1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran na Venezuela zailaani Marekani

Saumu Mwasimba2 Julai 2007

Marafiki wawili wakosoaji wakubwa wa Marekani rais Mahmoud Ahmed Nejad na mwenzake Hugo Chavez wa Venezuela leo wamezindua ujenzi wa mtambo wa mafuta katika pwani ya Iran.

https://p.dw.com/p/CHBl
Vigogo wawili wapinzani wa Marekani marais Hugo Chavez na Mahmoud AhmedNejad
Vigogo wawili wapinzani wa Marekani marais Hugo Chavez na Mahmoud AhmedNejadPicha: AP

Hatua hii imechukuliwa na viongozi hao kuuimarisha uhusiano wa mataifa yote mawili.

Wakizindua rasmi ujenzi wa mtambo huo wa mafuta katika kiwanda cha Asaluyeh viongozi hao wawili waliahidi kusimama kidete dhidi ya maadui wote wakiilenga hasa Marekani.

Rais Chavez wa Venezuelea katika ziara yake hii ya kwanza nchini Iran ameahidi kuziunganisha ghuba ya uajemi na eneo la Carribean akisema Iran na Venezuela zitajenga dunia iliyobora kabisa.

Aliongeza kusema kwamba anamshukuru mwenyezi mungu kuona Iran na Venezuela zinasimama pamoja daima.

Hapo jana viongozi wa nchi hizo mbili ambazo ni wanachama wakubwa katika nchi zinazotoa mafuta kwa wingi duniani OPEC walitoa ahadi za kuimarisha ushirikiano na biashara katika kikao cha siku nzima ambacho kilitabiri kuanguka kwa Marekani.

Rais AhmedNejad wa Iran alisema hatua kubwa imechukuliwa kuimarisha ushirikiano wakidugu kati ya Iran na Venezula zikiwa na lengo la kuendeleza nchi zao na kusimama wima dhidi ya maadui wote duniani.

Rais wa Iran pia aliiusifu sana ushirikiano wake na Chavez na kuongeza kusema Viva Iran na Venezuela yaani zidumu Iran na Venezula na mataifa yote ya kimapinduzi na kifo kwa maadui.

Chavez amekuwepo Iran kwa siku mbili baada ya kuzitembelea nchi zinazogongana na Marekani kama vile Urussi na Belarus.

Akiwa Urussi alitoa matamshi makali dhidi ya Marekani akisema….

’’Nchi yetu ni ya amani tunatilia mkazo juu ya amani na pia tunatekeleza amani nje na ndani katika amerika ya kusini na eneo la Karibean na ulimwenguni kote.Sisi sio nchi inayoendesha vita wanaopenda vita ni wengine na wanajaribu kuutawala ulimwengu lakini hawatafaulu.’’

Chavez pia alikuwa mgeni wa aina yake kwa kiongozi wa juu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei hasa ikizingatiwa Chavez sio muislamu.

Khamenei alimwambia rais Chavez kwamba Marekani haiwezi kuharibu uhusiano wa Iran na Venezuela kwasababu uhusiano huo ni wa asili na ni lazima uimarishwe.

Kwa mujibu wa afisa mmoja anayehusika na masuala ya mafuta, mtambo wa mafuta unaotazamiwa kumalizika katika muda wa miaka minne utakuwa na uwezo wa kutoa tanni millioni 1.65 kwa mwaka na mradi kama huo pia unapangiwa kuanzishwa nchini Venezuela.

Kinu cha Venezuela kitaiwezesha Iran kuyafikia kwa ubora zaidi masoko ya Amerika ya kusini na Brazil.

Chavez ni kiongozi aliyeko mstari wa mbele katika Amerika ya kusini anayeiunga mkono Iran na mpango wake wa Kinuklia unaotiliwa mashaka na nchi za magharibi kwamba unanuiwa kutengenezea silaha za maangamizi makubwa licha ya Iran kupinga madai hayo.