1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kongamano la kiuchumi lafunguliwa Urusi

6 Juni 2019

Kongamano la kila mwaka la kiuchumi nchini Urusi limefunguliwa mjini Saint Petesburg wakati ikiwa katika mzozo na magharibi huku wawekezaji wa kigeni wakiwa wamekatishwa tamaa na ukuaji wa taratibu wa uchumi.

https://p.dw.com/p/3JyZn
Russland Moskau | Präsidenten Wladimir Putin & Xi Jinping, China
Picha: Reuters/E. Novozhenina

Kongamano la kila mwaka linalojadili masuala ya kiuchumi nchini Urusi limefunguliwa hii leo mjini Saint Petesburg, huku lengo kuu kwa taifa hilo likiwa ni kurejesha imani kwa wawekezaji wa kigeni ambao wamekatishwa tamaa na ukuaji wa taratibu wa uchumi tangu mwanzoni mwa mwaka huu. 

Kongamano hilo la kimataifa la uchumi ambalo hapo awali liliitwa "Russian Davos", na wakati ambapo uchumi wa nchi hiyo ulikuwa ukinawiri, limeandaliwa na rais Vladmir Putin na linafanyika wakati wakiwa kwenye mvutano na mataifa ya Magharibi.

Rais wa China Xi Jinping ni mgeni wa heshima kwenye kongamano hilo. Kuhudhuria kwake kunachukuliwa kama ishara kwamba Urusi inabadilisha mkondo kisiasa na uchumi kuelekea mashariki. Jinping atahutubia mkutano huo pamoja na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres kesho Ijumaa.

Karlspreis für UN-Generalsekretär Guterres
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres atahutubia pia kongamano hilo la uchumiPicha: picture-alliance/dpa/H. Kaiser

Mapema hii leo, rais Putin na Jinping walizungumza na vyombo vya habari baada ya kukutana na Jinping. "Ningependa kwa mara nyingine nimshukuru Xi Jinping pamoja na wenzetu kutoka China kwa kazi nzuri tunayoifanya kwa pamoja. Lakini pia napenda kuelezea imani yangu kwamba kwamba makubaliano tuliyofikia yataimarisha zaidi mashirikiano kati ya China na Urusi." alisema Putin

Suala la kukamatwa kwa mfanyabiashara maafuru wa Marekani Michael Carvey, ambaye ni mwasisi wa kampuni kubwa ya uwekezaji nchini Urusi ya Baring Vostok huenda likagubika fikra za wengi. Carvey aliye katika kifungo cha nyumbani alikamatwa pamoja na wenzake watano kwa madai ya ufisadi ingawa anasema madai hayo yaliibuliwa kufuatia mzozo na mbia mwenzake. 

Mwenzake raia wa Ufaransa Philippe Delpal yuko kizuizini akisubiri mashitaka. Balozi wa Marekani nchini Urusi amesusia kongamano hilo, huku Ufaransa ikituma balozi badala ya waziri, tofauti na mwaka kongamano lililopita ambapo rais Emmanuel Macron  aliongozana na ujumbe mkubwa kuhudhuria kongamano hilo.

Alexei Kudrin Russland Moskau
Alexei Kudrin amekiri suala la Carvey limetikisa uchumi wa UrusiPicha: Imago Images/Kremlin Pool

Mkuu wa taasisi ya ukaguzi ya Urusi Alexei Kudrin amekiri kwamba suala hilo limeleta mshituko kwenye  sekta ya uchumi. Lakini, waziri wa fedha Anton Siluanov amesema majadiliano kuhusu suala hilo yanaendelea huku akitoa mwito wa suala ya uhuru wa mahakama kutizamwa mapana yake.

Baada ya miaka miwili ya mdororo wa kiuchumi uliosababishwa na kuanguka kwa bei ya mafuta pamoja na vikwazo ilivyowekewa urusi kutokana na ushiriki wake kwenye mzozo wa Ukraine uchumi wa taifa hilo uliimarika mwaka 2017 lakini hadi robo ya kwanza ya mwaka huu umepanda kwa asilimia 0.5 tu. Kwa maana hiyo inahitaji uwekezaji wa hali na mali.

Miradi inayotajwa kuwa ya kitaifa kuanzia ya afya hadi miundombinu inapangwa kumalizika ifikapo mwaka 2024 na itagharimu dola bilioni 388. Takriban dola bilioni 115 zitatokana na uwekezaji binafsi wa ndani na wa kigeni.

Waziri wa Uchumi Maxim Oreshkin amesema huku akiangazia hatari zitokanazo na kupungua kwa mikopo ya watumiaji kuwa kama hakutachukuliwa hatua kuna uwezekano kwa taifa hilo kukumbwa na mdororo mwingine wa kiuchumi ifikapo mwaka 2021.