Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo | Magazetini | DW | 12.11.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo

Wahariri wa magezeti ya Ujerumani hii leo wamejishughulisha na ziara ya kansela Angela Merkel nchini Marekani. Kansela Merkel pamoja na rais George W Bush wa Marekani wanataka kuutanzua mgogoro wa kinyuklia wa Iran kwa njia ya amani.

Tangu kutokea uvumi kwamba Marekani inataka kuishambulia kijeshi Iran, rais Bush alizungumzia matumizi ya juhudi za kidiplomasia kuumaliza mzozo wa Iran wakati alipokutana na kansela Merkel nyumbani kwake huko Crawford katika jimbo la Texas. Bi Merkel akiwa mjini Texas alionekana mwenye matumaini kuwa suluhisho la kidiplomasia linaweza kupatikana.

Gazeti la Die Welt la mjini Berlin linailinganisha ziara ya rais wa Ufaransa, Nicolas Sarkozy na ziara ya kansela Merkel nchini Marekani. Mhariri anasema rais Bush alionekana mchangamfu wakati wa ziara ya kansela Merkel kuliko siku mbili alizokutana na rais Sarkozy huko Vernon. Hakuna cha kusisimua ambacho wapigaji picha wangeweza kukipata, lakini kwa upande wa ziara ya Merkel, rais Bush alifanya matembezi wakati wa asubuhi na kusikiliza ndege wakiimba shambani kwake huko Texas.

Mhariri anasema pengine wakati wakitembea walizungumzia juu ya mipaka katika mzozo wa Iran na kwamba Urusi bado inatakiwa kushirikishwa katika kutafuta ufumbuzi wa mzozo huo. Rais Bush aliweza kulijadili swala la Iran na kansela Merkel. Ikiwa rais Bush atashawishika kufikia mwaka ujao, swala la Iran litahitaji dhihirisho la nguvu na uwezo.

Gazeti la Tagesszeitung kutoka mjini Berlin linaona kwamba kansela Merkel yuko katika nafasi nzuri. Merkel yuko hatua chache mbele ya rais Sayrkozy. Sarkozy alianza kuilekeza Ufaransa katika njia ya ushirikiano wa kirafiki na Marekani wiki iliyopita. Rais Bush amewashukuru marafiki wake wawili kwa kuwa katika ngazi ya kimataifa sio serikali nyingi zinazoikumbatia serikali ya Marekani. Mbali na hayo hakuna serikali inayokutaka kushirikiana na Marekani.

Zamani Ujerumani haikuwa mshirika muhimu sana wa Marekani, lakini sasa Marekani inaihitaji Ujerumani na Ufaransa ziwe katika upande wake. Kupitia harakati zake za kijeshi na diplomasia yake ya utata, Marekani imedhoofika na sasa inaitegemea sana Ulaya katika kuitanzua migogoro ya kimataifa. Ila hakuna yeyote mjini Berlin wala Paris anayetakiwa kufura kichwa kwa hilo.

Gazeti la Trierishe Volksfreund linasema kwa kuwa kansela Merkel amefaulu kuzuia mambo fulani katika ziara yake kuliko rais Sarkozy alivyofaulu siku chache huko mjini Washington, kwa kiwango fulani kansela Merkel ni kiongozi wa Ulaya anayechukua usukani katika kufanya mdahalo na ikulu ya Marekani, na kwa hiyo anaweza kuitwa kiongozi aliyefanikiwa.

Gazeti la Mainzer Allgemeine linatoa changamoto. Mhariri anasema ziara ya muda wa saa 46 ya kansela Merkel jimboni Texas inaweza kugharimu uchumi wa Ujerumani fedha nyingi.

Kwa sababu ziara ya kansela Merkel katika shamba la kiongozi mwenye uwezo mkubwa zaidi duniani ina matokeo yake; nayo ni kwamba Ujerumani itakuwa na msimamo mkali zaidi dhidi ya Iran.

Uvamizi wa kijeshi utakuwa suluhisho lengine iwapo Iran itakataa kubadili msimamo wake juu ya mpango wake wa nyuklia. Msimamo huo ulifaulu kutoa ufumbuzi wa mzozo wa nyuklia wa Korea Kaskazini, lakini hii ni kwa sababu nchi hiyo haina mafuta na haina uwezo wa kukabiliana na vikwazo vya kimataifa.

Ujerumani sasa inaingia katika mtego kwa kuwa Iran ni mshirika wake muhimu sana wa kibiashara na uchumi wa Ujerumani unaweza kuathirika na hatua yoyote ya kujaribu kuibana Iran. Kansela Merkel atakabiliw ana kilio kikubwa mara tu atakapojaribu kutimiza ahadi zake kwa rais Bush bila cha ikiwa wala lakini.

 • Tarehe 12.11.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHRg
 • Tarehe 12.11.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHRg
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com