1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idadi ya vifo vya COVID-19 duniani yapindukia milioni 3

Grace Kabogo
18 Aprili 2021

Idadi ya watu waliokufa duniani kutokana na ugonjwa wa COVID-19 imepindukia milioni tatu kufikia Jumamosi, licha ya kampeni ya chanjo dhidi ya ugonjwa huo ikiendelea kushika kasi.

https://p.dw.com/p/3sBRK
Coronavirus - Intensivstation in Berlin
Picha: Christophe Gateau/dpa/picture alliance

Kwa mujibu wa takwimu za shirika la habari la Ufaransa, AFP zaidi ya vifo 12,000 duniani kote viliripotiwa kila siku katika muda wa wiki moja iliyopita na kupindukia vifo milioni tatu kufikia Jumamosi.

Janga hilo halionyesha dalili ya kupunguza makali yake, huku watu 829,596 wakiambukizwa virusi vya corona siku ya Ijumaa pekee, idadi hiyo ikiwa ya juu zaidi kwa watu kuambukizwa kwa siku moja.

Mji mkuu wa India, New Delhi siku ya Jumamosi ulizifunga shughuli zake za umma baada ya kurekodi visa vipya 234 vya corona pamoja na vifo 1,341.

Ufaransa yatangaza karantini kwa watu kutoka nchi kadhaa

Nayo Ufaransa imetangaza kuwa nchi hiyo itaweka masharti kwa watu wanaowasili nchini humo kutoka Argentina, Brazil, Chile na Afrika Kusini kukaa karantini ya lazima kwa siku 10 kufuatia wasiwasi wa aina mpya ya kirusi cha corona.

Ndege kutoka mataifa hayo hazitapigwa marufuku, lakini abiria wanaotokea nchi hizo watatakiwa kukaa karantini la sivyo wakabiliwe na faini.

Frankreich Passagiere im Flughafen Nice Cote d'Azur
Abiria katika uwanja wa ndege wa Nice Cote d'Azur, UfaransaPicha: Lionel Urman/abaca/picture alliance

Ufaransa imetetea uamuzi wake wa kutopiga mafuruku safari za ndege kutoka mataifa matatu ya Argentina, Chile na Afrika Kusini kwa kusema aina mpya ya kirusi kilichopatikana katika nchi hizo haijafikia kiwango cha kutisha kama kilichoshuhudiwa nchini Brazil.

Hatua hizo mpya za karantini zitaanza kutekelezwa hatua kwa hatua katika siku zijazo hadi zitakapotekelezwa kikamilifu kufikia Jumamosi ijayo. Hivi karibuni, Ufaransa iliimarisha vikwazo vyake vya kupambana na wimbi la tatu la virusi vya corona.

Uingereza ambayo tayari imetoa chanjo kwa asilimia 60 ya raia wake angalau kwa dozi ya kwanza, sasa inarekodi takriban vifo 30 kwa siku kutoka vifo 1,200 vilivyokuwa vikirekodiwa mwishoni mwa mwezi Januari.

Mapema Jumamosi, Uhispania iliongeza muda wa karantini ya lazima kwa abiria wanaowasili kutoka katika nchi 12 za Amerika Kusini na Afrika, zikiwemo Brazil na Afrika Kusini.

Siku moja baada ya Italia kutangaza kupunguza sehemu ya hatua zake za kukabiliana na kuenea kwa virusi vya corona katika shule na mikahawa kuanzia Aprili 26, wafanyakazi kwenye tasnia ya burudani waliandamana siku ya Jumamosi mjini Roma wakitaka msaada zaidi wa serikali. Pia wanataka kutangazwa rasmi tarehe ya kufunguliwa tena kwa kumbi za sanaa nchini humo.

Ibada ya kuwakumbuka waliokufa Ujerumani

Wakati huo huo, siku ya Jumapili Ujerumani itafanya ibada maalum ya kitaifa kuwakumbuka takriban watu 80,000 waliokufa kwa ugonjwa wa COVID-19.

Kansela Angela Merkel na Rais Frank-Walter Steinmeier wataungana na waumini katika Ibada itakayofanyika kwenye Kanisa la kumbukumbu la Kaiser Wilhelm mjini Berlin. Baadae viongozi hao watahudhuria hafla katika jumba la tamasha la Berlin ambapo Rais Steinmeier atahutubia.

Berlin | Angela Merkel und Frank-Walter Steinmeier
Rais Frank-Walter Steinmeier na Kansela Angela Merkel Picha: Getty Images/AFP/J. MacDougall

Matukio ya Jumapili yanafanyika wakati ambapo maafisa wa afya wa Ujerumani wameonya kuwa watu wengi wataathiriwa na virusi vya corona, wakati nchi hiyo ikipambana kukabiliana na wimbi baya la tatu.

Mapema Jumapili, taasisi ya kudhibiti magonjwa ya kuambukiza nchini Ujerumani, Robert Koch imethibitisha visa vipya 19,185 vya virusi vya corona na kuifanya idadi jumla ya mamabukizi nchini humo kufikia 3,142,262.

Taasisi hiyo pia imerekodi vifo vipya 67 vya COVID-19 na kuongeza idadi ya waliokufa kwa virusi hivyo kufikia 79,914.

Soma zaidi: Ujerumani yataka hatua kali kuzuia wimbi la tatu la COVID-19

Israel kwa upande wake imetangaza kuondoa amri ya kuvaa barakoa nje kuanzia siku ya Jumapili.

Hali hiyo jumla inaonyesha jinsi janga la virusi vya corona linavyoendelea kuitikisa dunia tangu kisa cha kwanza cha virusi hivyo kiliporipotiwa kwa mara ya kwanza nchini China mnamo Desemba 2019.

Zaidi ya watu milioni 139 wameambukizwa virusi vya corona duniani kote huku janga hilo likiathiri pakubwa uchumi wa ulimwengu.

Afrika na chanjo za COVID-19

Hayo yanajiri wakati ambapo nchi za Afrika zimekuwa zikiendelea kuwachanja watu wake dhidi ya COVID-19 kwa wiki sasa, lakini maendeleo yanaonekana taratibu. Matatizo ya ugavi, mkanganyiko kuhusu ratiba za chanjo na hofu ya madhara ya chanjo hizo zimekuwa zikisababisha ucheleweshaji huo.

Uganda Coronavirus Impfung
Muuguzi akijiandaa kutoa chanjo ya virusi vya corona Kampala, UgandaPicha: Luke Dray/Getty Images

Hata hivyo, Kituo cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa barani Afrika, CDC kimeonya kuwa chanjo zinazosambazwa barani Afrika kupitia mpango wa kimataifa wa COVAX, wa kununua na kusambaza chanjo za bure kwa nchi maskini zaidi duniani unaoungwa mkono na Shirika la Afya Duniani, WHO hazitatosha kulidhibiti janga la virusi vya corona.

WHO imesema kuwa hadi sasa chini ya asilimia 2 ya chanjo ulimwenguni, zimetolewa katika bara la Afrika.

Mkuu wa Kituo cha Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya barani Afrika, APHRC Dk. Catherine Kyobutungi amesema nchi za Afrika kwa ujumla ziko nyuma, hali inayokatisha tamaa.

Kyobutungi amesema kila nchi inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ingawa tatizo moja kubwa linabakia kuwa nchi masikini zinapata chanjo kidogo.

Libya kwa upande wake imeanza zoezi la kutoa chanjo kwa wananchi wake siku ya Jumamosi, huku ikitoa kipaumbele kwa wazee na wafanyakazi wa huduma za afya.

(AFP, AP, DW https://bit.ly/3x6HcEb)