Lavrov afanya mazungumzo na Tillerson | Matukio ya Kisiasa | DW | 06.08.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Lavrov afanya mazungumzo na Tillerson

Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov na mwenzake wa Marekani Rex Tillerson wamekutana leo hii kwa mazungumzo marefu katika wakati ambapo kuna mvutano kati ya mataifa yao.

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi Sergei lavrov amesema anaamini wenzake wa Marekani wako tayari kuendeleza mazungumzo na Urusi kuhusu masuala magumu licha ya mivutano ya mahusiano kati ya nchi hizo mbili

Lavrov aliyekutna na Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Marekani Rex Tillerson pembezoni mwa mkutano wa kimataifa mjini Manila, Ufilipino, amesema kitu cha kwanza ambacho Tillerson aliuliza ni kuhusu kulipiza kisasi kwa Urusi dhidi ya vikwazo vipya vya Marekani dhidi ya nchi hiyo.

Mkutano huo ulikuwa wa kwanza tangu Rais Donald Trump alisaini kuwa sharia vikwazo ambavyo Urusi ilisema vinatangaza vita kamili na kumaliza kabisa matumaini ya kuimarisha mahusiano ya nchi hizo mbili.

Deutschland | Hamburg - G20 Donald Trump und Vladimir Putin (picture-alliance/AP Photo/E. Vucci)

Mahusiano kati ya Urusi na Marekani yamesambaratika

Lavrov amesema pia alimtaja Rais Vladmir Putin, ambaye katika mahojiano na televisheni ya Urusi wiki iliyopita, alifafanua haja ya Urusi kulipiza kisasi dhidi ya vikwazo vya Marekani kuhusiana na jukumu lake katika mzozo wa Ukraine na hivi karibuni vikaongezwa ili kuiadhibu Urusi kwa kuingilia uchaguzi wa rais nchini Marekani.

Lavrov aliyataja mazungumzo yake na Tillerson kuwa marefu na akasema yaligusia mada nyingi pana, kuanzia suala la nyuklia katika rasi ya Korea hadi mipango ya uratibu kati ya Urusi na Marekani ili kustahimili mashambulizi.

Pande hizo mbili zimekubaliana kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Urusi Sergei Ryabkov na mwenzake wa Marekani Thomas A. Shannon wataendelea kujadiliana kuhusu masuala magumu kuhusu ajenda ya nchi hizo mbili.

UKRAINE

Akizungumza kwenye televisheni ya taifa ya Rossiya24, Lavrov pia amesema kuwa Tillerson alimwambia mwakilishi maalum wa Marekani kuhusu Ukraine, Kurt Volker, mjumbe wa zamani wa Marekani katika Jumuiya ya Kujihami ya NATO, atakutana na mshauri wa Putin, Vladmir Surkov, "katika siku zijazo"

Marekani ilimtuma Volker nchini Ukraine mwezi uliopita kutathmini hali katika nchi hiyo ambayo ilikuwa Jamhuri ya uliokuwa muungano wa Kisovieti, ambako makubaliano ya mwaka wa 2015 ya kusitisha vita kati ya majeshi ya Ukraine na wanaharakati wanaopigania kujitenga ambao wanaungwa mkono na Urusi katika mashariki mwa nchi hiyo unavunjwa mara kwa mara. Marekani inasema mgogoro huo ni kizuizi kikuu katika juhudi za kuimarisha mahusiano kati yake na Urusi

Mwandishi: Bruce Amani
Mhariri: Yusra Buwayhid

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com