Hali ya wasi wasi yaongezeka katika Rasi ya Korea | Matukio ya Kisiasa | DW | 24.05.2010
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Hali ya wasi wasi yaongezeka katika Rasi ya Korea

Wasi wasi huo umeongezeka baada ya Korea Kaskazini kutishia kuvishambulia vipaza sauti vya Korea Kusini katika eneo la mpaka.

default

Meli ya kijeshi ya Korea Kusini ya Cheonan inayodaiwa kuzamishwa na Korea Kaskazini.

Hali ya wasi wasi imezidi kuongezeka kati ya Korea Kusini na Korea Kaskazini, baada ya Korea Kaskazini kutishia kuvishambulia vipaza sauti vya Korea Kusini vinavyoeneza propaganda kuwa Korea Kaskazini iliizamisha meli ya jeshi la majini la Korea Kusini na kuwaua mabaharia 46. Mapema leo, Korea Kusini ilitangaza kulipiza kisasi baada ya uchunguzi wa kimataifa kuonyesha kuwa manowari ya Korea Kaskazini ilifyatua kombora lililosababisha kuzama kwa meli moja ya jeshi la majini la Korea Kusini mwezi Machi, mwaka huu.

Waziri wa Ulinzi wa Korea Kusini, Kim Tae-Young alisema kuwa matangazo hayo yaliyosimamishwa mwaka 2004, sasa yataanza tena katika eneo la mpaka ambalo lina mvutano. Hata hivyo, Korea Kaskazini imekanusha kuhusika na madai hayo ya kuizamisha meli hiyo na kutishia kuanzisha vita iwapo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake. Taarifa iliyotolewa na jeshi la nchi hiyo imeeleza kuwa kauli mbiu za propaganda zimeanza kutumika katika eneo hilo la mpaka na kwamba jeshi la Korea Kusini lilikuwa linaelekea kuweka vipaza sauti.

Tayari Korea Kusini imetangaza vikwazo vipya  dhidi ya nchi hiyo jirani ya Korea Kaskazini. Vikwazo hivyo ni pamoja na kusitisha biashara kati ya nchi hizo mbili, uwekezaji na kuzuia meli za Korea Kaskazini kuingia Korea Kusini. Akizungumza katika televisheni ya taifa, Rais wa Korea Kusini, Lee Myung-Bak aliwatolea mwito viongozi wa Korea Kaskazini kuiomba radhi haraka nchi hiyo pamoja na jumuiya ya kimataifa, ili kurejesha uhusiano baina ya nchi hizo mbili katika hali ya kawaida. Rais Lee alisema ataliwasilisha suala hilo kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Baadhi ya wachambuzi wanaamini kuwa nchi mojawapo ya Korea itajiingiza katika vita.

Kwa upande wake Rais Barack Obama wa Marekani ameunga mkono hatua zilizochukuliwa na Korea Kusini na ameahidi kuwa nchi yake itaipa nchi hiyo ushirikiano katika kukabiliana na uchokozi wa aina yoyote katika siku zijazo. Aidha, Ikulu ya Marekani imeitaka Korea Kaskazini kuacha tabia yake ya vitisho wakati ambao kuna hali ya wasi wasi mkubwa katika rasi ya Korea. Marekani ambayo ina wanajeshi 28,000 katika rasi ya Korea inaiunga mkono moja kwa moja Korea Kusini.

Wakati huo huo, serikali ya Japan inafikiria kuiwezeka Korea Kaskazini vikwazo vikali baada ya nchi hiyo kushutumiwa kwa kuizamisha meli ya Korea Kusini. Shirika la habari la Japan, Kyodo limeeleza kuwa Waziri Mkuu wa Japan, Yukio Hatoyama amelitaka baraza lake la mawaziri kufikiria uwezekano wa kuiwekea vikwazo Korea Kaskazini. Kwa mujibu wa shirika hilo la habari, Japan inaiunga mkono Korea Kusini. Mwezi Aprili, Japan iliongeza kwa mwaka mmoja zaidi vikwazo vya kibiashara ilivyoweka mwaka 2006 dhidi ya Korea Kaskazini, baada ya nchi hiyo kufanya jaribio la kwanza la kinyuklia. Vikwazo hivyo ni pamoja na kuzuia kuingiza Japan bidhaa kutoka Korea Kaskazini na kukizuia kivuko pekee kilichopo kati ya mataifa hayo mawili.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (AFPE/RTRE/DPAE)

Mhariri:Othman Miraji

 • Tarehe 24.05.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/NVcH
 • Tarehe 24.05.2010
 • Mwandishi Kabogo Grace Patricia
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/NVcH

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com