1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Jacob Zuma apigania Kesi ya rushwa dhidi yake ifutwe

Saumu Mwasimba4 Agosti 2008

Wafuasi wake waandamana kumuunga mkono

https://p.dw.com/p/EqOt
Jacob Zuma adai kesi ni njama za kisiasa za kutaka kuizima ndoto yake''Picha: AP

Kiongozi wa chama tawala cha ANC nchini Afrika Kusini Jacob Zuma amekanusha tuhuma za rushwa zinazomkabili akisema kuwa ni njama za kisiasa zilizoundwa kumzuia kuwa rais wa nchi hiyo mwaka ujao.Maelfu ya wafuasi wake wameandamana nje ya mahakama kuu mjini Pietermaritzburg wakipinga hatua hiyo.

Jacob Zuma alifika mahakamani katika kesi ya rushwa dhidi yake iliyosubiriwa kwa muda mrefu huku wafuasi wake wakimkaribisha kwa heshima mkubwa wakiwa wabebeba mabango wameimba nyimbo za kupinga tuhuma za rushwa dhidi ya kiongozi huyo.

Zaidi ya wafuasi 1000 wameandamana nje ya mahakama kuu ya mjini Petermaritzburg wakilaani kwamba tuhuma za rushwa dhidi ya Zuma ni njama za kisiasa zilizopangwa kimakusudi kumzuia asiweze kuwa rais wa nchi hiyo mwaka ujao.

Wafuasi hao wameapa kulemaza shughuli zote za mji huo ambako ndiko alikozaliwa Jacob Zuma.

Akiwasili mahakamani mapema hii leo Zuma alionekana mtulivu huku akitabasamu wakati akiwapungia mkono maafisa wa chama cha ANC na wafuasi wa chama hicho.Wakili wake Kemp J Kemp amedai kwamba kesi hiyo ifutwe kwasababu waendesha mashataka hawakufuata utaratibu wa kikatiba walipoamua kumfungulia tena mashataka bwana Zuma.

Wakili huyo ameongeza kusema mbele ya mahakama kwamba hakuna haki yoyote iliyotetendeka na hivyo Zuma hapasi kufunguliwa tena mashtaka.

Hii ni mara ya pili dola inajaribu kumshtaki kiongozi huyo kwa madai ya ulaji rushwa baada ya mwaka 2006 jaji kutupilia mbali juhudi za dakika za mwisho za mwendesha mashtaka na kuitaja kesi hiyo kuwa ni janga.

Zuma alishatakiwa upya siku kadhaa baada ya kumuangusha rais Thabo Mbeki na kuchukua uongozi wa chama hicho mwezi Desemba jambo ambalo wafuasi wake wanalitaja kama ni tukio lililochangiwa kisiasa.

Wafuasi wa Zuma wanasema njama za kisiasa zimepangwa na wakereketwa na watiifu wa rais Thabo Mbeki kwa lengo la kuyazima matumaini ya kisiasa ya bwana Zuma.

Chama cha ANC kimetoa taarifa na kusema kwamba katika kipindi kizima cha uchnguzi na uendeshaji mashataka wa kesi hii kiongozi huyo wa ANC haki yake imekuwa ikikiukwa mara zote na vyombo vya dola.

Wafuasi wa Zuma wamesema kwa upande mwingine kwamba hata akifungwa jela watampigia kura wakati wa uchaguzi mkuu.

Maafisa wa ngazi za juu katika chama cha ANC walifika kumuunga mkono Zuma ambaye wanataka awe mgombea wao katika uchaguzi wa rais mwaka ujao.

Zuma anakabiliwa na mashtaka 16 ya rushwa ikiwemo kupokea hongo ya zaidi ya randi millioni 4 katika kipindi cha 10 malipo hayo yanahusishwa zaidi na mshauri wake wa zamani Schabir Sheikh ambaye anatumikia kifungo cha miaka 15 jela.