya Nobel katika miaka mitatu ijayo maana anastahili. Haitakuwa vibaya kwa ulimwengu mzima, linamalizia gazeti hilo.

Kuhusu bajeti ya Ujerumani mwaka huu wa 2010 itakayojadiliwa bungeni wiki hii, gazeti la Neue Westfälische kutoka Bielefeld linasema hali ni ya kukatisha tamaa.

Serikali ya Ujerumani ina nakisi ya bajeti ya kiasi cha Euro bilioni 85,8. Mhariri wa Neue Westfälische anasema serikali haina chaguo lengine kwa kuwa bado inakabiliwa na mgogoro wa kifedha na kiuchumi. Matumaini ya Wajerumani sasa yanabebwa na waziri wa fedha, Wolfgang Schäuble, ambaye ameahidi kupunguza matumizi ya fedha katika serikali kuu kuanzia mwaka ujao.

Bundesinnenminister Wolfgang Schäuble

Waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble

Gazeti la Frankfurter Allgemeine Zeitung, kwa upande wake, linamkosoa waziri wa fedha, Wolfgang Schäuble.

Gazeti linasema waziri Schaüble anazungumzia uaminifu katika uchumi, lakini hazungumzii kinaga ubaga deni kubwa lililopo serikalini. Anaahidi kulipunguza deni hilo, lakini haelezi vipi anavyotaka kulifikia lengo hilo.

Tukimalizia na mada kuhusu kukatiliwa kwa waziri wa mambo ya kigeni wa Bulgaria, Rumania Jeleva, kuwa kamishna wa Umoja wa Ulaya, gazeti la Frankfurter Rundschau linasema bunge la Ulaya linaweza kujivunia kwa ushujaa wake.

Rumjana Schelewa Kandidatin für die EU Kommission

Akiyekuwa kamishna mteule wa Bulgaria katika Umoja wa Ulaya Rumiana Jeleva

Hatua ya bunge la Ulaya kumzuia Jeleva kuwa kamishna wa Umoja wa Ulaya imesababisha pia kujiuzulu wadhifa wake wa waziri wa mashauri ya kigeni wa Bulgaria. Gazeti linasema Jeleva hakuweza kuwasilisha hoja za kusisimua na alishindwa kuthibitisha kwamba ni mwanasiasa shupavu. Mhariri anamalizia kwa kusema mtu wa aina hiyo hana kitu cha kutafuta katika makao makuu ya Umoja wa Ulaya mjini Brussels, Ubelgiji.

Mwandishi: Josephat Charo/ Deutsche Presse

Mhariri: Othman Miraj

 • Tarehe 20.01.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LbUm
 • Tarehe 20.01.2010
 • Mwandishi Josephat Nyiro Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/LbUm