Mali: Hatuna mpango wa kuzungumza na 'magaidi'
8 Mei 2026
Waziri wa Mambo ya Nje wa Mali Abdoulaye Diop amesema akizungumza na wanadiplomasia, kwamba serikali mjini Bamako haina mpango wowote wa kufanya mazungumzo na makundi ya kigaidi yanayoendesha shughuli zao kinyume cha sheria na ambayo yamehusika na matukio mabaya yaliyowakumba watu wa eneo hilo kwa miaka mingi.
Kauli ya waziri Diop imetolewa siku chache baada ya wapiganaji itikadi kali wa kundi la Ukombozi wa Azawad linalowajumuisha waasi wanaotaka kujitenga wa Touareg na washirika wao wa kundi la JNIM kuanzisha mashambulizi makubwa dhidi ya taasisi za uongozi wa kijeshi unaoiongoza Mali tangu mwaka 2020.
Watu zaidi wauawa kwenye mashambulizi
Alhamisi, vyanzo mbalimbali vililiambia shirika la habari la AFP kuwa mashambulizi mawili katikati mwa Mali yaliyofanywa na makundi hayo ya itikadi kali yenye mafungano na Al Qaeda yalisababisha vifo vya watu zaidi ya 30 katika vijiji vya Korikori na Gomossogou.
Kundi la waandishi wa habari waliobobea katika masuala ya usalama wa kanda ya Sahel wamesema idadi hiyo ya vifo inakadiriwakufikia watu 50 huku wengine wengi wakiwa hadi sasa hawajulikani walipo.
Kumeripotiwa pia msako unaoendelea dhidi ya wanasiasa wa upinzani na maafisa kadhaa wa kijeshi ambao wanaendelea pia kukamatwa na kushikiliwa na mamlaka za kijeshi. Waasi hao wamepata mafanikio kwa kuudhibiti mji wa Kidal na kambi muhimu ya kijeshi ya Tessalit huku wakizuia barabara nyingi zinazoelekea katika mji Mkuu Bamako.
Jeshi: Hali ya usalama bado ni tete
Msemaji wa Jeshi la Mali Meja Djibril Maiga amesema zaidi ya maafisa 10,000 wa ndani na kutoka nje ya nchi wanashiriki zoezi la kuwadhibiti waasi hao lakini akasisitiza kuwa kuwa hali ya usalama bado ni tete. "Adui aliyekosa mwelekeo hakuwa na chaguo jingine, isipokuwa kuzuia barabara zinazoelekea mjini Bamako kwa kutumia mbinu tata."
Mamluki wa Urusi wa Africa Corps ambao zamani walijulikana kama Wagner wamesema wanaendelea kuisaidia serikali ya Mali kukabiliana na makundi hayo ambayo tayari yametangaza azma yao ya kuuangusha utawala wa kijeshi unaoongozwa na Jenerali Assimi Goita.