Idlib- Mkoa wa Syria uliotengwa na dunia | Matukio ya Kisiasa | DW | 05.02.2020
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Idlib- Mkoa wa Syria uliotengwa na dunia

Huku akisaidiwa na Urusi rais wa Syria Bashar al Assad ameendelea kuwashambulia raia wa mkoa wa Idlib. Ingawa watu kwenye eneo hilo wanatamani kukimbilia nchi jirani ya Uturuki lakini imefunga mipaka yake ili kuwazuia.

Huku akisaidiwa na Urusi, rais wa Syria Bashar al Assad bila ya kujali ameendeleza mashambulizi ya mabomu kwa raia wa mkoa wa Idlib. Ingawa watu kwenye eneo hilo wanatamani kukimbilia nchi jirani ya Uturuki lakini imefunga mipaka yake ili kuwazuia.

Video iliyoonekana kwenye ukurasa wa twitter wa raia wa Syria, Mustafa Dahnon ilimuonyesha akisema "Watu wa Idlib wanaweza ama kubaki na kushuhudia kifo kikiwajilia ama wanaweza kujaribu kuvuka mpaka wa Uturuki kwa matumaini ya kupata mahala salama na maisha bora".

Video hiyo ilipigwa mwishoni mwa wiki iliyopita wakati maelfu ya watu walikuwa wamekusanyika katika mpaka wa Syria na Uturuki wakiwa na mabango yaliyokuwa na kaulimbiu iliyosema "Kutoka Idlib hadi Berlin" ili kuikumbusha jumuiya ya kimataifa kutambua kilio chao na kuchukua hatua za kuwasaidia. Watu waliokusanyika hapo walihisi kama ulimwengu umewatenga.

Majeshi yenye nguvu ya rais wa Syria Bashar al Assad

pamoja na washirika wake Urusi kwa miezi miwili yamekuwa yakiwashambulia raia wa Idlib. Mkoa huo ulioko kaskazinimagharibi mwa Syria ni eneo la mwisho linalodhibitiwa na waasi na wenye itikadi kali. Lakini Assad anataka kulibadilisha hilo.

Watoa huduma za tiba wanasema hakuna tena vituo vya afya vilivyosalia kwenye mkoa huo. Wakati hospitali ya Ariha iliposhambuliwa katika siku za karibuni takriban raia 10 waliuawa. Wanasema hawawezi kutembea mwendo mrefu kutafuta huduma hizo kwa kuwa wanaweza ama kukabiliwa na kitisho kikubwa zaidi ama hata kufa wakiwa njiani.

Assad na mshirika wake Urusi walijiwekea mkakati wa kulirejesha eneo hilo la mwisho linalodhibitiwa na waasi wa Hayat Tahrir al-Sham, lakini pia kuliangamiza kabisa kundi hilo. Kulingana na mwakilishi maalumu wa Marekani katika vita hivyo vya Syria James Jeffrey Urusi na Syria wamerusha mabomu zaidi ya 200 wakiwalenga raia katika kipindi cha siku chache zilizopita.

Türkei Präsident Erdogan

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan

Baadhi wanaliona shambulizi hilo kama ishara ya Urusi kwa Uturuki kwamba inatakiwa kujizuia katika operesheni inazozifanya nje ya mipaka yake lakini Erdogan anajichukulia kama mdhamini wa vikosi vya waasi wa Syria, hii ikiwa ni kulingana na mkurugenzi wa wakfu wa Heinrich Böll ulioko Instanbul wenye mahusiano na chama cha Kijani cha nchini Ujerumani, Kristian Brakel.

Uturuki inayounga mkono majeshi ya waasi mkoani Idlib hivi karibuni ilishambulia vituo 12 vya ufuatiliaji wa usitishwaji wa mapigano vilivyoko kwenye mkoa huo. Wizara ya ulinzi ya Uturuki imesema mashambulizi hayo ya karibuni ya Urusi dhidi ya ujumbe wa Uturuki yamesababisha vifo vya wanajeshi wake watano na mkandarasi mmoja wa kiraia aliyeandamana nao.

Uturuki nayo ililipiza kisasi cha mashambulizi hayo na baadae rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alidai kwamba yaliwaua wanajeshi wa Syria wapatao 35. 

Lakini pia amesema Uturuki inajihusisha na vita vya Idlib kwa kuwa nayo inataka nafasi katika meza ya mazungumzo wakati mustakabali wa Syria utakapokuwa unajadiliwa.

Walakini "wasiwasi mkubwa wa Erdogan ni kwamba Wasyria waliokata tamaa kabisa wanaweza kujaribu kukimbilia Uturuki kutokana na mshambulizi ya Assad," anasema Brakel. Kulingana na Umoja wa Mataifa watu wapatao 390,000 wameikimbia Idlib tangu mapema mwezi Disemba 2019. Kwa ujumla watu 750,000 wanaaminika kukimbia Idlib miezi tisa iliyopita huku ukionya kuhusu mzozo unaonyemelea wa kibinaadamu.