1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mabomu Hormuz: Ni tishio kiasi gani kwa usafiri baharini?

22 Aprili 2026

Hofu ya mabomu ya majini katika Mlango wa Hormuz yanaibua wasiwasi wa usalama wa meli, huku mataifa yakijadili hatua za kusafisha njia hiyo muhimu ya kimataifa inayopitisha asilimia 20 ya biashara ya mafuta na gesi.

https://p.dw.com/p/5Cf2Z
Bulgaria | Uteketezaji wa bomu la baharini katika Bahari Nyeusi
Mabomu ya chini ya maji yanaweza kuwa tishio katika maeneo yaliyoathirika kwa miongo kadhaa ijayo [Faili: Bahari Nyeusi, Bulgaria, Julai 1, 2022]Picha: BULGARIAN MINISTRY OF DEFENCE Via REUTERS

Mvutano umeongezeka katika Mlango wa Hormuz baada ya Iran kudai kuwa imeweka mabomu ya majini ili kuzuia usafiri huru wa meli katika njia hiyo muhimu ya kimataifa.

Mlango wa Hormuz ni njia nyeti ya usafirishaji wa mafuta duniani, hivyo tishio lolote linaweza kuwa na athari kubwa kwa uchumi wa kimataifa na usalama wa nishati.

Siku ya Ijumaa, Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz alisema nchi yake iko tayari kusaidia katika operesheni za kusafisha mabomu ya majini pamoja na ufuatiliaji wa bahari ili kulinda njia hiyo.

Alisema Ujerumani inaweza kutoa meli maalum za kusafisha mabomu, lakini akasisitiza kuwa hatua hiyo itahitaji msingi imara wa kisheria kabla ya kutekelezwa.

Kauli hiyo ilifuatia mashauriano kati ya viongozi wa Ulaya kuhusu uwezekano wa kuanzisha operesheni ya pamoja ya kimataifa kulinda mlango huo baada ya vita vinavyoendelea katika eneo hilo.

Iran inavyoweza kujilinda dhidi ya mashambulizi ya Marekani

Kauli kinzani na hali ya sintofahamu

Wakati huo huo, waziri wa mambo ya nje wa Iran Abbas Araghchi alisema njia hiyo iko wazi kwa usafiri wakati wa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Lebanon.

Kwa upande wake, Rais wa Marekani Donald Trump alieleza kuwa mlango huo uko tayari kwa matumizi kamili ya meli.

Hata hivyo, siku iliyofuata Iran ilibadilisha msimamo wake na kutangaza tena kufunga njia hiyo, hali iliyoongeza mkanganyiko na wasiwasi wa kimataifa.

Licha ya kauli hizo, wataalamu wanaonya kuwa hata uwezekano wa kuwepo kwa mabomu ya majini unatosha kuzuia meli nyingi kutumia njia hiyo.

Hatari halisi ya mabomu ya majini

Kwa mujibu wa mtaalamu wa vita vya chini ya maji Johannes Peters wa Taasisi ya Sera za Usalama ya Chuo Kikuu cha Kiel, bado haijathibitishwa kama mabomu hayo yapo.

"Hatujui kwa uhakika kama mabomu yapo, lakini tishio lenyewe linatosha kuwazuia watu kupita,” anasema Peters.

Anaongeza kuwa hali ya vita katika eneo hilo inafanya kuwa vigumu kwa wataalamu kwenda kuchunguza moja kwa moja chini ya maji.

Iran yaonesha uwezo wake wa makombora Tehran

Mabomu ya majini hufanyaje kazi?

Mabomu ya majini ni vifaa vya kulipuka vilivyowekwa chini ya maji na vinavyolenga kulipuka pale vinapochochewa na meli au manowari zinazopita karibu. Kwa kawaida, ni gharama nafuu lakini vina uwezo mkubwa wa kusababisha uharibifu.

Kuna aina kuu tatu za mabomu haya kulingana na mahali yanapowekwa: yale yanayoelea juu ya maji (drifting), yale yanayoning'inia chini ya maji yakiwa yamefungwa ardhini (moored), na yale yanayolala moja kwa moja chini ya bahari (bottom mines).

Tofauti na mabomu ya zamani yaliyotumika wakati wa Vita Kuu ya II ya Dunia, ambayo yalihitaji kugusana moja kwa moja na meli ili kulipuka, mabomu ya kisasa yana teknolojia ya hali ya juu zaidi.

Kwa mujibu wa mtaalamu Johannes Peters, mabomu ya sasa yanaweza kulipuka bila kugusana na meli, yakitumia vihisi vya sumaku, mawimbi ya sauti au mabadiliko ya shinikizo la maji yanayosababishwa na meli.

