1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kinyang'anyiro cha mrithi wa Strauss-Kahn chaiva

24 Mei 2011

Makubaliano ya siri kati ya Ulaya na Marekani kumchagua kiongozi mpya wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) huenda yakaathiri uhalali wa shirika hilo na ahadi ya G20 kuzipa usemi zaidi nchi zinazoinukia kiuchumi.

https://p.dw.com/p/11Mmf
Mkuu wa zamani wa IMF, Dominique Strauss-Kahn
Mkuu wa zamani wa IMF, Dominique Strauss-KahnPicha: AP

Nchi zinazoinukia kiuchumi duniani zimeghadhibishwa na uwezekano kuwa Ulaya na Marekani huenda zikajiamulia kati yao wenyewe nani atakaeliongoza shirika la IMF, huku Waziri wa Fedha wa Ufaransa, Christine Lagarde akiungwa mkono na nchi hizo.

Shirika la IMF linalosimamia utulivu wa fedha duniani na linaloongoza kuziokoa nchi za Ulaya zinazokabiliwa na matatizo ya fedha, linahitaji kiongozi mpya baada ya Dominique Strauss-Kahn kujiuzulu wiki iliyopita kufuatia mashtaka ya kumdhalilisha kingono mhudumu wa kike wa hoteli moja jijini New York. Strauss-Kahn amekanusha madai hayo.

Kwa zaidi ya miongo sita, makubaliano yasio rasmi kati ya Ulaya na Marekani, yanahakikisha kuwa mkuu wa IMF anatokea nchi ya Ulaya na raia wa Marekani anaiongoza Benki ya Dunia, taasisi kuu inayopiga vita umasikini kote duniani.

Waziri wa Fedha wa Ufaransa, Christine Lagarde, anayetajwa kumrithi Strauss-Kahn
Waziri wa Fedha wa Ufaransa, Christine Lagarde, anayetajwa kumrithi Strauss-KahnPicha: AP

Lagarde anaheshimiwa kote, lakini nchi zinazoendelea zingependa kuona wagombea kadhaa kutoka nchi tofauti, wakizingatiwa kuiongoza IMF, hata ikiwa mwishoni atakaechaguliwa atatokea Ulaya.

Afisa wa ngazi za juu kutoka nchi mojawapo inayoinukia kiuchumi duniani ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa wanajaribu kuwa na utaratibu utakaohakikisha kuwa hakutofanywa makubaliano ya siri.

Aprili mwaka 2009, viongozi wa nchi tajiri duniani G20 waliidhinisha utaratibu ulio wazi na unaozingatia ujuzi, wanapochagua viongozi wa taasisi za kimataifa. Lakini hawakuweza kuafikiana kuwasuala la uraia lisizingatiwe kabisa.

Wakati uchumi wa nchi tajiri ukikabiliwa na ukuaji mdogo na matatizo ya fedha, mataifa yanayoinukia kiuchumi kama vile India na China yanazidi kuwa muhimu kuongoza madai ya kimataifa. Vile vile yanataka kuwa na usemi zaidi katika Benki ya Dunia na IMF mjini Washington.

Kufuatia majadiliano magumu, China ilizishinda Ufaransa na Uingereza na sasa ni mwanachama wa tatu mwenye kura nyingi katika taasisi hizo mbili, baada ya Marekani na Japan. Hata kura za nchi zingine zinazoinukia kiuchumi zimeongezwa katika IMF na hivyo Brazil, India, Uturuki, Mexico na Korea ya Kusini zina usemi zaidi.

Hiyo humaanisha kuwa nchi hizo zitatoa mchango mkubwa zaidi katika IMF na mikopo ya dharura kwa nchi zinazohitaji msaada. Sasa mataifa hayo yanataka kupewa nafasi ya kugombea wadhifa wa mkuu wa IMF.

Tatizo la serikali ya Barack Obama ni kwamba, ikimuunga mkono mgombea wa nchi inayoinukia, basi Marekani itapaswa pia kukubali kumkabidhi mwengine wadhifa wa mkuu wa Benki ya Dunia.

Hilo huenda likawakera wabunge wa Marekani wanaodhibiti michango inayotolewa kwa taasisi hizo za kimataifa. Hata hivyo wengi wanaamini kuwa Marekani hatimae itamuunga mkono mgombea kutoka Ulaya.

Mwandishi: Prema Martin/Reuters
Mhariri: Sekione Kitojo