Je, Trump amepoteza silaha yake ya sera za kigeni?
23 Februari 2026
Baada ya Mahakama Kuu ya Marekani kuamua baadhi ya ushuru wa dharura wa Rais Donald Trump haukuwa halali,rais huyo alijibu kwa kutangaza ushuru mpya wa asilimia 10 na kuupandisha hadi 15,
Uamuzi wa Mahakama Kuu ulipokelewa kwa matumaini ya tahadhari na wafanyabiashara wengi waliotarajia utulivu katika sera ya biashara ya Marekani. Hata hivyo, matumaini hayo yalidumu kwa muda mfupi tu.
Rais Trump, ambaye kwa muda mrefu ameutumia ushuru kama silaha kuu ya sera yake ya kiuchumi na kidiplomasia, alisaini tangazo jipya la ushuru wa muda wa asilimia 10 kwa bidhaa zote zinazoingia nchini humo, kabla ya kuuongeza hadi asilimia 15 siku iliyofuata.
Kwa mujibu wa wachambuzi, hatua hiyo imeongeza wimbi jipya la sintofahamu katika uchumi wa dunia. Kwa kampuni ya uhandisi ya Ujerumani ya Ziehl-Abegg, soko la Marekani si la kawaida — ni soko lao kubwa zaidi, likichangia zaidi ya asilimia 20 ya mapato yao. Lakini mwaka wa ushuru wa Trump haukuwa mwepesi, na mwaka huu unaweza kuwa mgumu zaidi.
China, mnufaika mkuu wa uamuzi wa Mahakama, Marekani
Chama cha Sekta ya Uhandisi ya Mitambo cha Ujerumani, VDMA, kinaonya kuwa kampuni za Ulaya zinaweza kuwa miongoni mwa watakaoumia zaidi katika awamu hii mpya ya ushuru. Oliver Richtberg ni afisa kutoka chama VDMA.
Hadi sasa, China inaonekana kunufaika zaidi na uamuzi huu wa Mahakama Kuu kwa sababu awali ilikuwa na ushuru wa juu kuliko wetu, sasa itatozwa asilimia 15 tu, jambo linaloweza kuifanya iwe na ushindani mkubwa zaidi katika soko la Marekani — swali ni kama hili ndilo Rais Trump alilokusudia.
Rais Trump anatarajiwa kuzuru China mwishoni mwa Machi, lakini nguvu yake ya majadiliano sasa inaonekana kupungua, kwani ushuru mpya unaweza kudumu kwa siku 150 pekee bila idhini ya Bunge la Marekani.
Hata hivyo, wachambuzi wanasema Trump bado ana mbinu nyingine za kisheria za kuendeleza sera yake ya ushuru, jambo linaloongeza hali ya kutotabirika katika masoko ya kimataifa.
Mwelekeo mpya huenda ukaathiri uwekezaji na matumizi Ulaya
Carsten Brzeski ni mkuu wa utafiti na mchumi mkuu wa kanda ya euro kutokan benki ya ING
"Tunakabiliwa na wimbi jipya la mashaka linaloathiri uchumi wa Ulaya; kampuni zitasita kuwekeza na watumiaji watapunguza matumizi, hivyo faida kubwa ambayo Ulaya inahitaji sasa ni uhakika, uwazi na utulivu kuhusu sera za ushuru."
Kwa mujibu wa Brzeski, hali hii mpya ya sintofahamu inaweza kuathiri uwekezaji na matumizi barani Ulaya, huku kampuni zikisita kufanya maamuzi makubwa kutokana na kukosekana kwa uhakika.
Wachumi wengi sasa wanaushauri Umoja wa Ulaya kuharakisha mchakato wa kuidhinisha makubaliano ya biashara na Marekani yaliyofikiwa Julai mwaka jana, lakini ambayo yalisimama baada ya Trump kutoa matamshi ya kutaka kuiunganisha Greenland na Marekani.
Kwa biashara za Ulaya na dunia kwa ujumla, kilicho muhimu zaidi si tu kiwango cha ushuru, bali ni utabiri na utulivu wa sera. Katika dunia ya mabadiliko ya ghafla na ushuru wa kushtukiza, uhakika ndio bidhaa adimu zaidi.