1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kupambana na virusi vya Corona zapamba moto Ulaya

Sekione Kitojo
3 Aprili 2020

Hatua za ujenzi wa wodi za muda katika vyumba vya maktaba na kumbi za mikutano, zimechukuliwa wakati wafanyakazi wa sekta ya afya  wa mataifa ya Ulaya wakielemewa na jukumu la kuwaokoa maelfu ya wagonjwa wa virusi hivyo.

https://p.dw.com/p/3aPlW
Serbien Heroes at the time of isolation caused by Covid 19
Wodi za muda za kupambana na ugonjwa wa COVID-19Picha: DW/J. Djukic Pejic

Hatua za kupambana na  maambukizi ya virusi vya corona  zinaendelea  mnamo wakati  shehena za  madawa, vifaa vya  kujikinga na mashine za kusaidia  kupumua  vikiendelea  kuwa  haba kila  muda unavyokwenda. 

USA New York Coronavirus Bellevue Hospital provisorisches Leichenschauhaus
Vyumba vya muda vya kuwahifadhi wagonjwa wa maambukizi ya COVID-19Picha: Getty Images/E. Munoz

Wimbi la  vifo vinavyotokana  na  virusi vya corona pamoja  na kupotea  kwa nafasi za  ajira  limeikumba Marekani  na  Ulaya. Kiasi ya  wamarekani  milioni 10  wametupwa nje  ya  ajira  katika  kipindi cha  wiki  mbili zilizopita, ikiwa  ni  kuporomoka  kwa  kushangaza kabisa  nchini  Marekani kwa  soko  la  kazi  hali  ambayo  haijawahi kushuhudiwa. Duniani  kote watu waliothibitika  kuambukizwa  virusi vya  corona wamepindukia  milioni moja na  vifo vimefikia  watu 53,000, kwa  mujibu wa idadi iliyokusanywa  na  chuo kikuu  cha Johns Hopkins.

Mahospitali katika  jimbo  la  Catalonia nchini  Uhispania  likiwa jimbo  la  pili  nchini  humo  kuathirika  na maambukizi  ya  janga  la virusi  vya  corona, yako  katika  hali mbaya  ya  kuelemewa, kiongozi  wa  jimbo  hilo Quim Torra  ameliambia  shirika  la  habari la  Reuters leo.

Jimbo  hilo  la  pili  nchini  Uhispania  kwa  idadi  ya  wakaazi  ina idadi  kubwa ya  wagonjwa  wa  virusi  vya  corona  katika  kiwango cha  wagonjwa  mahututi  wanaofikia 2,053, kwa  mujibu wa  data  za hivi  karibuni, na  imewaorodhesha  watu 2,335 waliofariki, ikiwa  ni ya  pili  kwa  vifo  baada  ya  mji  mkuu  Madrid.

China Wuhan Krankenhaus Behandlung Coronavirus Patient
Mgonjwa mahututi wa virusi vya Corona akipatiwa matibabu Picha: picture-alliance/Xinhua/X. Yijiu

Hatua  zilizotumika  hapa  Ujerumani  kudhibiti  kusambaa kwa  virusi vya  corona zina matokeo  chanya kiasi, lakini  ni  mapema  mno kusema  kila  kitu  ni  shwari, shirika  la  serikali la  udhibiti wa magonjwa limesema  leo.

Boris Johnson kubakia nyumbani

Kwa siku chache zilizopita  hadi  sasa, mtu mmoja  aliyeambukizwa na  virusi  vya  corona nchini  Ujerumani, amekuwa  kwa  wastani akimuambukiza  mtu  mmoja mwingine , kwa  mujibu wa  taasisi  ya kupambana  na  magonjwa  ya  kuambukiza ya Robert  Koch. Wiki moja  iliyopita , idadi  hiyo  ilikuwa mtu mmoja  anawaambukiza watu watano, ama  hata  saba. Lakini  data  hizo  mpya  hazileti uhalali wa kuwa kila  kitu ni  shwari, amesema  Lotha Wieler rais wa  taasisi hiyo  ya  Robert Koch.

Waziri mkuu  wa  Uingereza  Boris Johnson amesema  leo  kuwa ataendelea  kujitenga baada  ya  kuthibitika  kuwa  na  virusi  vya COVID-19, kufuatia  wiki moja  ya  kubakia  nyumbani  na kufanyakazi  akiwa huko.

Wachuuzi  wa  kando kando ya  barabara wakivalia vifaa  vya kujifunika  pua  na  mdomo pamoja na  glovu mikononi walionekana wakiuza  bidhaa  mbali  mbali  pamoja  na  nyanya, karoti na  mboga nyingine  na  nyama  ya  nguruwe kwa wanunuzi leo  Ijumaa  katika mji  wa  Wuhan ambao  ndio  kitovu kilichoanzia ugonjwa  huu  wa virusi  vya  corona., wakati wafanyakazi wanajitayarisha  kwa  ajili ya  kumbukumbu  ya  kitaifa  mwishoni mwa juma kwa wafanyakazi wa  sekta  ya  afya na  wengine waliofariki kutokana  na  kuzuka kwa  virusi  hivyo.

China Wuhan | Coronavirus | Paar in Schutzanzug
Wakaazi wa mji wa Wuhan Picha: Getty Images/AFP/N. Celis

Nchi tatu za  Afrika  zimetoa  taarifa  ya  mapema  kuwa  janga  la corona  limeharibu  uwezekano wa  ukuaji wa  uchumi  wao  mwaka huu. Burkina Faso jana  ilipunguza  matarajio  yake  ya ukuaji  wa pato  jumla  la  taifa , GDP kwa  mwaka  2020  kutoka  asilimia 6.3 hadi  asilimia  2, katika  hotuba ya  taifa  aliyotoa  rais Roch Kabore.

Cote d'Ivore ilikuwa  nchi  ya kwanza  kufanya  hivyo  siku  ya Jumanne kwa  kusema  makadirio yake  yamepunguzwa  kwa  nusu kutoka  asilimia 3.6.