1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AfD yalenga kuimarisha umaarufu wake Ujerumani, Ulaya

Iddi Ssessanga
28 Julai 2023

Kufuatia kuongezeka kwa umaarufu unaovitia kiwewe vyama vikongwe, chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, AfD nchini Ujerumani kinafanya kongamano Ijumaa likiwa na malengo ya ushindi katika uchaguzi wa Ulaya na majimbo.

https://p.dw.com/p/4UVIC
Demonstration der AfD für Energiesicherheit und Inflationsschutz
Picha: Christoph Soeder/dpa/picture alliance

Wanachama wapatao 600  wa AfD wamekusanyika Magdeburg -- mji ulioko katika Ujerumani ya mashariki iliyokuwa zamani ya kikomunisti ambapo chama hicho kina uungwaji mkono mkubwa -- huku makundi yanayopinga itikadi kali yakifanya maandamano nje.

Wakati kongamano hilo likiendelea, AfD iliweka wazi nia yake, huku rais mwenza Alice Weidel akisema chama hicho kilipanga kuweka mgombea wake wa ukansela katika uchaguzi wa kitaifa wa 2025 kwa mara ya kwanza.

Soma pia:Chama cha siasa kali cha AfD chashika nafasi ya pili Ujerumani

Chama hicho kinapanga kujadili mpango wake na wagombeaji wa uchaguzi wa Ulaya mnamo Juni 2024 katika wikendi mbili zijazo.

Kwa nini chama cha AfD ni maarufu mashariki mwa Ujerumani ?

Chama cha Alternative for Germany (AfD) kiliundwa mwaka wa 2013 kama kwa madhumuni ya kupinga matumizi ya sarafu ya Euro, kabla ya kubadilika na kuwa chama kinachopinga Uislamu na uhamiaji na kilitumia wimbi la wakimbizi chini ya kansela Angela Merkel kujiimarisha kisiasa.

Katika kura za maoni za hivi karibuni, AfD imeshika nafasi ya pili katika ngazi ya kitaifa, mbele ya chama cha Social Democrats cha Kansela Olaf Scholz na nyuma kidogo ya muungano wa vyama vya kihafidhina vya CDU na CSU ambao ndiyo chama kikuu cha upinzani.

Soma pia:Kushamiri kwa itikali kali za kulia huenda kukazuwia uhamiaji wafanyakazi wenye ujuzi

Wananufaika kutokana na kutoridhika kwa umma kuelekea muungano tawala wa sasa, unaojumuisha chama cha mrengo wa kati kushoto cha SPD cha Scholz, chama cha Kijani na na Free Democrats, ambacho ni rafiki kwa biashara, pamoja na kutoridhika kutokana na mfumuko mkubwa wa bei na uhamiaji.

Wigo mpana wa wapigakura wanaoiunga mkono AfD

Matthias Jung, kutoka taasisi ya uchunguzi wa maoni ya wapigakura ya Forschungsgruppe Wahlen, aliiambia AFP kuwa chama kinavutia wigo mpana wa wapiga kura wasioridhika.

"Wanatofautiana kutoka kwa kijana aliyejihami na mpira wa besiboli, ambaye ana mtazamo finyu wa ulimwengu, hadi wale walio upande wa kulia kabisa, hadi mtu asiyependa siasa, anayekerwa na sera za sasa za serikali na ambaye haoni upinzani wa kihafidhina kama chama mbadala wa kuaminika."    

Andrea Roemmele, kutoka Shule ya Utawala ya Hertie ya Berlin, aliongeza: "Wanachama wa serikali ya Ujerumani wanatumia muda wao kubishana... wakati AfD imeacha nyuma ugomvi (wa ndani) ambao ulikuwa ukiwatia hofu wafuasi wake."

Soma pia: Misimamo mikali ya mrengo wa kulia yaongezeka Ujerumani

Hali si shwari ndani ya chama cha AfD

AfD imekuwa na mafanikio haswa mashariki mwa Ujerumani, ambapo wengi wanahisi kuwa walipoteza kutokana na kuungana tena kwa pande mbili mnamo 1990.

AfD tayari inapata uungwaji mkono wa takriban asilimia 30 katika kura za maoni mashariki mwa nchi.

Majimbo ya Thuringia, Saxony na Brandenburg yatapigia kura kuchaguwa wawakilishi wa mabunge yao Septemba 2024, na kuna uwezekano kwamba katika angalau moja ya mabunge matatu AfD itashinda viti vingi zaidi.

Katika majimbo ya magharibi ya Bavaria na Hesse, ambako uchaguzi wa majimbo utafanyika Oktoba hii, AfD ina uungwaji mkono fulani lakini inadumaa katika uchunguzi wa maoni ya wapigakura.

Chanzo: AFPE