1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kisa cha Kuuliwa Khashoggi chazidi Kuhanikiza Magazetini

Oumilkheir Hamidou
24 Oktoba 2018

Kuuliwa Jamal Khashoggi katika ubalozi mdogo wa Uturuki, kukataliwa kwa mswaada wa bajeti ya Italia na halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya na uchunguzi wa shirika la OECD kuhusu elimu ni miongoni mwa mada magazetini.

https://p.dw.com/p/375Vs
Türkei | Fall Khashoggi
Picha: Reuters

 

 

Tunaanzia njia panda inayoiunganisha Uturuki na Saudi Arabia. Gazeti la "Mannheimer Morgen" linazungumzia kitendawili cha kuuliwa Jamal Khashoggi, mwandishi habari mashuhuri na mkosoaji mkubwa wa mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman. Gazeti linajikita katika kile kilichosemwa na rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan bungeni na kuandika: "Kwa mara nyengine tena Erdogan ameonyesha jinsi anavyochanganya siasa na karata. Suala watu wanalojiuliza ni jee Erdogan kweli ana ushahidi kibindoni, unaodhihirisha kile kilichomsibu Khashoggi alipokuwa katika ubalozi mdogo wa Saudi Arabia mjini Istanbul? Ushahidi kwa hivyo unaozisuta hoja za upuuzi zilizotolewa na viongozi wa Saudi Arabia eti Khashoggi ameuwawa kwa bahati mbaya baada ya ugomvi kutokea."

Erdogan anataka kuleta mfarakano

Gazeti la "Badische Zeitung" linasema Erdogan anataka kusababisha mfarakano kati ya mfalme Salman wa Saudi Arabia na mwanawe wa kiume anaesemekana ndie aliyetoa amri ya kuuliwa Khashoggi. Gazeti linaandika: "Erdogan anataka zaidi kuhakikisha mwanamfalme huyo anang'oka madarakani. Na ili kulifikia lengo hilo anahitaji uungaji mkono wa rais wa Marekani Donald Trump na ndio maana anatilia mkazo umuhimu wa kushirikiana na Marekani. Idara ya upelelezi ya CIA inahusishwa katika uchunguzi ili kumtanabahisha rais Trump  sera yake kuelekea Mashariki ya kati haitotekelezeka ikiwa anamhusisha mwanamfalme Mohammed bin Salman."

Mswaada wa bajeti ya italia wakataliwa

Gazeti hilo hilo la "Badische Zeitung" la mjini Karlsruhe linaripoti kuhusu mzozo ulioripuka kati ya halmashauri kuu ya Umoja wa ulaya na Italia. Chanzo ni mswaada wa bajeti ambayo haiambatani na muongozo wa kudhamini utulivu wa sarafu ya Euro. Viongozi wa Italia wanashikilia hawatopendekeza nyengine. Gazeti linaendelea kuandika: "Sihaba hatimae halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya imesimama kidete dhidi ya wanaokiuka masharti ya bajeti. Serikali ya wanaopigania uzalendo mjini Roma imepewa muda wa wiki tatu iwasilishe mswaada uliofanyiwa marekebisho. Kisa hiki ni cha aina yake. Hadi wakati huu halmashauri kuu ya Umoja wa wa ulaya haijawahi kuukataa mswaada wa bajeti ulipendekezwa na nchi mwanachama."

Eti elimu ni matajiri tu

Mada yetu ya mwisho magazetini inatupeleka Paris ambako shirika la kimataifa la ushirikiano wa kiuchumi na Maendeleo OECD limechapisha ripoti yake ya mwaka kuhusu hali ya elimu duniani. OECD linasi bado watoto wa familia zinazojimudu  ndio wanaosoma zaidi. Gazeti la "Hannoversche Allgemeine" linaandika: "Uchunguzi huu mpya unaonyesha asili mia 15 tu ya watoto ambao wazee wao hawakufanikiwa kufanya mtihani wa Abitur nchini Ujerumani au mtihani wa kidato cha sita, ndio wanaofanikiwa kumaliza masomo ya chuo kikuu-idadi hiyo ni ndogo mno ikilinganishwa na kiwango cha wastani kilichowekwa na shirika la OECD. Ukweli huo ni kinyume na ahadi iliyotolewa na mataifa wanachama kwamba mwenye kufanya bidii atatunzwa. Sio kila mmoja anafaidika na hilo linasikitisha."

 

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri: Iddi Ssessanga