Maafa ya nyuklia bado mada kuu kwenye magazeti ya Ujerumani | Magazetini | DW | 15.03.2011
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Maafa ya nyuklia bado mada kuu kwenye magazeti ya Ujerumani

Katika maoni yao ya leo (15.03.2011), wahariri wa magazeti ya Ujerumani waunga mkono uamuzi wa serikali kuendelea kusubiri uamuzi wa kurefusha matumizi ya nishati ya nyuklia.

Afisa wa Kijapani katika mavazi ya kujikinga na mionzi ya nyuklia

Afisa wa Kijapani katika mavazi ya kujikinga na mionzi ya nyuklia

Kutokana na maafa yaliyosababishwa na kuripuka vinu vya nishati ya nyuklia nchini Japan, mjadala mkubwa umezuka tena nchini Ujerumani juu ya hatari ya nishati hiyo.

Serikali sasa imeamua kusimamisha kwa miezi mitatu, muda wa kurefusha matumizi ya vinu vya nyuklia. Lakini je, hatua hiyo inatosha?

Mhariri wa gazeti la Der Neue Tag anasema kwa muda mrefu watu nchini Ujerumani wamekuwa wanaambiwa kwamba vinu vya nishati ya nyuklia vimo katika hali salama kuliko vinu vingine kwengineko kote duniani.

Lakini sasa, ghafla serikali ya Ujerumani imeamua kuvifunga vinu vikuukuu mara moja. Pia itaongeza kwa miezi mitatu muda wa kusubiri kuanza kwa hatua ya kurefusha matumizi ya vinu hivyo.

Je, hatua hiyo inatokana na kutambua kwamba, wakati wote pana hatari ya kutokea maafa au uamuzi huyo umechukuliwa kwa sababu ya kampeni za uchaguzi?

Mhariri wa gazeti la Flensburger Tageblatt anauunga mkongo uamuzi wa serikali ya Ujerumani wa kuvifunga vinu vikuukuu mara moja.

Mhariri huyo anaeleza kuwa, ingawa uamuzi huo hauna maana ya Ujerumani kuacha mara moja kutumia nishati ya nyuklia, bado ni hatua ya busara, kwani jambo muhimu siyo kuvuta muda, bali ni hekima ya usalama.

Sababu ni kwamba, hata ikiwa Ujerumani itajitoa haraka katika matumizi ya nishati ya nyuklia, bado patakuwa na maswali mengi ya kujibiwa. Kwa mfano, taka za nyuklia zitapelekwa wapi? Na je, nini kitatokea kwa vinu vya nyuklia katika nchi za jirani?

Lakini pamoja na yote hayo, jambo moja ni muhimu, kwamba Ujerumani haitarejea tena katika mtazamo wa miaka iliyopita juu ya nishati ya nyuklia.

Mhariri wa gazeti la Nürmberger Nachrichten pia anaipongeza serikali kwa uamuzi wa kusimamisha hatua ya kurefusha muda wa matumizi ya vinu vya nyuklia, lakini anasema serikali imeupitisha uamuzi huo ili kujiongezea siku.

Kutokana na maafa yanayotokea Japan, uamuzi wa serikali ya Ujerumani wa kuongeza kusimamisha muda wa kuitekeleza hatua ya kurefusha matumizi ya vinu vya nyuklia nchini, unaonekana kuwa ni hatua ya busara. Lakini serikali hiyo inahitaji muda huo angalau hadi wakati wa kufanyika uchaguzi.

Hapo awali serikali ilisema ilivihitaji vinu vya nyuklia kama hatua ya mpito tu katika tekinolojia. Lakini sasa serikali hiyo inahitaji muda huo wa miezi mitatu mpaka wakati wa uchaguzi na kuvuka hapo.

Mwandishi: Abdul-Mtullya/ Dt.Agenturen/Deutsche Zeitungen/
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman