1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Israel na Lebanon zarefusha usitishaji mapigano

24 Aprili 2026

Rais Donald Trump amesema kwamba Israel na Lebanon zimeongeza muda wa kusitisha mapigano kwa wiki tatu, huku mazungumzo ya Marekani na Iran ya kukomesha vita vya Mashariki ya Kati yakiwa katika mkwamo.

https://p.dw.com/p/5Ck5r
Rais wa Marekani Donald Trump azungumza katika Ikulu ya White House, huku makamu wa Rais JD Vance na Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio wakiwa wamesimama nyuma yake
Trump alisema Vance na Rubio pia walihudhuria mikutano na maafisa 'wa ngazi za juu' kutoka Israel na LebanonPicha: Mark Schiefelbein/AP Photo/picture alliance

Trump alitangaza kurefushwa kwa mpango huo wa kusitisha mapigano alipokutana na mabalozi wa nchi hizo mbili na licha ya mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel nchini Lebanon na mashambulizi mapya ya makombora kutoka kwa wanamgambo wa Hezbollah wanaoungwa mkono na Iran, ambao hawakuwa sehemu ya mazungumzo huko Washington.

Trump alisema duru ya pili ya mazungumzo hayo "ilikwenda vizuri” na kwamba "Marekani itashirikiana na Lebanon ili kuisaidia kujilinda dhidi ya Hezbollah."

Kusisitiza udhaifu wa makubaliano hayo ya kusitisha mapigano, jeshi la Israel lilisema liliishambulia mitambo ya kurusha makombora nchini Lebanon ambayo ilikuwa imefyatua makombora kwenye mipaka yake. Hezbollah ilisema ilirusha makombora kwenye mji wa Shtula wa Israel ili kujibu mashambulizi ya Israel kwenye kijiji cha Yater cha Lebanon.

Wizara ya afya ya umma ya Lebanon ilisema shambulio la anga la Israel liliwaua watu watatu kaskazini mwa nchi, katika eneo la Nabatiya. Jeshi la Israel lilisema liliwaua wanamgambo watatu waliorusha kombora kuelekea ndege ya kivita ya Israel. Kila upande unaushutumu mwingine kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.

Moshi waonekana kwenye kijiji cha kusini mwa Lebanon huku jeshi la Israel likiendesha operesheni zake huko
Licha ya usitishwaji mapigano, Hezbollah na Israel zimeendelea kushambuliana kwa makomboraPicha: Gil Eliyahu/REUTERS

Mazungumzo ya Marekani na Iran kwenye mkwamo

Rais huyo wa Marekani alisema awali kuwa hana haraka ya kukomesha vita na Iran, akiongeza kwamba "muda unayoyoma" kwa jamhuri hiyo ya Kiislamu kwani meli ya tatu ya Marekani ya kubeba ndege za kivita iliwasili Mashariki ya Kati.

Bado haijawa wazi ni lini, au kama, Marekani na Iran zitakutana tena katika mji mkuu wa Pakistan, Islamabad, ambako wapatanishi wanajaribu kuzileta pamoja nchi hizo ili kufikia makubaliano ya kidiplomasia ya kukomesha mzozo huo.

Mazungumzo yaliyopangwa mapema wiki hii hayajafanyika. Iran inasisitiza kuwa haitahudhuria hadi Marekani itakapoondoa mzingiro wake wa kijeshi kwenye bandari na meli za Iran. Ikulu ya White House inasisitiza kuwa haitashiriki hadi Tehran itakapofungua mlangobahari kwa meli za kimataifa.

Papa Leo XIV, wakati akiwa safarini kurudi nyumbani kutoka ziara ya Afrika, alizihimiza Marekani na Iran kurudi kwenye mazungumzo ili kukomesha vita.

Amri ya kuziangamiza boti

Trump, ambaye siku ya Alhamisi alifuta uwezekano wa matumizi ya silaha ya nyuklia dhidi ya Iran, hapo awali alikuwa ameamuru Jeshi la Wanamaji la Marekani kuharibu boti yoyote ya Iran itakayokamatwa ikitega mabomu huko Hormuz.

Manowari tatu za kubeba ndege za kivita ziko katika eneo hilo baada ya meli ya USS George H.W.Bush kuwasili katika Bahari ya Hindi. Manowari moja iko katika Bahari ya Uarabuni na nyingine iko katika Bahari ya Shamu. 

Boti ya jeshi la walinzi wa mapinduzi la Iran likifanya operesheni ya kuzikamata meli zinazopita katika Mlango-Bahari wa Hormuz
Trump ameamuru Jeshi la Wanamaji la Marekani kuharibu boti za Iran zitakazokamatwa zikitega mabomu huko Hormuz.Picha: IRIB TV/AFP

Rais Donald Trump ameliamuru jeshi la Marekani "kuzifyatulia risasi na kuziangamiza" boti ndogo za Iran zinazotega mabomu katika Mlango-Bahari wa Hormuz. Ametangaza hatua hiyo Alhamisi siku moja baada ya Iran kuonyesha tena uwezo wake wa kuzuia safari za meli kwenye mlango huo wa kimkakati.

Ujumbe wake kwenye mitandao ya kijamii kuhusu boti hizo ndogo lilijiri muda mfupi baada ya jeshi la Marekani kukamata meli nyingine ya mafuta inayohusishwa na usafirishaji haramu wa mafuta ya Iran.

Trump adai kuna mzozo wa uongozi nchini Iran

Trump amedai kuwa mgawanyiko wa uongozi kati ya watu wenye msimamo wa wastani na wenye msimamo mkali unaichanganya Iran. Trump, aliyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House. Hatujui nani ndio kiongozi nchini Iran. Kwa sababu kuna mabadiliko ya utawala. Khomeini hayupo. Aliuawa. Aliuawa na timu yake yote pia ikauawa, kisha kundi la pili likaingia, wote wameuawa, na sasa kuna kundi la tatu. Na wana wasiwasi kidogo kwamba nao pia wanaweza wakauawa.

Rais wa Iran na spika wa bunge walichapisha taarifa kwenye mitandao ya kijamii wakitangaza kwamba nchi hiyo haina watu wenye msimamo mkali au wenye msimamo wa wastani. "Sisi sote ni Wairani na wanamapinduzi," walisema.

Vyanzo: Mashirika