″Kama ndoto ya amani″ | Magazetini | DW | 09.05.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Magazetini

"Kama ndoto ya amani"

Masuala muhimu katika magazeti ya leo ya Ujerumani ni kuapishwa kwa serikali mpya Ireland Kaskazini ambalo lilikuwa tukio la kihistoria. Maadui wa zamani, Mprotestanti Ian Paisley, na Mkatoliki na mkuu wa chama cha Sinn Fein, Martin McGuiness wameungana katika serikali moja.

Ian Paisley na Martin McGuiness

Ian Paisley na Martin McGuiness

Kwanza ni maoni ya gazeti la “Die Welt”, ambalo limeshangazwa sana na tukio hili:

“Ni jambo ambalo haliaminiki kabisa kuweza kutokea, yaani kwamba vyama viwili ambavyo misimamo ni tofauti kama vile DUP cha Reverend Ian Paisley na chama cha Sinn Fein vinakubali kushirikiana katika serikali ya muungano. Ni kama moto na maji. Lakini tusisahau kuwa hatua hii ni mwanzo tu wa utaratibu mgumu wa maridhiano.”

Gazeti la “Rheinzeitung” lina matarajio mazuri kuhusiana na serikali hii ya muungano:

“Wanaoweza kumaliza ugomvi ni watu wenye nguvu tu. La sivyo, mkataba wa amani hautatekelezwa. Hivyo ndivyo hali ilivyo nchini Ireland Kaskazini. Mshupavu mprotestanti Ian Paisley na mwanaharakati wa zamani wa IRA mkatoliki Martin McGuiness wanaunda serikali inayounganisha madhehebu zote mbili. Hii ni kama ndoto ya amani huko Ireland Kaskazini. Pia utaratibu wa maridhiano una msingi imara, kwa vile Paisley, McGuiness na wenzao wana mamlaka ya kuwaunganisha pia wale wachache ambao bado wana msimamo mkali.”

Ni maneno yake mhariri wa “Rheinzeitung”. Gazeti kubwa la “Frankfurter Allgemeine Zeitung” linakumbusha muda wa miezi michache iliyopita ambapo serikali ya muungano ilionekana kuwa ni mbali sana.

“Wairishi wengi kutoka pande zote mbili za kisiasa, hawakuamini viongozi wao wangeshirikiana, na ikiwa ndiyo walidhani itakuwa ni janga tu. Huenda kwa wengi wa chama cha kupigania muungano na Uingereza bado ni jambo ambalo ni vigumu kukubali, yaani kwamba wanamgambo wa zamani wako katika serikali yao. Kwao ni kama kutojali wahanga wa ugaidi wa IRA. Lakini pia wale wanaojiita Republikans wanaotaka kujitenga na Uingereza nakujitegemea na ambao zamani walikabiliwa na ubaguzi wa kijamii na kisiasa, inawabidi kusahau kasoro zao.”

Tukielekea mjini Berlin, kule gazeti la “Tagesspiegel” linaangalia utaratibu mzima wa amani. Baada ya miaka 40 mzozo wa Ireland Kaskazini umemalizika na sasa mkoa huu wa Uingereza unaweza kujitawala. Gazeti limeandika:

“Utaratibu huu wa amani unatoa mfano mzuri. Licha ya kuchukua muda mrefu, ulifuata sheria fulani za kupatanisha, na katika kuangalia nyuma tunaweza kuona wapi matokeo fulani yalisababisha na hatua fulani. Tunachojifunza hapa ni kwamba: hakuna mzozo ambao hauwezi kutatuliwa.”

Na hatimaye ni gazeti la “Frankfurter Rundschau” ambalo linazingatia hasa jukumu la waziri mkuu wa Uingereza, Tony Blair, katika kupatanisha huko Ireland Kaskazini:

“Tony Blair alijitolea kwa namna isiyo na mfano mwingine, alifuatia lengo lake, alichunguza hali vizuri na aliufahamu vizuri kila pande husika. Amani ya Ireland Kaskazini ni mafanikio yake makubwa zaidi. Lakini tunajiuliza kipindi hiki cha mamlaka ya Tony Blair kingeweza kuleta faida gani nyingine ikiwa waziri huyu mkuu angeonyesha uwezo huu wakuleta amani katika nchi nyingine pia badala ya kuingia vitani. Huko Ireland Kaskazini, Tony Blair aliwapatia nafasi magaidi kupanda jukwaa na kisiasa. Nchini Iraq lakini hakutumia fursa ya kutatuliwa mzozo kwa subira.”

 • Tarehe 09.05.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHT0
 • Tarehe 09.05.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHT0
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com