Kongamano la kimataifa la kiuchumi mjini Davos | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.01.2016
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Kongamano la kimataifa la kiuchumi mjini Davos

Kongamano la kimataifa la kiuchumi linaendelea Davos. Hotuba ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry na wa ulinzi Ashton Carter zinasubiriwa .Mada iliyohodhi majadiliano ya jana ilihusu umoja wa Ulaya.

default

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron akihutubia kongamano la kimataifa mjini Davos

Viongozi kadhaa wa Ulaya akiwemo pia waziri mkuu wa Ufaransa Manuel Valls wameelezea matumaini yao kuuona Umoja wa Ulaya ukijiepusha na "balaa" la kujitoa Uingereza, lakini Ufaransa inaonya "sio kwa kila hali"."

Akiwa mjini Paris rais Francois Hollande amesisitiza pia umuhimu wa kubakia Uingereza katika Umoja wa ulaya lakini amesisititza atakuwa macho kuhakikisha kanda ya Euro inazidi kujiimarisha.

"Kujitoa Uingereza utakuwa msiba" amesema kwa upande wake waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble aliyeketi karibu na viongozi wa serikali za Ugiriki na Uholanzi kujadiliana kuhusu mustakbal wa Umoja wa Ulaya.

Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron ameamua kuitisha kura ya maoni nchini mwake kuhusu mustakbal wa nchi hiyo ndani ya Umoja wa ulaya. Anashinikiza umoja wa Ulaya ufanyiwe marekebisho. Akifanikiwa kuwafikiana na viongozi wenzake wa Umoja wa ulaya,kura hiyo ya maoni inaweza kuitishwa mwaka huu na Cameron ameahidi kufanya kampeni kwaajili hiyo.

Lakini madai kadhaa yanayotolewa na Cameron yanaangaliwa na baadhi ya viongozi wa Ulaya kuwa "yamepindukia".

Schweiz Davos Weltwirtschaftsforum 2016 Wolfgang Schäuble

Waziri wa fedha wa serikali kuu ya Ujerumani Wolfgang Schäuble

Waziri mkuu wa Uiengereza anafafanua kile anachohisi ni muhimu kwa nchi yake akisema:"Tunachokihitaji ni kanuni na muongozo bayana kwa namna ambayo nchi ambayo si mwanachama wa kanda ya Euro,haitojikuta katika hali ya udhaifu, na haitobaguliwa;na tunataka pawepo haki kati ya mifumo iliyoko. Na nnafikiri hilo linawezekana."

Baadhi ya nchi za Ulaya zinahisi katika suala la kurahisishwa shughuli za umoja wa ulaya na pia kuondolewa vizuwizi ili kuimarisha mashindano ya kibiashara-,ridhaa inawezekana. Kizingiti kinakutikana lakini katika suala la kanda ya Euro na huduma za jamii kwa wahamiaji.

Mada hizo tete zitajadiliwa viongozi wa Umoja wa ulaya watakapokutana mwezi ujao mjini Brussels.

Wolfgang Schäuble ataka uanzishwe mpango wa misaada ya dharura

Weltwirtschaftsforum Davos 2016 - Li Yuanchao, Vize-Präsident China

Makamu wa rais wa China Li Yuanchao

Mbali na suala la Uingereza,kikao cha jana mjini Davos kilizungumzia pia wimbi la wakimbizi,ugaidi na kuzidi kupata umaarufu makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia.

Kuhusu wakimbizi waziri wa fedha wa serikali kuu ya Ujerumani ametoa wito wa kubuniwa mpango wa dharura wa msaada kama ule ulioanzishwa na Marekani vita vikuu vya pili vya dunia vilipomalizika.

Kwa upande wa mada za kiuchumi,makamo wa rais wa China Li Yuanchao alihutubia kikao cha jana mjini Davos na kuuhakikishia ulimwengu nchi yake ina auwezo wa kuendeleza ukuaji imara wa kiuchumi .

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP/

Mhariri: Mohammed Khelef

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com