1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

....

26 Februari 2015

Wahariri leo wanaizingatia ripoti iliyotolewa na shirika la haki za binadamu Amnesty International na juu ya sheria mpya kuhusu Uislamu nchini Austria

https://p.dw.com/p/1Ei7k
Bibi Ensaf Haidar, mke wa mwanaharakati wa mtandao wa kijamii Raif Badawi akipigania haki za mumewe.
Bibi Ensaf Haidar ,mke wa mwanaharakati wa mtandao wa kijamii Raif Badawi akipigania haki za mumewe ,Picha: picture alliance/empics

Gazeti la "Märkische Allgemeine" linasema ripoti iliyotolewa na shirika la kutetea haki za binadamu duniani,Amnesty International inaonyesha kiwango kikubwa cha kukiukwa haki za binadamu katika mwaka uliopita. Katika ripoti hiyo shirika hilo linasema mwaka uliopita ulikuwa wa maafa makubwa sana kuhusu kukiukwa haki za binadamu. Mhariri wa gazeti la "Märkische Allgemeine" anakubaliana kabisa na ripoti hiyo na anasema kwamba binadamu wamefikia katika hatua ya kujiangamiza wenyewe.

Wadhalimu wanatoka nchi za magharibi vile vile

Mhariri wa gazeti la "Märkische Allgemeine" anatilia maanani kwamba wale wanaowatendea binadamu wenzao unyama mkubwa, kama vile, kuwachinja, hawatoki tu katika nchi zinazofadhili ugaidi, bali pia wanatoka katika nchi za magharibi.

Naye mhariri wa "Hannoversche Allgemeine" anasisitiza kwamba mwaka uliopita hauna kifani, katika kukiukwa haki za binadamu, tokea kumalizika vita kuu vya pili. Mhariri huyo anaeleza kwamba kwa sasa wapo watu Milioni 57 duniani walioyakimbia makaazi yao kwa sababu ya vita, njaa au ugaidi.Mhariri huyo anesema binadamu amefikia hatua ya kujiangamiza mwenyewe.

Waislamu wa Austria wapewa sheria mpya
Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" linaizungumzia sheria mpya juu ya Uislamu iliyopitishwa nchini Austria. Mhariri wa gazeti hilo anasema sheria hiyo ni hatua sahihi, na anaeleza kuwa sheria hiyo inaweka misingi inayowawajibisha Waislamu wa Austria juu ya namna ya kuishi katika nchi hiyo.

Gazeti linasema katika msingi wa sheria hiyo Waislamu wa Austria watapaswa kuuabudu Uislamu wa kiulaya! .Maimamu sasa hawatatoka Uturuki kwa wingi kama ambavyo imekuwa hadi sasa na wala fedha za kujengea misikiti kutoka Saudi Arabia hazitaruhusiwa tena kupokewa na mashirika ya kiislamu ya nchini Austria.

Wabunge wa Ujerumani wafumbia macho udhalimu nchini Saudi Arabia


Gazeti la "Mannheimer Morgen" linailaumu serikali ya Ujerumani kwa kuendeleza uhusiano mzuri sana na utawala wa Saudi Arabia bila ya kujali kasoro za ukiukaji wa haki za binadamu katika nchi hiyo. Mhariri wa gazeti hilo anahoji kwamba Wabunge wengi wanaulaani unyama unaofanywa na magaidi wa dola la kiislamu na pia wanavilaani vitendo vinanyoenda kiynume na maadili ya demokrasia na uhuru wa kutoa maoni.

Hata hiyvo mhariri anesema jambo la ajabu ni kwamba Wabunge hao hawasumbuliwi na uhusiano mzuri uliopo baina ya serikali ya Ujerumani na utawala wa Saudi Arabia. Mhariri huyo anaeleza kwamba utawala huo unatenda udhalimu unaofanana na ule wa magaidi wa dola la Kiislamu IS.

Mwandishi:Mtullya Abdu.Deutsche Zeitungen.

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman