Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo | Magazetini | DW | 29.10.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani leo wamejishuhulisha na programu hiyo mpya ya chama cha SPD na vipi itakavyoiathiri serikali ya mseto mjini Berlin.

Katika mkutano wake wa chama mjini Hamburg, chama cha SPD kimezindua proramu yake mpya. Kutumia mpango huo kinataka kuimarisha utamaduni wake kama chama cha mrengo wa kushoto.

Gazeti la Tagesspiegel kutoka mjini Berlin ambalo limeandika kuwa kampeni ya chama cha SPD sasa imeanza kuchukua mwelekeo na mkakati wake unazidi kuwa wazi. Chama cha SPD kinazidi kusukumwa na upinzani kiegemee zaidi siasa za mrengo wa kushoto, ili upinzani upate uungwaji mkono zaidi na kuwashawishi walioukimbia.

Gazeti la Handelsblatt la mjini Düsseldorf linasema mbiu ya mkutano wa chama cha SPD mjini Hamburg ilikuwa ´Msukumo kwa Wote´. Chama cha SPD kinataka kujitenga na muungano wa vyama vya CDU-CSU. Wakati huo huo kina hisia za tamaa ya kuungwa mkono na sehemu mbalimbali.

Hakuna wakati katika mkutano wa mjini Hamburg uliowasisimua wanachama waliokuwa katika ukumbi wa mkutano huo kama wakati bwana Kurt Beck aliposhikana mkono na Franz Münterfering. Ama kweli ishara hii inapotosha. Hadi kufikia mwanzoni mwa mwaka ujao chama cha SPD kitaitisha mabadiliko zaidi katika mpango wa Hartz IV na pendekezo linalotaka umri wa kustaafu uwe miaka 67.

Mhariri wa gazeti la Landeszeitung kutoka mjini Lüneburg amemtupia macho kansela wa zamani wa Ujerumani Gerhard Schröder. Kana kwamba ilihitajika kuwa ishara ya kubadili mwelekeo wa bwana Schröder, wanachama wa SPD walipendekeza kuweka kikomo cha kasi kwa magari katika barabara kuu za Ujerumani.

Kwamba mazingira yalitumiwa sana, ni jambo lililodhihirika. Lakini pengine hiyo haijahusu kweli mazingira, kwa kuwa chama cha SPD kimedhihirisha wazi kurejea katika siasa za mrengo wa kushoto na hususan pia kwenda kinyume na sera za mageuzi za kiongozi wake wa zamani, Gerhard Schröder.

Ushirikiano na muungano wa CDU-CSU sasa ni wazi kwamba huenda umalizike kabla mwaka wa 2009. Hatari ya washirika wa serikali ya mseto kulazimika kubadili mawazo yao wakati wowote usiojulikana imedhihirika wazi baada ya mkutano wa chama cha SPD mjini Hamburg.

Gazeti la Ostthüringer kutoka mjini Gera linauliza, kwa nini chama cha SPD kinazungumzia nadharia ya demokraisia ya kijamii katika programu yake. Mhariri pia ameuliza kwa nini imelazimu kulifufua wazo hilo ambalo hasa haliungwi mkono katika eneo la mashariki mwa Ujerumani, ni hatua inayobakia kitendawili. Mhariri anauliza ni nani atakayekipigia kura chama cha SPD mashariki mwa Ujerumani ikiwa tayari kuna chama cha Linke ambacho tayari kina sera kama hiyo?

Tunamalizia na gazeti la Mindener Tagesblatt. Mhariri anasema kwa kutumia mkutano wa mjini Hamburg chama cha SPD kimetangaza msimamo wake katika uchaguzi wa mwaka wa 2009 na mgombea wake wa wadhifa wa ukansela pia. Kwamba chama hicho hakitagombea uchaguzi na bwana Kurt Beck kama mgombea wake wa ukansela, ni jambo ambalo sasa si gumu kubashiri.

Ikiwa mpangilio huu utasuluhisha tatizo la utambulisho wa chama na kupungua kwa umaarufu wake katika miezi michache iliyopita, yote yataonekana katika kura ya maoni ijayo, lakini hasa katika chaguzi za majimbo zitakazofanyika mwaka ujao. Mhariri wa gazeti la Handelsblatt anauliza, je ni kwa umbali gani bwana Kurt Beck ataweza kuyafuatilia maswala haya?

 • Tarehe 29.10.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C7l9
 • Tarehe 29.10.2007
 • Mwandishi Josephat Charo
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/C7l9