Ijumaa kuu yasherehekewa mjini Jerusalem | Masuala ya Jamii | DW | 06.04.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Masuala ya Jamii

Ijumaa kuu yasherehekewa mjini Jerusalem

kiwa ni Ijumaa kuu maelfu ya Wakristo wamekwenda hija mjini Jerusalem, Israel, Huko wanafuata njia aliyopitia Yesu Kristu katika mji mkongwe ambapo alibeba msalaba kabla ya kusulubiwa. Waliokuja Jerusalem ni waumini wa makanisa mbali mbali na kutoka nchi mbali mbali.

Wakristo wa kanisa la orthodox la Ethiopia mjini Jerusalem

Wakristo wa kanisa la orthodox la Ethiopia mjini Jerusalem

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Israel, idadi ya watalii waliofika Jerusalem imeongezeka ikilinganishwa na miaka iliyopita kwa sababu ya hali ya utulivu zaidi katika eneo la Mashariki ya Kati mwaka huu. Waumini wanatoka hasa Marekani, India, Korea Kusini, Philippines na Urusi wakiwa ni wa madhehebu mbali mbali ya kikristo. Mwaka huu makanisa yote ya kikristo yanasherehekea Pasaka wakati sawa, kawaida lakini kuna tofauti ya wiki kadhaa kati ya sherehe za Ukristo wa Magharibi na makanisa ya orthodox ya Mashariki. Wiki hii Wayahudi pia wanasherehekea Passah ya kukumbuka kutoka utumwani nchini Misri.

Kama mwandishi wa Deutsche Welle wa Jerusalem, Bettina Marx, anavyoripoti, wiki nzima kabla ya Jumapili ya Pasaka, mji wa Yerusalem umejaa mahujaji wanaoomba katika lugha mbali mbali. Wakiwa ni peke yao au katika makundi wanatembeleakatika barabara nyembamba kati kati ya mji mkongwe wa Jerusalem na kuwafuata viongozi wao wa safari au mapadre au watawa.

Lengo kuu la mahujaji ni barabara ya “Via Dolorosa” ambayo inasemekana imetumiwa na Yesu Kristo kabla ya kusulubiwa. Baadhi kati yao pia wanabeba msalaba wa mbao, njiani mahujaji wanaimba. Kuna vituo 14 vya kukumbusha majonzi ya Yesu. Mwanzo ni ngome ya Antonia ambapo Pontius Pilatus alimkatia Yesu hukumu ya kifo. Mwisho wa njia ni kwenye kanisa la kaburi ambalo limejengwa pale Yesu Kristu aliposulubiwa na kuzikwa. Kanisa hilo linatumiwa na makanisa sita tofauti ya Kikristo.

Pale kumejengwa pia nyumba ya utawa ya Waethiopia. Watawa hawa wanatoka Marekani, Ujerumani na Uingeresa, anaeleza mmojawao aitwaye Kwillamariam: “Tumeanza kuomba Jumapili iliyopita. Wiki nzima tunaendelea kuomba. Waethiopia walikuwa wakiomba hapa mjini Yerusalem kwa muda mrefu. Hata mfalme wa Saba alikuja Yerusalem kuomba.”

Inatarajiwa kuwa kesho Jumamosi ya Pasaka kutakuja waumini wengi zaidi watakaotaka kuhudhuria sherehe ya moto mtakatifu katika kaburi la Yesu Kristu. Wengi wanasubiri usiku kucha. Katika miaka iliyopita kumetokea fujo, lakini sasa inabidi waumini wajipatie tiketi za kuingia.

Nchini Ujerumani katika mahubiri yao, maaskofu walitoa mwito kwa waumini wao kuimarisha upendo na ukaribu kati ya watu. Mwenyekiti wa kanisa la Protestani la Ujerumani, askofu Wolfgang Huber, alionya kutoingia hali ya kutojali matatizo ya kijamii. Kardinali wa mjini Cologne Joachim Meisner alikumbusha kuwa ujumbe wa Pasaka hasa ni kutia moyo binadamu.

Baba Mtakatifu Benedikt 16. anapanga kuongoza msululu kwenye njia ya msalaba mjini Rome ambayo ni maarufu kabisa kati ya waumini. Sherehe hiyo itatangazwa moja kwa moja na televisheni katika zaidi ya nchi 40 duniani. Pope huyu anatarajiwa pia kubeba msalaba wa mbao.

Katika kijiji kidogo nchini Philippines, watu saba walisulubiwa wakikumbuka kifo cha Yesu Kristo. Wanaume hawa saba walisulubiwa kwa kutumia misumari na kukaa kwenye misalaba kwa dakika tano. Halafu misumari zimetolewa tena. Maelfu ya waumini wamehudhuria tukio hilo ambalo limekosolewa na kanisa katoliki.

 • Tarehe 06.04.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHlG
 • Tarehe 06.04.2007
 • Mwandishi Maja Dreyer
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHlG
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com