Ilani ya uchaguzi ya CDU/CSU yahanikiza Magazetini | Magazetini | DW | 04.07.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Magazetini

Ilani ya uchaguzi ya CDU/CSU yahanikiza Magazetini

Ilani ya uchaguzi ya vyama vya CDU na CSU ndio iliyohanikiza magazetini . Hata hivyo wahariri wamemulika pia hotuba ya rais wa Ufaransa Emmanuel Macron mbele ya wawakilishi katika kasri la Versailles

 .

Tunaanzia lakini Ujerumani ambako miezi chini ya mitatu kabla ya uchaguzi mkuu, vyama ndugu vya CDU/CSU vimetangaza hatimae ilani yao ya uchaguzi. Wahariri wanakubaliana viongozi wa vyama hivyo vya kihafidhina, kansela Angela Merkel na waziri mkuu wa jimbo la Bavaria Horst Seehofer walitaka kuonyesha mshikamano uliopo licha ya malumbano ya miezi kadhaa. Gazeti la Hannoversche Allgemeine linaandika: "Lengo linalowaunganisha wana CDU na CSU ni moja tu, nalo ni kuibuka na ushindi uchaguzi mkuu utakapoitishwa, septemba 24 inayokuja. Mengine ni makadirio tu. Katika miezi ya malumbano kati ya CDU na CSU, na kansela kufika hadi ya kuitwa "kansela wa wakimbizi", wana CDU/CSU walitambua ugonvi huo unaweza kuwapeleka wapi. Hivi sasa, nafasi ya malumbano inashikiliwa na  "hali yakuaminiana kwa dhati:" Na hali hiyo wana CDU/CSU wanaitarajia pia kutoka kwa wapiga kura. Ikiwa wapinzani watawaachia, basi hali hiyo inaweza kuwapatia ushindi wakati wa uchaguzi."

Ilani ya uchaguzi ya vyama ndugu vya CDU/CSU imepewa jina "Kwaajili ya Ujerumani, nchi tunakopenda kuishi na kwa nafasi". Katika ilani hiyo Merkel na Seehofer wameahidi ajira kwa kila mjerumani hadi ifikapo mwaka 2025. Mhariri wa gazeti la mjini Koblenz,"Rhein-Zeitung" anahisi ahadi hiyo ni sawa na ndoto". Gazeti linaendelea kuandika: "Kumpatia ajira kila mjerumani hadi ifikapo mwaka 2025 ni miongoni mwa miradi ambayo inategemea hali namna ilivyo katika soko la ajira na huko serikali haina ushawishi mkubwa. Pindi  uchumi wa dunia ukiporomoka, lengo hilo kuu halitoweza kufikiwa. Ndio maana kwa kuchagua mwaka 2025, imechaguliwa tarehe ya mwisho wa mhula ili kutathmini hali ya mambo. Kwa jumla ilani hiyo ya uchaguzi inakidhi matarajio ya wapiga kura. Katika nyakati za patashika, hakuna anaetaka majariibio. Zimwi likujualo halikuli likakwisha wanasema wahenga."

Macron awahutubia wawakilishi wa umma katika kasri la Versailles

Mada yetu ya pili na ya mwisho magazetini inatupeleka Ufaransa ambako rais mpya Emmanuel Macron amewahutubia wawakilishi wa mabaraza yote mawili ya bunge; baraza la taifa na baraza la Seneti katika ukumbi wa kasri la fahari la Versailles. Wawakilishi wasiopungua 30 wamesusia kikao hicho kilichoitishwa siku moja kabla ya hotuba ya waziri mkuu Edouard Philippe kuhusu mwongozo wa serikali yake. Gazeti la "Badisches Tagblatt linachambua hotuba ya rais Macron na kuandika: "Emmanuel Macron hajafafanua kikamilifu njia gani Ufaransa inabidi iifuate. Lakini ameshaanza na jana amedhihirisha hatishiki: Anataka kuwepo uwiano kidogo  na katika mfumo wa kupiga kura nchini Ufaransa, anataka aina fulani ya mageuzi endelevu yatakayorahisisha mageuzi ya kina. Emmanuel Macron ameainisha alichokisema anakidhamiria aliposhadidia ikilazimika ataitisha kura ya maoni ya wananchi ili kuufanyia marekebisho mfumo wa kupiga kura. Ni sawa na kitisho kwa wale watakaotaka kumbisha.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse

Mhariri:Yusuf Saumu

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com