Hatima ya Bafana Bafana na Misri kuamuliwa keshona alhamisi. | Michezo | DW | 16.06.2009
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Michezo

Hatima ya Bafana Bafana na Misri kuamuliwa keshona alhamisi.

Kombe la mashirikisho-Afrika Kusini:

default

Watazamaji kupata tiketi za bure kwa C-cup ?

Kombe la mashirikisho -Confederations Cup,linalofungua pazia kwa Kombne lijalo la Dunia nchini Afrika Kusini, leo ni mapumziko baada ya changamoto za jana kabla ya kesho wenyeji-Bafana Bafana kufungua duru ya pili kati yao na New Zealand-mpambano utakaoamua hatima yao.Spain, mabingwa wa Ulaya waweza kesho kuwatimua mabingwa wa Asia-simba wa Mesopotemia-Iraq na kukata tiketi yao ya nusu-finali.

Misri,mabingwa wa Afrika , wapeleka malalamiko kwa FIFA juu ya uamuzi wa rifu wa kumtimua nje mchezaji wao na kuwaadhibu kwa mkwaju wa penalty ulioipa Brazil jana bao la ushindi na mafiraouni waliowatoa jasho wabrazil wametishia huenda wakaigomea mechi yao na Itali hapo alhamisi.

Kocha wa bafana Bafana-Afrika kusini Joel Santana,amesema anaitazamia New Zealand kutoa ubishi mkali katika mpambano wa kufa-kupona kwa kila moja ya timu hizi mbili.Afrika kusini walimudu sare tu nyumbani na Iraq juzi wakati New Zealand walichezeshwa kindumbwe-ndumbwe na mabingwa wa ulaya Spain na kuzabwa mabao 5-0.Ushindi tu kesho utawaokoa wenyeji Bafana Bafana; na kocha Santana amewaonya watoto wake kutowadharau "All whites"-Timu ya taifa ya New Zealand.Katika kundi hili,mabingwa wa Ulaya Spian wanaongoza kileleni kwa pointi 3 kabla ya kuteremka tena kesho uwanjani kwa miadi yao na simba wa mesopotemia.

Jana mabingwa wa Kombe hili la mashirikisho walitolewa jasho kali na mabingwa wa Afrika-mafiraouni Misri.Ni bao la mkwaju wa penalty la jogoo lao Kaka lililowaokoa dakika ya mwisho mabingwa hao.

Misri,lakini bado inabisha hukumu ya mwisho ya mpambano wa jana na imepeleka rasmi malalamiko yake kwa FIFA juu ya jinsi rifu alivyoamua kumtimua nje mchezaji wake Al Muhamadi kwa unawa mpira langoni. Rais wa Shirikisho la dimba la Misri Samir Zaher, ameliambia shirika la habari la Ujerumani -DPA- kuwa Misri haitacheza na waazuri -mabingwa wa dunia-Itali alhamisi hii ikiwa haikupatiwa kwanza jibu na FIFA.

Heba ya dimba ya afrika imo hatarini ikiwa mabingwa hao wa Afrika watawakwepa mabingwa wa dunia-Itali hapo Alhamisi.Kocha wa mafiraouni mzee Hassan Shehata,alidai kuwatoa jasho wabrazil kama Misri ilivyofanya jana ni ushahidi kuwa timu za Afrika ni imara.

Wakati Misri katika miadi yake hiyo na Itali, wanahitaji ushindi kusalia mashindanoni,mabingwa wa dunia Itali, wakiongozwa na kocha wao Marcello Lippi wanataka kuifuata Spain nusu-finali endapo wakiwatimua nao nje mafiraouni kabla miadi na Brazil. Kaka,stadi wa Brazil, amewaonya wenzake wakifanya uzembe kama jana mbele ya Misri,watakiona kilichomtoa kanga manyoya.

Muandishi: Ramadhan Ali

Mhariri: Mohammed Abdul Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com