1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Lipumba aitaka serikali kuionya Urusi kuhusu kundi la Wagner

George Njogopa26 Januari 2023

Chama cha upinzani nchini Tanzania cha CUF kimeitaka serikali ya nchi hiyo kufanya uchunguzi wa kina kubaini iwapo kuna Watanzania wengine waliojiunga na kundi la wapiganaji mamluki wa nchini Urusi la Wagner.

https://p.dw.com/p/4Mk7O
Mwenye kiti wa Chama cha upinzani cha CUF nchini Tanzania, Profesa Ibrahim Lipumba
Mwenye kiti wa Chama cha upinzani cha CUF nchini Tanzania, Profesa Ibrahim LipumbaPicha: DW/S. Khamis

Mwenyekiti wa chama hicho cha CUF, Ibrahim Lipumba ambaye amekuwa na mkutano na waandishi wa habari amesema serikali ya Tanzania inawajibu wa kuitamkia bayana Urusi kutowatumia raia wa Tanzania katika kundi hilo la Wagner au kuwajumuisha katika vita inayoendelea baina ya Moscow na Ukraine.

Mwanasiasa huyo anaona kwamba mamlaka nchini Tanzania zinayo dhima ya kuhakikisha kwamba hakuna raia yoyote anayeingizwa kwenye mitego ya aina hiyo hata kama baadhi yao wanashawishiwa kwa ahadi ya kupata mafungu manono ya fedha.

Mtanzania huyo aliyefahamika kwa jina la Nemes Kimaro alifariki dunia hivi karibuni, wakati akiwa na vikosi vya kundi binafsi la Ulinzi la Urusi, Wagner ambalo wapiganaji wake wanashiriki vita hiyo bega kwa bega na majeshi ya Urusi huko Ukraine.

Mamluki wa Kiafrika kwenye kundi la Wagner 

Vikosi binafsi vya jeshi la Urusi la Wagner na wanajeshi wa Ukraine wamekuwa wakipambana nchini Ukraine
Vikosi binafsi vya jeshi la Urusi la Wagner na wanajeshi wa Ukraine wamekuwa wakipambana nchini UkrainePicha: Igor Russak/REUTERS

Duru za habari zinasema alijiunga na vikosi hivyo baada ya kuondolewa kutoka gerezani na kwamba baada ya kutumika katika vita hivyo aliahidiwa kupatiwa kiasi cha fedha na kisha kuruhusiwa kurejea uraiani nyumbani.

Mwili wake ulitazamiwa kuwasili leo jioni ukitokea Moscow, Urusi na baadaye kupokelewa na familia yake yenye maskani yake maeneo ya Kimara jijini Dar es salaam.

Akuzungumzia tukio hilo, hivi karibuni Waziri wa mambo ya nje, Stergomena Tax alionya kuhusu raia wa Tanzania kujiunga na vikosi vya kigeni akisema mwenendo huo haukubaliki kisheria.

Kundi la Wagner linatajwa kuwa na uzoefu wa kuwasajili raia wengi wa kigeni wanaotumika katika maeneo yenye mizozo na baadaye kuahidi kuwapatia ujira mnono wa malipo ya fedha baada ya wakiwa wamekamilisha operesheni zao.