1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hamid Karzai aitaja Iran kuwa rafiki, Marekani ina mashaka

Sekione Kitojo6 Agosti 2007

Rais wa Afghanistan Hamid Karzai yuko ziarani nchini Marekani leo Jumatatu na anatarajiwa kukamilisha mazungumzo na rais George W. Bush yatakayohusu hali inayozidi kuporomoka ya kiusalama nchini humo na pia kutamka na kuwashangaza wengi nchini Marekani kwa kuitaja Iran nchi inayoangaliwa kuwa ni hasimu mkubwa wa Marekani , kuwa ni rafiki mkubwa badala ya adui.

https://p.dw.com/p/CH9z
Rais Bush akitembea na rais Hamid karzai katika eneo la Camp David kabla ya mazungumzo yao.
Rais Bush akitembea na rais Hamid karzai katika eneo la Camp David kabla ya mazungumzo yao.Picha: AP

Wapiganaji wa Taliban wamesema kuwa rais wa Afghanistan Hamid Karzai na rais wa Marekani George W. Bush , wanaokutana Camp David leo Jumatatu, wanapaswa kutoa uamuzi wa kuwaacha huru waasi walioko kifungoni ama watawajibika na vifo vya mateka 21 raia wa Korea ya kusini.

Kitisho hicho cha wapiganaji wa Taliban kinakuja wakati majadiliano ya kuwaacha huru waasi hao yamekwama na hakuna hata makubaliano ya wapi yafanyike mazungumzo baina ya wateka nyara hao na wanadiplomasia wa Korea ya kusini. Ubalozi wa Korea ya kusini umesema leo kuwa unamatumaini makubwa na mazungumzo ya ana kwa ana na wapiganaji wa Taliban nchini Afghanistan, ambapo mmojawao alifanikiwa kuzungumza na wapatanishi.

Wataliban wamekwisha wauwa wawili kati ya mateka hao na wamekuwa mara kwa mara wakitoa vitisho , kuwauwa mateka waliobaki wanawake 18 na wanaume watatu hadi pale serikali ya Afghanistan itakapokubali kuwaacha huru waasi walioko kifungoni.

Karzai akiwa nchini Marekani inawezekana atachukua maamuzi mazito pamoja na rais Bush kwa kubadilishana wafungwa , kwasababu , Bush na Karzai wanawajibu wa kupata kuachiliwa kwa mateka hao, msemaji wa Taliban Qari Mohammed Yousuf ameliambia shirika la habari la Reuters kwa simu kutoka katika eneo ambalo halikutambulika.

Pamoja na mada hiyo kuu, lakini marais hao wanatarajiwa pia kuzungumzia suala la biashara ya madawa ya kulevywa, na maendeleo ya kiuchumi nchini humo.

Lakini Karzai, ambaye aliingia madarakani mwaka 2002 akiungwa mkono na Marekani, aliingiza kiwingu katika mazungumzo hayo hata kabla ya kuanza, baada ya kusema kuwa Iran ni rafiki, nchi ambayo inaonekana na Marekani kuwa inaleta kitisho kwa amani na dunia. Katika mahojiano yaliyotangazwa jana Jumapili, Karzai alionekana kukanusha madai ya Marekani kuwa silaha za Iran zinasaidia kuporomosha hali ya usalama nchini Afghanistan.

Matamshi yake hayo yanakwenda kinyume kabisa na msimamo wa Marekani, ambao unaiona Iran kuwa nchi korofi ambayo inatoa msaada wa fedha na silaha kwa magaidi nchini Afghanistan na Iraq na pia ikiwa na nia ya kutengeneza silaha za kinuklia.

Msimamo wa Marekani hata hivyo ulisisitizwa tena na waziri wake wa mambo ya kigeni Condoleezza Rice wakati akitetea uamuzi wa nchi yake wa kuuza silaha zenye thamani ya mabilioni ya dola kwa Saudi Arabia na mataifa mengine ya ghuba ili kuzuwia nia ya Iran.