Iran yasema usitishaji mapigano waanza kuvunjwa
8 Aprili 2026
Waziri Mkuu wa Pakistan, Shehbaz Sharif, alisema siku ya Jumatano (Aprili 4) kwamba uvunjwaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran "umeripotiwa" na kuzitaka pande zote kuheshimu makubaliano hayo.
"Uvunjwaji makubaliano umeripotiwa kwenye maneo machache kwenye eneo la mgogoro ambao unahujumu dhamira ya mchakato wa amani," aliandika Sharif kwenye mtandao wa X.
"Kwa heshima na taadhima nazitaka pande zote kujizuwia kuchukuwa hatua za kuyaharibu makubaliano haya na ziyaheshimu kwa wiki hizi mbili kama ilivyokubalika, ili diplomasia ituongeze kuelekea amani ya kudumu," aliongeza.
Kauli ya mpatanishi huyo mkuu wa mgogoro huo ilikuja muda mchache baada ya Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Iran, Abbas Araghchi, kuzungumza na mkuu wa majeshi wa Pakistan na kumjulisha juu ya kile alichosema ni "uvunjwaji wa makubaliano ya usitishaji mapigano unaofanywa na Israel nchini Lebanon."
Kwa mujibu wa masharti iliyoyaweka Iran kwenye mpango wake wa vipengele kumi wa kusitisha mapigano, usitishaji huo unapaswa kujumuisha pia Lebanon, Iraq na Yemen.
Jeshi la Israel lilifanya mashambulizi saba mfululizo kwenye maeneo kadhaa ndani ya Lebanon siku ya Jumatano, likidai kuwalenga wapiganaji wa kundi la Hizbullah.
Shirika la habari la Tasnim lilikinukuu chanzo kimoja serikalini kikisema kuwa Iran "itajitowa kwenye makubaliano hayo ya kusitisha mapigano endapo mashambulizi dhidi ya Lebanon yataendelea."
Iran yadunguwa, yarusha droni Ghuba
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi la Iran (IRGC) lilisema lilikuwa limeidunguwa droni moja kusini mwa nchi hiyo mchana wa Jumatano, masaa kadhaa baada ya kutangazwa kwa makubaliano hayo ya kusitisha mapigano.
"Dakika chache zilizopita, mfumo wa ulinzi wa anga umeidunguwa droni ya kiwango cha juu chapa Hermes 900 kwenye anga la Lar, jimbo la Fars. Uingiaji wa ndege yoyote ya adui wa Kimarekani ama Kizayuni au ndege zao kwenye anga letu, hata kama si kwa ajili ya kufanya mashambulizi, unachukuliwa kuwa uvunjaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano na utachukuliwa hatua kali na za haraka." Lilisema shirika la utangazaji la Iran (IRIB) likilinukuu jeshi hilo.
Kwa upande wake, Iran imefanya mashambulizi kuelekea Umoja wa Falme za Kiarabu, Qatar, Saudi Arabia na Kuwait, likisema linajibu mashambulizi yaliyofanywa kutokea ardhi za mataifa hayo ya Ghuba.
Saudi Arabia ilisema ilizidunguwa droni tisa juu ya anga lake mchana wa Jumatano, ingawa haikusema wapi droni hizo zilikotokea.
Iran kuendelea kusimamia Hormuz
Katika hatua nyengine, Araghchi alisema Iran ingeliendelea kuwa na udhibiti wa Mlango Bahari wa Hormuz, licha ya Rais Donald Trump wa Marekani kudai kuwa Iran ingeliufunguwa Mlango Bahari huo.
Akiandika kupitia mtandao wa X, Araghchi amliema usafirishaji wa meli za mizigo "unaweza kuendelea kwa uratibu wa vikosi vya jeshi la Iran na kwa kuzingatia pia hali ya kiusalama na kiufundi."
Kuufunguwa tena Mlango Bahari huo ni sehemu ya matakwa ya Marekani kwenye makubaliano ya kusitisha mapigano.
Kwa upande wake, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, amesema Iran itapaswa kukabidhisha akiba yake ya madini ya urani yaliyorutubishwa vyenginevyo Marekani itayachukuwa, ingawa hakuweka bayana itayachukuwaje.
"Tunawaangalia. Tunajuwa walichonacho na watakitowa na tutakipata, na tutakichukuwa. Ikibidi, tutafanya tena, kwa njia yoyote ile." Alisema Hegseth.