KABUL: Watuhumiwa sita wakamatwa kwa mauaji ya mjerumani | Habari za Ulimwengu | DW | 09.03.2007
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Habari za Ulimwengu

KABUL: Watuhumiwa sita wakamatwa kwa mauaji ya mjerumani

Polisi nchini Afghanistan wamewakamata watu sita wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya mjerumani aliyekuwa akifanya kazi na shirika la kutoa misaada ya kiutu, German Agro Action, nchini Afghanistan.

Mjerumani huyo aliuwawa jana kwa kupigwa risasi katika wilaya ya Sayad katika mkoa wa Sar - e - Pul kaskazini mwa Afghanistan. Wavamizi waliwapora watu wengine watatu waliokuwa wakisafiri ndani ya magari mawili wakati waliposimamishwa.

Msemaji wa shirika hilo lenye makao yake hapa mjini Bonn, amethibitisha kuuwawa kwa mtoaji misaada huyo.

Mkurugenzi wa shirika linaloshughulikia usalama wa mashirika ya misaada nchini Afghanistan, Nic Lee, amesema eneo la kaskazini mwa Afghanistan ni hatari kwa watoa misaada ya kiutu.

´Mashirika ya misaada yanafanya kazi nyingi na yanakutana mara kwa mara na raia ambao hawafikiwi na watu wengine. Hilo linaweza kuwa hatari kwa watoaji misaada hasa kama kazi yao inatatiza shughuli zisizo halali. Kwa njia hiyo mizozo inaweza kuzuka baina yao na wafanyabiashara haramu au makundi ya magaidi. Inaweza kusababisha kifo na tayari watu wameuwawa.´

Gavana wa mkoa wa Sar - el - Pul, Sayed Mohammad Munib Eqbal, amethibitisha kukamatwa kwa washukiwa hao sita ambao sasa wanahojiwa na polisi.

Aidha kiongozi huyo amesema maafisa zaidi wa polisi wametumwa katika eneo hilo kuwasaka washukiwa zaidi ikiwa ni sehemu ya uchunguzi wa pamoja unaofanywa na jeshi la ISAF linaloongozwa na shirika la kujihami la kambi ya magharibi, NATO.

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com