Aidha, mabomu hayo yanaweza "kupangwa” kulenga aina maalum ya meli kwa kutumia alama za sauti (acoustic signatures), hali inayoruhusu meli rafiki kupita bila hatari huku zile za adui zikilengwa.

Karte Straße von Hormus (700x394) Englisch

Kusafisha mabomu ni kazi ngumu na ya muda mrefu

Mchakato wa kuondoa mabomu ya majini unajumuisha kuyatafuta na kuyasafisha, jambo linaloweza kuchukua muda mrefu na rasilimali nyingi.

Hatua ya kwanza ni kugundua vitu vinavyotia shaka chini ya maji, kisha wataalamu huamua kama ni bomu au la. Ikiwa ni hatari, linaweza kuondolewa, kuteguliwa au kulipuliwa kwa njia salama.

Hata hivyo, teknolojia mpya imeanza kubadilisha mbinu hizi. Kwa mfano, wanajeshi wa Ukraine wanatumia droni za chini ya maji kutambua na kuharibu mabomu bila kuhatarisha maisha ya binadamu.

Njia hii imefananishwa na huduma ya "kusafisha mabomu chini ya maji,” ambapo mashine hufanya kazi hatari badala ya wanadamu.

Droni zabadilisha operesheni za kijeshi baharini

Jeshi la wanamaji la Ujerumani pia limeanza kutumia mifumo ya kisasa ya droni katika kutafuta mabomu ya majini.

Kwa mujibu wa afisa Andreas, mifumo ya kujitegemea (autonomous systems) sasa inatumika kuchunguza chini ya bahari badala ya meli kupita moja kwa moja juu ya maeneo hatarishi kama ilivyokuwa zamani.

Mbinu hii imepunguza hatari kwa wanajeshi na pia imeongeza ufanisi, kwani droni hutuma picha na taarifa moja kwa moja kwa wachambuzi walioko mbali.

Hata hivyo, bado binadamu wanahitajika kutafsiri taarifa hizo na kufanya maamuzi kuhusu jinsi ya kushughulikia mabomu yaliyogunduliwa.

Bahari ya Baltiki | Meli ya kutafuta mabomu ya majini “Dillingen” ya Jeshi la Wanamaji la Germany
Meli za kutafuta mabomu ya majini kama hii hapo awali zililazimika kupita moja kwa moja juu ya eneo lenye mabomu ili kuyagundua yaliyo chini ya majiPicha: FILIP SINGER/EPA-EFE

Licha ya maendeleo haya, wataalamu wanaonya kuwa inaweza kuchukua miongo kadhaa kusafisha kabisa mabomu katika eneo lililoathiriwa na vita.

Changamoto za kutumia droni Hormuz

Kutumia droni katika eneo nyeti kama Mlango wa Hormuz kuna changamoto zake. Moja ya changamoto kubwa ni uwezo mdogo wa betri, unaozuia muda ambao droni zinaweza kufanya kazi baharini.

Afisa Andreas anaeleza kuwa droni nyingi zinahitaji kuendeshwa karibu na eneo la uchunguzi, jambo ambalo ni hatari katika eneo lenye mvutano mkubwa kama Hormuz.

Kutokana na uwepo wa silaha za masafa marefu kutoka Iran, inalazimu operesheni kufanyika kwa tahadhari kubwa ili kulinda maisha ya wahusika.

Droni ya chini ya maji “Greyshark” ya kampuni ya Euroatlas kutoka Germany
Droni ya chini ya maji “Greyshark” ya kampuni ya Euroatlas kutoka GermanyPicha: Euroatlas

Teknolojia mpya na matumaini ya usalama

Makampuni ya teknolojia yanaendelea kubuni droni zenye uwezo mkubwa zaidi. Kampuni ya Euroatlas imetengeneza droni ya chini ya maji iitwayo Greyshark, yenye uwezo wa kufanya kazi kwa muda mrefu zaidi na kusafiri umbali mkubwa.

Kwa mujibu wa Markus Beer, droni hizi zinaweza kusaidia kufanya upelelezi wa chini ya maji bila kuweka maisha ya wanadamu hatarini na bila kuongeza mvutano wa kijeshi.

Greyshark inaweza kupiga picha zenye ubora wa juu na kutambua vitu vilivyo chini ya bahari kwa uhuru, jambo linaloweza kuboresha kwa kiasi kikubwa operesheni za kusafisha mabomu.

Kwa ujumla, licha ya hatari zinazoletwa na mabomu ya majini, maendeleo ya teknolojia yanaweza kuwa suluhisho muhimu katika kuhakikisha usalama wa njia muhimu za baharini kama Mlango wa Hormuz.