1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kiongozi mkuu wa genge la wahalifu Haiti, Ti Greg auawa

22 Machi 2024

Kiongozi wa genge la wahalifu la Delmas 95, Ti Greg ameuawa na polisi siku moja tu baada ya kiongozi mwengine wa genge la wahalifu kuuawa, hayo yanajiri wakati baraza la mpito likiwa linakaribia kukamilika

https://p.dw.com/p/4e0b1
Haiti - Makabiliano
Kiongozi mkuu wa genge la wahalifu la Delmas 95, Ti Greg ameuawa katika makabiliano baina ya polisiPicha: Odelyn Joseph/AP/picture alliance

Huko nchini Haiti, Mmoja wa viongozi wa genge la wahalifu la Delmas 95, Ti Greg ameuwawa wakati baraza la mpito likiwa linakaribia kukamilika, Kiongozi huyo ameuawa katika makabiliano na polisi, siku moja tu baada ya kiongozi mwengine wa genge la wahalifu kuuawa.

Soma zaidi. Kiongozi wa genge la wahalifu nchini Haiti Ti Greg auawa

Makabaliano kati ya polisi na magenge ya wahalifu nchini Haiti yamezidi kupamba moto katika eneo la Petion Ville, eneo lilipo kwenye mji mkuu wa nchi hiyo wa Port-au-Prince.

Katika makabiliano ya jana, Polisi wamethibitisha kuuawa kwa Kiongozi Mkuu wa genge la wahalifu la Delmas 95, Ernst Julme, anayejulikana kama Ti Greg, ikiwa ni siku moja baada ya kiongozi mwingine wa genge la wahalifu kuuawa katika kile polisi walichoeleza kuwa ni kuzuka upya kwa mashambulizi ya makundi hasimu ya magenge.

Haiti |  Port-au-Prince
Jimmy Cherizer, Afisa wa zamani wa polisi ambaye kwa sasa anaongoza genge la wahalifu la G9 nchini HaitiPicha: Joseph Odelyn/AP Photo/picture alliance

Kifo cha Julme au Ti Greg ambaye alikuwa ametoroka gerezani hivi karibuni,  ni pigo kwa mipango ya magenge ya wahalifu yanayolenga kuchukua udhibiti wa sehemu kubwa ya mji mkuu Port-au-Prince.

UN:Tumepokea orodha ya baraza la mpito Haiti

Kwa upande mwingine, Naibu Msemaji wa katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa , Farhan Haq, amesema kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amepokea ripoti kwamba makundi ya kisiasa nchini Haiti yamechagua wanachama wa baraza la mpito ambalo litachukua nafasi ya urais kabla ya uchaguzi ujao.

Baraza hilo, lilinuia kuwaleta pamoja viongozi wa kisiasa nchini Haiti ambao kwa muda mrefu hawajawa kwenye maelewano, Baraza limepewa jukumu la kuteua mbadala wa Waziri Mkuu Ariel Henry, ambaye alitangaza kujiuzulu mnamo machi 11 huku ghasia za magenge zikizuia kurejea kwake nchini humo.

Soma zaidi. Mji mkuu wa Haiti wakabiliwa na mashambulizi mapya ya magenge

Akihutubia mkutano wa waandishi wa habari kutoka Haiti kwa njia ya video, Mratibu wa misaada ya kibinadamu wa Umoja wa Mataifa wa taifa hilo la kanda ya Karibea Ulrika Richardson amesema shughuli za kila siku nchini humo zimesimama na watu wengi wameyakimbia makazi yao.

Katar Doha | UN Konferenz - Antonio Guterres
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amepokea ripoti kwamba makundi ya kisiasa nchini Haiti kwamba makundi ya kisiasa nchini Haiti yamechagua wanachama wa baraza la mpitoPicha: Karim Jaafar/AFP/Getty Images

"Hali hapa Haiti na haswa hapa Port-au-Prince ni mbaya, ya wasiwasi mkubwa na inatisha sana. Na kile tulicho nacho kwa sasa Haiti, ni wazi, ni mgogoro wa kibinadamu wa kiwango kikubwa kabisa. Na hayo ni matokeo ya muundo wa ukosefu wa utulivu wa kisiasa na ukosefu wa usalama uliokithiri, bila shaka hili ndiojambo ambalo pia tunalo na ambalo tunalifuatilia kwa ukaribu." amesema Ulrika.

Soma zaidi. Vikosi vya usalama- vyazima jaribio la kushambulia Benki Kuu ya Haiti

Mpango wa kukamilisha baraza la mpito ulisimamiwa huko Jamaica na Jumuiya ya serikali za nchi za Karibea (CARICOM), pamoja na wawakilishi wa serikali ya Haiti na wale wa upinzani. 

Jumuiya hiyo tayari imetoa orodha ya makundi ya kisiasa ambayo yanatarajiwa kuwakilishwa ndani ya baraza hilo.

Hata wakati hayo yakiendelea, Bado magenge ya wahalifu yanameendelea kuchukua udhibiti katika meneo ya mji mkuu wa Haiti wa Port-au Prince. Mataifa kama Marekani yameendelea kuwaondoa raia wake nchini Haiti, hapo jana  Marekani ilifanikisha kuwaondoa raia wake 90 waliokuwa katika mji wa kaskazini mwa nchi hiyo wa Cap Haiten.