1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maoni: Licha ya kufikiwa makubaliano, Brexit bado ni hadaa

Zainab Aziz Mhariri: Grace Patricia Kabogo
28 Desemba 2020

Baada ya Uingereza kujiondoa kwenye Umoja wa Ulaya, hatua zitakazofuata huenda zitakuwa sio ngumu sana kama wengi wanavyohofia. Lakini hatua hiyo inabaki kuwa kosa la kihistoria, anasema mwandishi wa DW Berndt Riegert.

https://p.dw.com/p/3nHuY
London Anti-Brexit Protest
Picha: Tolga Akmen/AFP/Getty Images

Waziri mkuu wa Uingereza na wajumbe wa Umoja wa Ulaya wanaonekana kuipenda tamthilia ya Brexit. Hilo linaweza kuthibitishwa na umma uliokasirika, haswa nchini Uingereza, wanawaona kwamba wajumbe hao walipambana hadi mwisho lakini ni kwa lengo la kuyahifadhi maslahi yao tu.

Mkataba uliofikiwa mnamo usiku wa mkesha wa Krismasi ungeweza kufikiwa miezi mitatu au hata miezi sita iliyopita. Kwa sababu mbali na mabadiliko machache kuhusiana na haki za uvuvi, yaliyobaki yote ni yale yale yaliyokuwa yamependekezwa na Umoja wa Ulaya kwa Uingereza wakati wa msimu uliopita wa kiangazi.

Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris JohnsonPicha: Paul Grover/REUTERS

Kwa vishindo na madaha, Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, anauwasilisha mpango huo kwa raia wake kama mafanikio mazuri kabisa. Anasema kwa majivuno, ahadi zote zilizotolewa wakati wa kampeni ya kura ya maoni kuhusu Brexit mnamo mwaka 2016 sasa zitatekelezwa.

Mhasiriwa wa utaifa mamboleo

Mfano mmoja wa kuonyesha waliopata hasara kutokana na mkataba huo wa Brexit ni wanafunzi wa Uingereza, ambao hawataweza tena kushiriki katika mpango wa masomo wa kubadilishana wa Erasmus ambao Uingereza uliuona kuwa ni ghali sana kwa serikali yake. Pia kwa sasa itakuwa vigumu zaidi kwa wasomi vijana kutoka nchi za nje kwenda kusoma Uingereza na badala yake jamii ya Uingereza italazimika kulipa gharama kubwa kuliko ada iliyokuwa inalipwa kwenye mpango wa masomo wa Erasmus.

Wanafunzi wa vyuo vikuu ndio watakaohasiriwa zaidi na Brexit
Wanafunzi wa vyuo vikuu ndio watakaohasiriwa zaidi na BrexitPicha: Chris Ison/empics/picture alliance

Waziri Mkuu Boris Johnson, kwa ujanja anawavutia raia wa Uingereza kwa kudai kuwa nchi hiyo imechukua udhibiti wake tena lakini ukweli ni kwamba bado hajaikwamua nchi yake kabisa kutoka kwenye mfungamano na Brussels na wala hakuna nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya inayotawaliwa na nchi nyingine bali nchi zinashirikiana katika misingi ya kisheria. Hakuna nchi inayolazimishwa kuwa mwanachama.

Dhana ya kupotosha kuhusu uhuru

Boris Johnson sasa anazungumza jinsi Uingereza ilivyojikomboa na kuwa huru tena swali ni je Uhuru huo ni kutoka kwa nani? Waziri mkuu na marafiki zake wa Brexit wanajidanganya kwa wazo hilo la kuwa huru tangu karne iliyopita, wakati meli za Uingereza zilipotawala bahari kama mhimili wa ulimwengu.

Leo hii, serikali yoyote inayotaka kushiriki katika biashara na uhusiano wa kimataifa lazima itoe sehemu ndogo ya uhuru wake ili kufurahiya faida za ushirikiano. Uwanachama katika Shirika la Biashara Ulimwenguni WTO, Umoja wa Mataifa, NATO, na pia Umoja wa Ulaya, huja na majukumu pamoja na haki kubwa na ndogo. Kwa yote haya hakuna nchi inayopaswa kutoa uhuru wake wa kujitawala kwa ajili ya kuyapata yote hayo.

Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen
Rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der LeyenPicha: Francisco Seco/REUTERS

Katikati ya janga la corona ambapo Uingereza imeathirika zaidi, Boris Johnson alipaswa kujua kuwa yalikuwepo mambo muhimu zaidi kuliko kufukuzia ndoto za ubinafsi. Alisahau kuwa Uingereza na Umoja wa Ulaya ziko karibu sana kwani siku mbili tu za kufungwa njia ya mfereji wa bahari kati ya Uingereza na Ufaransa zingemwonyesha ni kwa kiasi gani Uingereza inavyoweza kuathirika.

Wengine wanaofanana na wakereketwa wa Brexit ni Poland na Hungary, ambao pia wanahisi nchi zao zinamilikiwa au ni watumwa wa Umoja wa Ulaya, jumuiya ambayo kwa hiari yao wao ni wanachama.

Ukweli ni kwamba Brexit itaendelea kuwa hadaa. Waingereza walikuwa na hali nzuri ndani ya Umoja wa Ulaya bila ya maneno mengi ya Boris Johnson.

Chanzo:/https://p.dw.com/p/3nDdF