1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maelezo juu ya kifo cha Bhutto yatatanisha

29 Desemba 2007
https://p.dw.com/p/Chgq

ISLAMABAD

Wizara ya mambo ya ndani ya Pakistan imesema kundi la Al Qaeda na waasi wa Taliban wanahusika na kifo cha Waziri Mkuu wa zamani wa nchi hiyo Banazir Bhutto.

Msemaji wa Wizara ya mambo ya ndani Brigedia Generali Javed Cheema pia amesema kwamba Bhutto hakuuwawa kwa kupigwa risasi au kutokana na vipande vya shambulio la bomu la kujitolea muhanga.

Cheema anasema wakati Bhutto alipojaribu kukwepa shambulio la mripuko wa bomu kwa kuinama chini alirushwa na mtingishiko wa mripuko huo wa bomu na kwa bahati mbaya kichwa chake kikagonga kipaa cha jua cha gari na kusababisha mpasuko kwenye bufuru lake na hicho ndicho kilichosababisha kifo chake.

Lakini Farooq Naik mwanasheria mkuu wa Bhutto na afisa mwandamizi wa chama cha Bhutto cha PPP ametupilia mbali maelezo hayo ya serikali kuwa hayana msingi bali na mkururo wa uongo na kwamba risasi mbili zilimpata mama huyo moja tumboni na nyengine kichwani.

Chama cha Bhutto kinasema serikali ya Rais Pervez Musharraf inajaribu kuficha kushindwa kwake kumlinda Bhutto.

Maelfu ya waombolezaji wamehudhuria mazishi ya Bhutto katika jimbo la Sindh hapo jana.

Takriban watu 32 wameuwawa kutokana na ghasia zilizozuka baada ya kuuwawa kwa Bhutto hapo Alhamisi.